Home Makala Cheki Messi anavyomtimulia vumbi Mbappe huko Ulaya

Cheki Messi anavyomtimulia vumbi Mbappe huko Ulaya

1513
0
SHARE

LONDON, England

NI wazi nahodha wa Barcelona, Lionel Messi, anaelekea kunyakua tena Kiatu cha Dhahabu ambacho hutolewa kwa mfungaji bora wa Ligi za Bara la Ulaya, tuzo itakayokuwa ya tano kwa upande wake.

Iwapo Messi atamaliza msimu huu na mabao mengi kuliko washambuliaji wote Ulaya, bila shaka kigezo kitakachotumika ni kile kile ambacho ni kuzidisha idadi ya mabao na uwiano wa viwango vya ligi husika.

Kwa mfano, La Liga ina uwiano wa 2.0 wakati ligi kama Eredivisie ya Uholanzi na Turkish Super Lig ya Uturuki zina uwiano wa 1.5, hivyo mabao yanapozidishwa na uwiano huo humpa straika pointi zitakazomfanikisha kubeba kiatu.

Zikiwa zimesalia mechi mbili kabla ya kumalizika kwa msimu wa Ligue 1, ni ngumu kutabiri kama straika wa PSG, Kylian Mbappe, atampiku Messi mwenye mechi moja, katika vita ya kuwania kiatu cha dhahabu.

Ukiwaacha Messi na Mbappe ambao wamekuwa wakifukuzana kwa kasi msimu huu, hii hapa orodha ya mafowadi wengine hatari kwa kuzifumania nyavu…

Luuk de Jong- 28 x 1.5= 42.0

Straika huyo wa zamani wa Newcastle Utd, amekuwa na msimu bora katika timu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi, ambako amefunga jumla ya mabao 28.

Tangu arejee nchini kwao, Luuk ameweza pia kuweka rekodi ya kufunga mabao 93 katika mechi 156 alizocheza kwenye Eredivisie.

Mo Salah- 22 x 2.0= 44.0

Akimaliza kama mfungaji bora namba tatu baada ya kupachika mabao 22, Salah aliweza kuwadhihirishia mashabiki wa Liverpool kwamba moto wake haukuwa wa mabua.

Salah kwa sasa anashikilia rekodi ya kushinda kiatu cha dhahabu kwa misimu miwili mfululizo ambayo pia ni ya kwanza tangu atue Liverpool huku akiwa amefunga mabao 54 katika mechi 74 za EPL alizoitumikia timu hiyo.

Sadio Mane- 22 x 2.0= 44.0

Nyota mwingine ambaye kama angekuwa na makali zaidi angeweza kuwa kwenye uwezekano wa kushinda kiatu cha dhahabu Ulaya ni mshambuliaji hatari wa Liverpool, Mane.

Hata hivyo, Mane hakutoka kapa EPL, kwani mabao yake 22 yalimpa kiatu cha dhahabu. Ubora wake wa kucheka na nyavu umemfanya avuke idadi ya mabao 10 aliyofunga EPL msimu wa 2017-18.

Aubameyang- 22 x 2.0= 44.0

Arsenal ilichelewa sana kuwa na Aubameyang. Pengine hata mashabiki wake wanalitambua hilo, Mgabon huyo amekuwa msaada mkubwa wa kupachika mabao ndani ya timu hiyo ambapo tangu atue Emirates ameweza kutikisa nyavu mara 32 katika mechi 49, mabao 22 yakiwa ni ya msimu huu pekee.

Akiwa ni mmoja wa washindi watatu wa kiatu cha dhahabu EPL msimu huu, Aubameyang, anatarajiwa kuendeleza moto wake msimu ujao kama alivyokuwa akifanya Borussia Dortmund ambako hadi anaondoka alifunga mabao 98 katika mechi 148.

Duvan Zapata- 22 x 2.0= 44.0

Licha ya kuitumikia Atalanta kwa mkopo akitokea Sampdoria, Mkolombia huyo hakutaka kukaa kizembe na msimu huu ameisaidia mno timu hiyo ambayo huenda ikacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Amekuwa akisakata soka Serie A tangu mwaka 2013, lakini Zapata hakuwahi kufikisha mabao 22. Mara ya mwisho kwake kufunga mabao mengi yalikuwa 11 tu.

Robert Lewandowski- 22 x 2.0= 44.0

Silaha hatari ya Bayern Munich, Lewandowski, imeendelea kuziumiza nyavu za timu pinzani huku akiwa na rekodi ya kufunga mabao pungufu ya 20 katika msimu mmoja tu tangu mwaka 2011.

Mabao yake 22 katika mechi 32 alizocheza msimu huu wa Bundesliga, yamemfanya Lewandowski awe mfungaji bora wa Bundesliga muda wote kwa wachezaji wasio Wajerumani.

Mbaye Diagne- 30 x 1.5= 45.0

Hili ni jina la kushtukiza zaidi katika orodha hii, kwani makali ya Msenegali huyo aliyezitumikia timu mbalimbali kwa mkopo akitokea Juventus, yameonekana zaidi msimu huu.

Uhamisho wake kutoka China hadi Uturuki mwaka 2017 haukutarajiwa kuwa wa nguvu kiasi hiki. Diagne anaumaliza msimu huu kibabe kwa kufunga mabao 20 katika mechi 18 alizoitumikia Kasimpasa na mengine 10 ameifungia timu ya Galatasaray ambao walimsajili Januari mwaka huu.

Fabio Quagliarella- 26 x 2.0= 52.0

Sampdoria ilishangaza wengi kwa kumwacha Zapata aende Atalanta kwa mkopo, lakini kumbe ilikuwa na imani kubwa kwa mkongwe, Quagliarella, ambaye licha ya umri wake mkubwa ameweza kufunga mabao mengi mno msimu huu kuliko miaka yote.

Kylian Mbappe- 30 x 2.0= 60.0

Tangu aoneshe maajabu yake katika fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, kinda huyo hatari wa Ufaransa ameendelea kuimarika zaidi na zaidi katika kikosi cha PSG.

Msimu huu ameweza kuifungia PSG mabao 30 na kunyakua taji la pili mfululizo la Ligue 1 (matatu jumla), huku akiwa na Kombe la Dunia katika umri wa miaka 20 tu.

Lionel Messi- 34 x 2.0= 68.0

Nani wa kumzuia fowadi huyo wa Kiajentina? Hasa akielekea kuumaliza msimu huu wa La Liga ambao amefunga mabao mengi zaidi (34 katika mechi 33) tangu msimu wa 2014/15 alipofunga mabao 43 katika mechi 38.

Kiwango chake cha kuzifumania nyavu kimeisaidia sana Barcelona kurudisha heshima yake msimu huu, lakini swali kubwa hapa ni hili, Messi, 31, ataweza kuendana na kasi ya Mbappe msimu ujao?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here