Home Makala CHUPUCHUPU SIMBA CHUPUCHUPU KWA AFRICAN SPORTS 1992

CHUPUCHUPU SIMBA CHUPUCHUPU KWA AFRICAN SPORTS 1992

407
0
SHARE

NA HENRY PAUL

MIONGONI mwa matukio yaliyowahi kufanywa na timu au wachezaji wa enzi hizo, wiki hii tunaangalia tukio moja lililoikuta klabu ya Simba, maarufu Wekundu wa Msimbazi, kuponea chupuchupu kufungwa na klabu ya African Sports ya Tanga.

Mchezo huo, ambao kwa kiasi kikubwa uliharibiwa na mwamuzi kutokana na maamuzi yake, ulikuwa ni wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), siku ya Jumamosi Machi 7, 1992.

Simba katika mechi hiyo ilicheza kandanda safi, tatizo lilikuwa ni kufunga, jambo ambalo ndio msingi wa mchezo huo. Tatizo lingine la timu hiyo ni kusheheni wachezaji wengi wa kiungo badala ya washambuliaji, wachezaji hao viungo walikuwa wanakaa na mipira muda mrefu badala ya kupiga mashuti golini.

Siku hiyo Simba iliwachezesha wachezaji watano wa kiungo ambao ni Ramadhani Lenny, Michael Paul ‘Nylon’, Hussein Marsha, Hamza Maneno na George Lucas ‘Gazza’.

Simba licha ya kupata nafasi nane za kufunga mabao katika kipindi cha kwanza, pia ilishindwa kufunga penalti iliyoipata katika dakika ya 12 kipindi cha pili, baada ya beki mmoja wa African Sports kuunawa mpira kwenye eneo la goli. Penalti hiyo ilipigwa na George Masatu na kudakwa na kipa Anthony Kasanga.

Mwamuzi wa mchezo huo, Hamisi Salum kutoka Morogoro, ambaye toka mwanzo wa mchezo alionekana anababaika katika maamuzi yake, mara baada ya kutoa penalti hiyo ambayo ilikuwa ni ya uamuzi sahihi alivamiwa na wachezaji wa Sports waliopandwa na hasira.

Cha kushangaza mwamuzi huyo licha ya kupigwa, kusukumwa na hata kukatiwa vifungo vya shati lake na kumfanya achezeshe muda uliobaki akiwa kifua wazi, lakini hakuchukua hatua yoyote kwa wachezaji hao wa Sports. Purukushani hizo za wachezaji wa Sports kumtesa mwamuzi huyo zilidumu kama dakika tano.

Mchezo huo ulichezwa kwa dakika 40 katika kipindi cha pili, baada ya mpira kusimama kwa dakika tano kutokana na kitendo cha timu ya Sports kulalamikia penalti hiyo. Simba ilibidi ijilaumu kwa kushindwa kupata angalau bao katika mechi hiyo.

Katika mechi hiyo Simba ilitawala kipindi cha kwanza zaidi ya asilimia 90, ambapo ilipata nafasi nzuri za kufunga kupitia kwa Michael Paul, Hussein Marsha, Twaha Hamidu, Gebo Peter na Hamza Maneno. Wachezaji hao walikuwa wanapokezana katika kosakosa ya kufunga mabao.

African Sports wao walitawala kipindi cha pili na kufanya kosakosa nyingi langoni mwa timu ya Simba, ambapo mipira mingi ilikuwa inadakwa na kipa Mohamed Mwameja na mashuti mengine yalikuwa yakitoka nje ya goli.

Hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika, timu zote mbili zilitoka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam matokeo yakiwa ni sare ya bila kufungana, 0-0.

Kikosi cha Simba kiliwakilishwa na kipa Mohamed Mwameja, Abuu Omari, Twaha Hamidu, Fikiri Magoso, George Masatu, Ramadhani Lenny (marehemu), Michael Paul, Hussein Marsha, Hamza Maneno/Issa Kihange (marehemu), Gebo Peter/Ali Machela (marehemu) na George Lucas ‘Gazza’.

Kikosi cha African Sports kiliwakilishwa na kipa Anthony Kasanga, Adam Idrissa, Abdul Donoa, Omari Nassoro/ Stanley Roman, Bakari Tutu, Stephen Kinduru, Mohamed Mgalike/Denis Said, Salum Makulila, Kulwa Shabani, Juma Burhan ‘Kakoko’ na Hamisi Hassan.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here