Home Michezo Kimataifa David Moyes Sasa amevaa viatu ‘saizi’ yake

David Moyes Sasa amevaa viatu ‘saizi’ yake

426
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

SUNDERLAND wameamua kumpa kibarua kocha mkuu wa zamani wa Manchester United, David Moyes, ambaye alikuwa amerithi mikoba ya Sir Alex Ferguson, aliyeamua kustaafu ukocha kutokana na umri wake na mafanikio aliyoyapata ndani ya kikosi hicho.

Ilikuwa ni jambo la kushangaza baada ya Ferguson kumtengenezea ulaji Mscotland mwenzake huyo ambaye wasifu wake haukuwa umelingana na kazi aliyokuwa amepewa ndani ya kikosi hicho ambacho kilikuwa ndiyo kwanza kimetoka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini England.

Wadau wa soka hawakuhoji sana na hata wale mashabiki wa Manchester United, hawakuwa na maswali mengi sana juu ya uteuzi huo, kwani walikuwa na imani kubwa na Ferguson kwamba alipendekeza mtu anayejua kwamba ataisaidia timu kutetea ubingwa waliokuwa nao na pia kushiriki vema michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA).

Ajabu ni kwamba, Manchester United walimpa vyote Moyes, naye akapoteza vyote, ambapo badala ya kikosi hicho kutetea ubingwa wao waliokuwa wameachiwa na Ferguson, wakajikuta wakimaliza Ligi nafasi ya sita na kuwafanya mashabiki wa Mashetani hao Wekundu kuwa wanyonge mbele ya wenzao.

Kama ingekuwa ni mtihani wa kwanini Moyes aliiongoza timu hiyo iliyozoea kutwaa vikombe kumaliza nafasi hiyo, jibu lingekuwa rahisi tu, kwamba timu ambazo amezoea kuzifundisha ndiyo nafasi ambayo zimekuwa zikishika.

Moyes alichukuliwa na Manchester United akitokea katika kikosi cha Everton, ambacho amekifundisha kwa muda mrefu ambapo mara kwa mara wamekuwa wakimaliza Ligi nafasi za katikati, tofauti na msimu wa 2004/05 ambapo angalau walijitutumua na kumaliza katika nafasi ya nne.

Msimu huo Chelsea ndio waliotwaa ubingwa, wakifuatiwa na Arsenal, iliyomaliza nafasi ya pili, Manchester United chini ya Sir Alex Ferguson wakamaliza nafasi ya tatu na Everton wakamaliza nafasi ya nne, mafanikio ambayo mpaka sasa Moyes hajayapata tena, anayasikia kwenye bomba tu.

Tangu hapo Everton chini ya Moyes ikawa ikimaliza nafasi za katikati ambazo timu haigombanii ubingwa wala haipo kwenye hatari ya kushuka daraja. Wao ndiyo zile timu ambazo zinasherehesha Ligi, hazina presha ya kushuka daraja wala haziwazi kutwaa ubingwa.

Hizo ndizo aina ya timu ambazo Moyes anatakiwa kuzifundisha na siyo timu kubwa kama Manchester United, ndiyo maana hakuweza kudumu kabisa kwenye kikosi hicho ambacho kina njaa ya mafanikio. Wao wanawaza ubingwa kila mahali, iwe Ligi Kuu au Klabu Bingwa Ulaya na kila kikombe kilichopo mbele yao.

Kwa sasa Moyes amekwenda sehemu sahihi kabisa, Sunderland ni mahala salama kwake, viatu alivyokabidhiwa vinamtosha kabisa, tofauti na vile alivyokuwa amekabidhiwa na Sir Alex Ferguson pale Old Trafford.

Hata hivyo, atakuwa na jukumu zito la kuhakikisha msimu ujao kikosi hicho kinakuwa zile sehemu zake za kutokushuka wala kupigania ubingwa, kwani msimu uliopita wakali hao walinusurika kutumbukia shimoni.

Msimu unaokuja Sunderland wanaanza kukipiga na Manchester City wakiwa ugenini na hapa Moyes atakuwa na kibarua cha kuhakikisha haanzi vibaya na hata ikiwa bahati mbaya akaanza hivyo anatakiwa kupigania ushindi kwenye michezo mingine.

Tangu kuondoka Everton, Moyes amekuwa na bahati mbaya ya kutimuliwa, kwani alivyoanza kupewa mkono wa kwaheri Manchester United, hali ilikuwa hivyohivyo hata kule nchini Hispania katika Klabu ya Real Sociedad.

Moyes anaweza kupata mafanikio akiwa na Sunderland, kwani inawezekana asiwe na presha kubwa kama ilivyo kwa timu kubwa kama Manchester United. Sunderland wao hawawazi ubingwa na badala yake wao wanataka kuona kila mara wakishiriki tu, sasa hapo Moyes atashindwa nini? Ngoja tusubiri Ligi ikianza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here