Home Michezo Kimataifa Claudio Ranieri Vs Arsene Wenger Itakuwa wikiendi ya burudani kwa mashabiki

Claudio Ranieri Vs Arsene Wenger Itakuwa wikiendi ya burudani kwa mashabiki

467
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

MWISHONI mwa wiki iliyopita mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Leicester City, walijikuta wakianza Ligi hiyo vibaya baada ya kubamizwa mabao 2-1 na Hull City, matokeo ambayo yamewafanya baadhi ya wadau kudhani kuwa utabiri wao wa kikosi hicho kupigwa kumbo Big 4 umeanza kutimia.

Wakati mabingwa hao wakijikuta kwenye matatizo hayo, huzuni ikahamia kwa mashabiki wa Arsenal, baada ya kikosi chao kusulubiwa kwa mabao 4-3, kutoka kwa Liverpool wakiwa Uwanja wao wa nyumbani wa Emirate.

Baada ya timu hizo kuianza Ligi vibaya, mwishoni mwa wiki hii zitakutana na hapo ndipo vumbi litakapotimka, kwani kila moja itakuwa ikihitaji kwa vyovyote kushinda ili kuwaridhisha mashabiki wao.

Ugumu wa mchezo huo kwa Arsenal unatokana na kwamba watakuwa ugenini, huku kocha wao mkuu, Arsene Wenger akiwa kwenye presha kubwa ya mashabiki, hasa kutokana na kushindwa kusajili wachezaji wenye sura ya kuipa mafanikio timu hiyo tofauti na timu nyingine za EPL.

Wakati Manchester United wakimsajili kwa fedha kubwa Paul Pogba kutoka Juventus, Wenger alitumia nguvu kuanza kulalamika kwamba kiasi hicho ni kikubwa na kusahau kwamba anatakiwa kukiboresha kikosi chake.

Badala ya Wenger kuilalamikia United kwamba wamemsajili Pogba kwa fedha nyingi, alitakiwa kuangalia mapungufu ya kikosi chake, kwani haohao aliokuwa anawalalamikia ndio walioibuka na ushindi, huku yeye akilala na viatu.

Hao Manchester United aliowalalamikia kwamba wamesajili kwa fedha nyingi, ndio hao walioibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Bournermouth, ugenini. Hapo ndipo ule msemo wa waswahili kwamba ‘Rahisi ghali’ unaanza kutimia kwa Wenger.

Wenger hataki kutumia fedha, wakati mashabiki wa kikosi hicho wakitaka kupata ubingwa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka mingi, yeye ameficha fedha na akisajili basi utasikia kinda wa miaka 17. Hapa kazi ipo.
Kwa vyovyote mchezo huo kati ya Arsenal na mabingwa watetezi Leicester City, utakuwa wa nenda kwa usalama, kwani licha ya kwamba ndiyo kwanza Ligi imenza, lakini waswahili wanasema ‘Nyota njema huonekana asubuhi’.

Wenger atataka kuhakikisha kikosi chake kinashinda ili kupunguza presha ya mashabiki ambao kama kawaida yao wameshaanza minong’ono ya kutomhitaji kocha huyo, huku kwa upande wa Leicester City kocha wao, Claudio Ranieri, akiwa anaandaa silaha zake kimyakimya.
Ranieri hatataka utani kabisa, atataka kushinda ili kuonyesha umma kuwa hajachukua ubingwa kwa kubahatisha na pia atataka kikosi hicho kuibuka na ushindi mbele ya mashabiki wao watakaomiminika uwanja wao wa nyumbani kuipa sapoti timu yao.

Kocha huyo hatataka unyonge, ikizingatiwa kuwa amepoteza mchezo wa kwanza na pia Wenger naye hatataka kuwaangusha mashabiki wake na hapo ndipo tutakapoona ladha ya mchezo na kuifanya wikiendi yetu kuwa poa.

Huenda kufungwa kwa Arsenal na presha zilizopo kwa mashabiki kukamfanya Wenger kuingia sokoni mapema, vinginevyo kwa kikosi hiki anaweza akajikuta anaendelea kutaabika mpaka msimu unamalizika.

Kama watafungwa tena na Leicester City, ni wazi ile morali ya wachezaji itaanza kupotea na tutaanza kushuhudia mabango ya mashabiki viwanjani wakionyesha kutokuwa na imani na kocha huyo aliyedumu muda mrefu kwenye kikosi hicho, lakini pia akidumu miaka kadhaa bila ubingwa wa Ligi.

Kwa upande wake Ranieri, naye akipoteza mchezo huo dhidi ya Arsenal mashabiki wanaweza wakaanza kuwa na wasiwasi, ikizingatiwa kuwa wenzao wanaendelea kusonga mbele wakitafuta ubingwa.

Presha ambayo ipo kwenye zile timu zinazogombea Big 4 ni kubwa sana na kwamba itakayolegea inaweza kujikuta inaachwa mbali na wenzake. Ngoja tuisubirie hii wikiendi ya Wenger na Ranieri tujue itamalizika vipi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here