Home Michezo Kimataifa CHELSEA WAPEWA SIRI YA AUBAMEYANG NA MORATA

CHELSEA WAPEWA SIRI YA AUBAMEYANG NA MORATA

517
0
SHARE

LONDON, England

CHELSEA ni kama bado wana mawenge ya kumkosa Romelu Lukaku aliyebadili gia angani na kutua Manchester United.

Mpaka sasa tajiri Roman Abramovich ameshapelekewa majina ya mastraika watatu ofisini kwake, lakini kimbembe kinakuja ni nani bora ili afunge naye mkataba.

Yumo kijana wa Real Madrid, Alvaro Morata, mkali wa mabao wa Juventus, Gonzalo Higuain na mfungaji bora wa Bundesliga msimu uliopita, Piere Emerick Aubameyang.

Kufuatia sintofahamu hii, beki wa zamani wa klabu hiyo, Marcel Desailly, ameibuka na kutoa ushauri wake kwa benchi la ufundi la Chelsea, lililo chini ya Antonio Conte.

Desailly anaamini straika pekee anayewafaa Chelsea msimu ujao ni ‘batman’ kutoka Dortmund, Pierre Aubameyang.

Akizungumza na jarida moja la nchini Ufaransa, Desailly alisema: “Lukaku lilikuwa chaguo la kwanza kwa Chelsea, hili halina ubishi. Ana nguvu na uwezo mkubwa wa kuuficha mpira.

“Lakini kwa sasa nafikiri Aubameyang ni chaguo sahihi zaidi. Kasi yake ni kitu muhimu kwa Chelsea kama akipangwa na Eden Hazard pale mbele.

“Sidhani kama Morata ni chaguo sahihi kwa Chelsea. hana kasi sana na si mzuri hasa kwa matumizi ya nguvu kwa mabeki wabishi kama wa Premier.

“Kwangu Aubameyang ni chaguo sahihi. Bei yake ni kawaida na ni mtu mzuri kwa mfumo wa Conte,” alishauri Desailly.

Lakini beki huyo wa Ufaransa, aliongeza kuwa Conte anaweza kukaa chini ya Diego Costa kwa ajili ya kuzungumza naye na kumaliza tofauti zao.

“Kuongea na Costa pia ni wazo zuri. Ni mtu muhimu sana kwa mashindano ya Ulaya msimu ujao, Chelsea ni lazima wawe na mtu wa aina ile. Kiongozi wa safu ya ushambuliaji. Kama watachagua kuzungumza naye ni jambo sahihi pia,” aliongeza Desailly.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here