SHARE

LONDON, England

MBIO za kumaliza zimefikia patamu baada ya Manchester United kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge.

Ushindi huo unaifanya Manchester United kuifunga Chelsea mechi mbili za Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika historia yao, mara ya mwisho walifanya hivyo mwaka 1988.

Chelsea ambao wapo nafasi ya nne, wamewazidi pointi tatu tu vijana wa Ole Gunnar solskjaer na kufufua matumaini makubwa ya kumaliza ndani ya ‘top four’ msimu huu.

Makala haya yanakuletea mambo matano yaliyotokea katika mchezo huo uliokutanisha vigogo wa soka la England ndani ya Uwanja wa Stamford Bridge.

KIWANGO CHA BRUNO FERNANDES

Manchester United walikuwa na kilio kikubwa kuhusu kiungo mwenye uwezo wa kuichezesha timu msimu huu. Scott McTominay na Nemanja Matic wanaweza kukaba na kuzuia, Fred ni mzuri zaidi kwa kuiunganisha timu kwa kazi yake kubwa anayoifanya uwanjani.

Lakini hakuna aliye na uwezo au kiwango kukaribia ubora wa kunyumbulika na kuichezesha timu kama Paul Pogba ambaye yupo nje kwa majeraha ya muda mrefu.

Bruno Fernandes anaweza kuwapa wanachokikosa kutoka kwa Pogba. Mchezaji huyo raia wa Ureno alicheza mchezo wake wa pili akiwa na jezi ya Manchester United na kuonesha kiwango cha juu.

Mikimbio yake, muda wote amekuwa akionekana na kutoa msaada kwa wenzie. Anapokuwa na mpira ni mwepesi, mwenye kujua wapi aupeleke, pia, ama uwezo wa kuisukuma timu kwenda mbele na mfungaji mzuri wa mabao anapopata nafasi hiyo.

Ni wazi Fernnades amekuwa msaada mkubwa kwa Manchester United katika michezo miwili aliyocheza. Pasi ya bao aliyoitoa kwa Harry Maguire inaonesha kuna mambo mengi yapok wake ambayo yatawasaidia Manchester United.

Unaweza kusema hajafanya jambo kubwa sana, kwani ameongeza ubunifu uliokosekana ndani ya kikosi hicho cha Solskjaer.

UMALIZIAJI MBOVU WA CHELSEA

Mambo yanaonekana kuwa tofauti kwa Chelsea ambao kikosi chao kimezungukwa na vijana wadogo kama Fikayo Tomori, Mason Mount, Tammy Abraham na Reece James, uwezo wao wa kuamua matokeo umekuwa mdogo hasa katika Uwanja wa Stamford Bridge.

Juzi, walionesha udhaifu mkubwa katika eneo la mwisho, hawakuwa makini kuzibadili nafasi zao kuwa mabao. Straika Michy Batshuayi ambaye alianza katika mchezo huo alishindwa kuonesha uwezo mkubwa mbele ya lango la wapinzani hao.

Straika huyo raia wa Ubelgiji alikosa nafasi mbili za wazi. Nafasi ambazo zingeweza kuwazamisha Manchester United katika mchezo huo. Mpaka mechi hiyo inamalizika, Chelsea walipiga mashuti 17, lakini ni moja tu lililenga lango la wapinzani wao.

Chelsea walionesha udhaifu mkubwa katika eneo la ushambuliaji, labda kukosekana kwa mfungaji bora wa timu hiyo, Abraham ilichangiwa kufanya vibaya, lakini ilikuwa fursa kwa wengine kuonesha uwezo wao na kumshawishi Frank Lampard kuwapa nafasi zaidi.

KUREJEA KWA ERIC BAILLY

Msimu mzima, mabeki wa kati walikuwa wakicheza Victor Lindelof na Harry Maguire. Kwa kiasi fulani, kombinesheni yao ilionekana nzuri sababu ya uwezo wa kila mmoja wao, lakini hawakuwa na ubora mkubwa kwa pamoja.

Mabeki wanafanana kiuchezaji, hawana kasi kubwa ya kuziba nafasi. Wote huonekana bora wanacheza sambamba na mtu mwenye kasi na uwezo wa kuziba makosa na nafasi.

Kama Eric Bailly. Beki huyo raia wa Ivory Coast alicheza mchezo wake wa kwanza msimu huu baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeraha.

Bailly alionesha kiwango kikubwa, macho ya mashabiki wa Manchester United yalimshuhudia mchezaji ambaye alikuwa na kasi kubwa, aliondoa hatari zote na kuficha makosa ya Maguire ambaye alifunga bao la pili.

Katika mfumo wa mabeki watatu, Bailly alicheza kulia karibu na Aaron Wan-Bissaka, aliifanya kazi yake vizuri na kuifanya United wamalize mchezo bila kuruhusu bao.

Kama beki huyo akiwa fiti, ataongeza ubora katika idara ya ulinzi ya Manchester United ambao ulikosekana kwa muda mrefu.

VAR KAMA KAWA

Imekuwa kawaida kwa wafuatiliaji wa Ligi Kuu England kuizungumzia Teknolojia ya Video kwa Mwamuzi (VAR). Wapo wanaoifurahia na kuchukia pale maamuzi yanapotolewa. Huku kukiwa na maoni ya kuwekwa video ambazo zitamuwezesha mwamuzi wa kati kuona na kufanya maamuzi kuliko kusikia kutoka kwa wengine.

Wakati mwingine mambo yanaweza kwenda tofauti, kama ilivyokuwa kwa Chelsea ndani ya Stamford Bridge. Vijana wa Lampard wanaweza kuilaumu VAR katika kipigo hicho walichokipata.

Kwanza, iliruhusu Maguire kuendelea kucheza licha ya kumchezea vibaya straika Batshuayi, asilimia kubwa wanaamini beki huyo wa Manchester United alistahili kuoneshwa kadi nyekundu.

Bahati mbaya, Chelsea walipata maumivu mara mbili sababu Maguire ambaye alitakiwa kutolewa kwa kadi nyekundu alifunga bao la pili ambalo liliwapa Manchester United matumaini makubwa ya kushinda mechi hiyo

Unaweza kusema beki wa Chelsea, Kurt Zouma alifunga bao safi. Lakini lilikataliwa kutokana na makosa yaliyofanya na Cesar Azpilicueta kumsukuma mchezaji wa wapinzani wao.

Pia, straika Olivier Giroud alifunga bao kwa kichwa, lakini lilikataliwa baada ya picha za marudio kuonesha akiwa amezidi sehemu ya mguu wake kabla ya kufunga. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here