SHARE

LONDON, England


KWA mara ya kwanza tangu tuzo ya FIFA ya mchezaji bora wa kiume duniani, kuna jina jipya la Luka Modric.

Kiungo huyo wa klabu ya Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia, alifanikiwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka huu.

Ushindi ambao unampa nafasi Modric ya kuwa mchezaji wa tatu baada ya Cristiano Ronaldo kushinda mbili za awali tangu tuzo hiyo maarufu kama FIFA ‘The Best’ ilipoanzishwa mwaka 2017.

Sababu za Modric kuwagaragaza nyota wenzake mwaka huu ni mafanikio yake katika msimu uliopita wa 2017/18.

Kiwango alichokionesha msimu huo kimeonekana kuwa ni cha hali ya juu.

Aidha, kura alizopigiwa Modric zimedhihirisha kwamba kiungo huyo alifanya kitu cha ziada ingawa bado hakijajulikana wazi na ndio maana amezua hali ya kutoeleweka na wadau wengi.

Hiyo imechochewa zaidi na mambo makubwa ambayo Ronaldo na Lionel Messi wamekuwa wakiyafanya kila kukicha.

Ikumbukwe kuwa msimu wa Modric ulianza kwa kuzawadiwa Mpira wa Dhahabu baada ya Real Madrid kunyakua taji la Klabu Bingwa ya Dunia.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Modric alikuwa ni kama roho idundayo katika safu ya kiungo cha Madrid hadi wababe hao waliponyakua taji la michuano hiyo na kuweka rekodi ya kulibeba mara ya tatu mfululizo.

Kiungo huyo pia alifanya vitu vyake katika ngazi ya kimataifa kwa kutimiza majukumu mazito ya kuiwezesha timu yake ya taifa ifuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia.

Baada ya hapo, Modric alichukua jukumu jingine la kuibeba Croatia katika fainali zenyewe zilizofanyika nchini Urusi, akicheza soka la kiwango cha juu mno na kukonga nyoyo za wafuatiliaji wengi wa mchezo huo.

Kwa kiasi kikubwa Modric alibeba mzigo mkubwa wa kuibeba Croatia kwa kuzunguka huku na kule ndani ya uwanja, bila kuchoka wala kukata tamaa.

Modric alifunga mabao muhimu na kuonesha ubora wake katika suala la kuwaongoza wenzake.

Nyota huyo aliushikilia usukani wa Croatia hadi kutinga fainali waliyochuana na timu ya taifa ya Ufaransa.

Hadi anamaliza na fainali za Kombe la Dunia, Modric alifunga jumla ya mabao manne, pasi nane za mabao katika michuano yote na mataji matatu.

Lakini Modric alikuwa na wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha tuzo hiyo ya FIFA ‘The Best’.

Takwimu za Modric na za wapinzani wake hao zimetokea kuibua mijadala miongoni mwa mashabiki wa soka wanaohoji imekuwaje kiungo huyo aibuke mshindi?

Hebu jionee takwimu za wachezaji hawa ambao ndio wamekuwa midomoni mwa wengi kufuatia Modric kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo.

 

Ronaldo

 • Straika huyo alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita wa 2017/18, akiwa na Real Madrid.
 • Taji hilo lilifuata baada ya kunyakua jingine la Klabu Bingwa ya Dunia 2017.
 • Mreno huyo alimaliza msimu wa 2017/18 kama mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (mabao 15).
 • Jumla ya mabao yote aliyofunga katika michuano yote ya msimu uliopita ni 45 na pasi za mabao tisa. 

Lionel Messi

 • ‘Mchawi’ huyo wa Kiargentina alinyakua mataji mawili ya La Liga na Kombe la Mfalme Hispania msimu uliopita, akiwa na Barcelona.
 • Msimu huo ndio ambao Messi alifunga mabao 34 na kuwa mfungaji bora wa La Liga.
 • Aidha, nyota huyo alitoa pasi 12 za mabao katika msimu uliopita wa La Liga, akilingana na Pablo Fornals wa Villarreal na Luis Suarez. 

Kevin De Bruyne

 • Umuhimu wake katika kikosi cha Man City uliifanya klabu hiyo kunyakua taji la Ligi Kuu England kwa rekodi ya kutisha ya pointi nyingi zaidi.
 • Kiungo huyo alitisha kwa kutoa pasi 16 za mabao kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.
 • Aidha, De Bruyne aliweza kufunga jumla ya mabao 13 katika michuano yote.

Antoine Griezmann

 • Straika huyo wa Atletico Madrid ni mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa.
 • Griezmann alifunga moja ya mabao katika fainali ya michuano hiyo waliyocheza na Croatia.
 • Kiwango chake kilimpa tuzo za Kiatu cha Fedha na cha Shaba (Adidas)
 • Alimaliza fainali za Kombe la Dunia na mabao manne pamoja na pasi mbili za mabao.
 • Mafanikio hayo ya Kombe la Dunia yalifuata baada ya kubeba taji la Europa akiwa na Atletico Madrid
 • Huko kwenye Europa, Griezmann alifunga mabao sita na kutoa pasi mbili za mabao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here