Home Michezo Kimataifa Cesc Fabregas na hadithi ya Said Ndemla

Cesc Fabregas na hadithi ya Said Ndemla

859
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza, kiungo wa Simba, Said Ndemla, licha ya uwezo wake mkubwa, aliona alikuwa hapati nafasi hali iliyosababisha baadhi ya wadau wengi wa soka kuanza kuhoji nini kimetokea.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa kwa sasa Simba imesheheni hasa katika idara ya kiungo, lakini kitendo cha Ndemla kukosekana mara kwa mara hata benchi kulisababisha maswali mengi mpaka pale Kocha wa Simba, Joseph Omog, alipoanza kumtumia baadhi ya michezo.

Ndemla alianza kusugulishwa benchi msimu uliopita alipokuja Jackson Mayanja, ndiyo maana hata msimu huu kiungo huyo alipokuwa mtokea benchi lawama zilianza kumwendea kocha huyo kwamba ndiye anayeteketeza kipaji hicho.

Hata hivyo, roho za mashabiki wa Ndemla zimeanza kurejea kwenye hali zao za kawaida, kwani ameanza kutumika na jambo zuri ni kwamba anapopewa nafasi anaonyesha uwezo mkubwa.

Kilio kilekile ambacho walikuwa wakiiiangua mashabiki wa Ndemla, ndicho hichohicho wanachokililia mashabiki wa Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu nchini England, hasa wale wanaomhusudu kiungo Cesc Fabregas.

Fabregas ambaye alikuwa akiitwa Pass Master, ndiye ambaye kwa sasa anasugulishwa benchi na Kocha Antonio Conte, mara kwa mara kiungo huyo mwenye uraia wa Hispania, ambapo ameonekana hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Katika michezo mitano ambayo Chelsea wamekwisha kucheza mpaka sasa, Cesc Fabregas hajaanza katika mchezo wowote kati yote hiyo na katika mchezo dhidi ya Liverpool waliopoteza kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, kiungo huyo aliingia dakika za lala salama na kuonyesha kiwango kikubwa.

Fabregas, ambaye miguu yake inapokuwa na mpira anajua wapi pa kuupenyeza ili ukalete madhara kwa wapinzani wao, ndiye ambaye leo hii anasubiri mpaka wenzake wacheze wachoke au mmoja kati yao aumie ndipo apate nafasi.

Uzuri wa Fabregas ni kwamba akipata nafasi anamuumbua kocha wake, kwani anaonyesha kile ambacho mashabiki wanakijua kutoka kwake, ni kama ilivyo kwa Ndemla, ambaye anajua vema kutumia miguu yake ndani ya uwanja kocha anapokosea na kumpa nafasi.

Mpaka leo mashabiki wa Arsenal wanamkumbuka nahodha wao huyo wa zamani jinsi alivyowatendea mambo makubwa. Hata kama wakiambiwa leo hii Arsene Wenger amemsajili, wanaweza kumiminika uwanja wa ndege kwenda kumsubiria kwa vifijo na nderemo.

Mhispania huyo alipoondoka Arsenal mwaka 2011 kwenda nchini Hispania kuichezea Barcelona, mashabiki wa kikosi hicho hawakumuelewa kocha wao, walijiuliza maswali mengi sana kwamba kwanini aliruhusiwa kuondoka.

Hata Barcelona walipoachana naye wengi walidhani atarudi Arsenal na mashabiki wa kikosi hicho walijiaminisha kuwa kijana wao anarudi nyumbani, lakini kocha kama kawaida yake hakuona umuhimu mkubwa wa kumrejesha, akaamua kwenda Chelsea.

Fabregas kama ilivyo kwa Didier Kavumbagu wa Yanga ambaye aliwaambia wamuongezee mkataba kabla ya kwenda Azam FC, ndivyo Mhispania huyo alivyowaambia Arsenal kwamba angetamani kurudi wakati alipomalizana na Barcelona lakini ikashindikana.

Inawezekana Konte hajui umuhimu wa Fabregas ndani ya kikosi hicho, ndiyo maana mara kwa mara amekuwa akimuanzisha benchi, lakini huenda baadaye ataona umuhimu wake kadri siku zinavyokwenda.

Hata kama Konte ataendelea kumtumia Mhispania huyo kama mtokea benchi, bado ukweli utaendelea kubakia palepale kwamba kiungo huyo ni kati ya viungo bora kuwahi kutokea kwa misimu ya hivi karibuni.

Mtu bora ni bora tu hata kama utajaribu kuificha nyota yake. Nyota ya Fabregas bado inawaka mbele ya mashabiki, ndiyo maana wanatamani kuona akipewa nafasi. Ndiyo maana jina la Pass Master, bado halijapotea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here