Home Michezo Kimataifa CHELSEA YAIBAMIZA ARSENAL 3-1 DARAJANI, SASA UBINGWA WASHINDWE WENYEWE

CHELSEA YAIBAMIZA ARSENAL 3-1 DARAJANI, SASA UBINGWA WASHINDWE WENYEWE

489
0
SHARE

LONDON, England

KAMA kuna mtu ataendelea kubisha kuwa Chelsea si mabingwa wa Premier League msimu huu, basi kesho mapema sana atahitajika Central Polisi kutoa maelezo ya kina.

Jana kwenye dimba la Stamford Bridge, Chelsea walikata ngebe za Washika mitutu wa jiji la London, Arsenal kwa kuwatandika bao 3-1 bila huruma na kujikita kileleni kwa pointi 59.

Chelsea walionekana kupania pointi tatu kwenye pambano hilo baada ya kuanza kulisakama lango la Arsenal kama nyuki kwenye dakika 15 za kipindi cha kwanza.

Mashambulizi hayo yaliyokuwa yakipitia kwenye wingi za pembeni, yalizaa matunda dakika ya 13 baada ya mlinzi wa kushoto, Marcos Alonso, kupachika bao la kuongoza kwa kichwa.

Alonso alifunga bao hilo akiumalizia mpira uliogonga mwamba baada ya Diego Costa kupiga kichwa wakati akiunganisha krosi iliyochongwa na Pedro.

Mlinzi wa kulia wa Arsenal, Hector Bellerin, alipata majeraha ya kichwa wakati akijaribu kumzuia Alonso na kupelekea kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Gabriel Paulista.

Baada ya mabadiliko hayo, Arsenal walionekana kurudi kwenye mchezo wakimiliki mpira kwa asilimia kubwa katikati ya uwanja.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Chelsea walitoka uwanjani kifua mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Chelsea wakionekana kupania zaidi kutafuta bao la pili.

Na kwenye dakika ya 53 ya mchezo, Eden Hazard, aliyecheza akiwa na maumivu ya kifundo cha mguu, alipachika bao la pili baada ya kuichambua beki ya Arsenal na kupiga shuti kali lililomshinda Petr Cech.

Baada ya bao hilo, Chelsea wakaonekana kutulia na kufanya mashambulizi ya kushtukiza pindi wanapopokonya mpira kutoka kwa wachezaji wa Arsenal.

Kikosi cha Arsene Wenger, aliyekuwa jukwaani akitumikia adhabu ya kufungiwa mechi nne, ndio walikuwa wa kwanza kufanya mabadiliko baada ya kumtoa kiungo, Francis Coquelin na kumwingiza Olivier Giroud.

Baadaye kidogo wakamtoa tena Theo Walcott na kumwingiza Danny Welbeck, mabadiliko yalioonekana kuwapa nguvu ya kutafuta bao la kuwarudisha mchezoni.

Lakini mabadiliko yaliyofanywa na Antonio Conte kwa kuwatoa Pedro na Hazard na kuwaingiza Fabregas na Willlian ndiyo yalizaa matunda kwa Chelsea kupata bao la tatu.

Fabregas ndiye aliyeshindilia msumari wa mwisho katika lango la Chelsea baada ya kutumia vyema makosa yaliyofanywa na Petr Cech.

Mfaransa Olivier Giroud, ndiye aliyefunga bao la kufutia machozi kwa Arsenal katika dakika ya 90.

Matokeo hayo yaliwafanya Arsenal kubaki na pointi zao 47 huku Chelsea wakijikita kileleni kwa tofauti ya pointi 12 na Tottenham wanaoshika nafasi ya pili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here