Home Michezo Kimataifa CHELSEA YAIBANJUA WATFORD 4-2, MAN UNITED WALIZWA NA HUDDERSFIELD

CHELSEA YAIBANJUA WATFORD 4-2, MAN UNITED WALIZWA NA HUDDERSFIELD

563
0
SHARE

LONDON, England

WIKIENDI hii imekuwa ya majaribu kwa vigogo wa Premier League katika mechi zao za mzunguko wa tisa, ambapo jana mabingwa watetezi Chelsea nusra wachapwe kwao na Watford, huku Man United ikiambulia kichapo ugenini.

Chelsea, waliocheza mechi ya mapema jana dhidi ya Watford, iliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-2, shukrani kwa juhudi za Pedro Rodriguez na Michy Batshuayi waliochangia kwa asilimia kubwa ushindi huo.

Pedro ndiye aliyekuwa wa kwanza kutupia jana, akiunganisha vizuri pasi ya Eden Hazard, zikiwa zimepita dakika 12 tu tangu filimbi ipulizwe, lakini zikiwa zimesalia sekunde chache mno timu ziende mapumziko, Watford walisawazisha bao hilo kupitia kwa kiungo Abdoulaye Doucoure kufuatia piga nikupige langoni mwa The Blues.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kusaka bao la kuongoza, na walikuwa ni Watford ambao walifanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Roberto Pereyra, dakika nne tu baada ya kuanza kwa mpira.

Hali ilionekana kuwa tete kwa mabingwa hao, hasa kwa kocha Antonio Conte ambaye alichekecha kichwa chake kuwaza namna gani ya kufanya ili kuondoa aibu hiyo, na ndipo alipoamua kuwapumzisha Marcos Alonso na Alvaro Morata ambapo nafasi zao zilichukuliwa na Batshuayi, Willian.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa kiasi kikubwa, ambapo Batshuayi aliisawazishia Chelsea bao dakika ya 71 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Pedro.

Chelsea ilijipatia bao lake la tatu dakika ya 87 kupitia kwa beki Cesar Azpilicueta, na Batshuayi akawa shujaa wa timu yake kwa kufunga bao la nne dakika ya 90 ya mchezo huo akitumia vizuri pande la Tiemoue Bakayoko.

Man United wakiwa ugenini kuchuana na Huddersfield, walishangazwa kwa kichapo cha mabao 2-1.

Vijana hao wa Mourinho walianza msimu huu kwa kasi mno, na ilionekana kama wangeendeleza ubabe wao jana lakini haikuwa kama walivyotarajia wengi.

Huddersfield ilipachika mabao yao katika dakika ya 28 na 33 kupitia kwa Aaron Mooy na Laurent Depoitre, huku lile la kufutia machozi kwa United likiwekwa kimiani na Marcus Rashford.

Matokeo mengine:

Man City 3 – 0 Burnley

Newcastle 1 – 0 Crystal Palace

Stoke City 1 – 2 Bournemouth

Swansea City 1 – 2 Leicester City

Hadi tunakwenda mitamboni, Southampton na West Brom ubao ulikuwa unasomeka 0-0.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here