SHARE

dele alli*Ndiye injini mpya inayotikisa kwenye kikosi cha England

LONDON, England

SIKUMBUKI ni lini tena niliwahi kuwa na shauku ya kutaka kuiona England kwenye michuano mikubwa. Mkusanyiko wa vijana wasioogopa, wenye kasi, nguvu na wapambanaji, unakufanya utabiri kitu ndani yao.

Nakumbuka tulishawahi kuzungumza kuhusu kizazi cha dhahabu kilichokuwa chini ya Steven-Goran Eriksson, ndio, walikuwa na vipaji vikubwa lakini mara zote nilikuwa nahoji kuhusu utimamu wao kiakili.

Ni jambo la kuvutia mno kukiona kikosi cha England kikienda kwenye mashindano makubwa kwa staili na ubunifu wao wa kipekee.

Kikosi cha sasa kimeshatambua kuwa hawana cha kupoteza, wameshafahamu kuwa hawaaminiki na walichofanikiwa ni kujiamini wao wenyewe. Hii inaleta taswira nzuri kwa mara ya kwanza kuona tuna timu kamili.

Nilipenda kiwango kilichoonyeshwa na Dele Alli, hakuwaangusha waliompa imani. Nilipenda namna alivyojitoa kwenye pambano lile.

Gwiji wa Ujerumani, Lothar Matthaus, alimtaja kama mchezaji bora katika kikosi hicho na alivutiwa mno na kiwango alichokionyesha.

Kutokana na pambano lile la England dhidi ya Ujerumani, nahodha wa zamani wa England, Bryan Robson, alitoa tathmini yake kwa namna alivyomtazama Delle Alli.

KUKABA

Alli anapenda kukaba, si ndio? Akiwa katikati ya viungo bora, Toni Kroos na Sami Khedira, Delle aliwapa wakati mgumu sana kwa usumbufu wake.

Kwa kiungo mchezeshaji, unatakiwa kutojiingiza mara nyingi katika matukio ya vurugu uwanjani, ndio maana wakati fulani hata anapojaribu kucheza faulo, haiwi katika kiwango cha kumshtua mwamuzi. Napenda sana ukabaji wake!

STAILI YA UCHEZAJI

Kama ningekuwa napambana naye uwanjani, nisingependa kucheza karibu yake. Ana ubunifu wa kipekee na mjanja mjanja sana. Hupenda kukaba kwa njia kama alivyokuwa akimsumbua Emre Can.

Yuko mchezoni wakati wote, ni msumbufu na kama ukiwa na hasira unaweza kujikuta umeingia kwenye mtego wa kupewa kadi nyekundu. Anatumia akili sana kwenye kufanya majukumu yake.

Najua atapata wakati mgumu sasa. Atatukanwa na kutolewa vitisho uwanjani. Najua kuna baadhi ya viungo watacheza kwa kumvuruga na kumkwatua kila wakati.

Lakini kitu muhimu anachotakiwa kufahamu pindi atakapokutana na changamoto hizi ni kuwa wachezaji bora hufanyiwa fujo za aina hizi.

Anatakiwa kutulia na kucheza soka lake, maana hasira zinaweza kuigharimu timu hata kumgharimu katika ukuaji wake kisoka.

KUCHEZA NAFASI NYINGI

Moja katika vitu vizuri ambavyo shule za soka hapa kwetu zimefundisha vijana ni kujitahidi kucheza nafasi nyingi uwanjani.

Wakati nilipoanza soka pale West Bromwich, Johnny Giles, aliyekuwa kocha mchezaji alichezesha beki wa kushoto, beki wa kati na kiungo mkabaji. Ilinisaidia sana kwenye ukuaji wangu.

Alli ana kichwa kizuri cha kusoma nafasi za wenzake uwanjani na kujua anapotakiwa kuziba. Kwa namna anavyokuwa na kukomaa zaidi kisoka, atakuwa mchezaji hatari zaidi katikati ya uwanja, ila kwa sasa naamini mbinu za Roy Hodgson, zilifanya kazi vyema kwake kwenye pambano dhidi ya Ujerumani.

Anaweza kucheza nafasi nyingi. Kushoto, nyuma ya straika wa kati, kiungo wa chini na kiungo mshambuliaji pia. Ni hazina kubwa kwa soka la England siku za baadaye.

all

NJIA ZAKE UWANJANI

Njia zake uwanjani zinavutia mno. Aliweza kuwaunganisha vyema Danny Welbeck na Danny Rose, upande wa kushoto. Alicheza vyema na kukaba kwa nafasi, hali iliyowapa wakati mgumu sana Ujerumani kwenye kupanga mashambulizi yao.

Aliwavuruga mno! Aliziba njia zote za Ujerumani na kuwapa nafasi wenzake kucheza kwa nafasi. Nilipenda mno namna alivyokaba na kushambulia kwa wakati. Ni jambo zuri kwa England kuwa na mchezaji wa aina yake kwenye kikosi chao.

PASI

Alli ni mtulivu sana akiwa na mpira, anafikiria zaidi ya mara mbili kabla ya kufanya maamuzi. Nilipenda namna alivyokuwa akijitahidi kutafuta pasi za kwenda mbele. Ni jambo zuri kwa kiungo kufikiri kwenye kuipandisha timu mbele na kutafuta matokeo.

MASHUTI

Alikuwa na nafasi nzuri dakika za mwisho, lakini aliamua kutoa pasi kwa Jamie Vardy. Angeweza kufunga eneo lile. Lakini kichwani alikuwa anaonekana kukaribia kujaribu alichoshindwa kukifanya baada ya pale. Alijaribu mara kwa mara kupiga mashuti.

Ni mwenye moyo wa kupambana na kujaribu nafasi kila wakati. Wakati fulani alimpa shida Manuel Neuer kwa mashuti yake ya kushtukiza.

Amefunga mabao mengi akiwa na Tottenham, hali iliyomfanya Neuer kuwa na tahadhari muda wote kinda huyu anapokuwa na mpira. Tunaweza kumsamehe Alli kwa kutofunga bao, lakini hatuwezi kuacha kumpongeza.

 

NGUVU

Ubora wa Alli kwenye nguvu ni wakuridhisha. Ni hazina nzuri kwa siku za baadaye. Niliwahi kuwa katika nafasi kama yake kipindi naanza soka, lakini mazoezi yalizidi kunibeba zaidi. Nilijiweka fiti muda wote. Naamini Alli anaweza kufuata nyayo zangu kwa kupenda mazoezi.

Ana kasi sana na anaingia vizuri kwenye boksi ya wapinzani. Bado ana muda mwingi wa kucheza soka la ushindani, kipindi hiki ana miaka 19. Ni rahisi kumtabiria mambo mazuri zaidi akiwa na miaka 23. Huu ni umri ambao kwa kawaida mchezaji unakuwa umeshakomaa maeneo yote.

UDHAIFU

Sijaona mapungufu mengi kutoka kwake. Nilichogundua zaidi ni ubovu wake wa kucheza mipira ya juu. Hawezi kabisa purukushani za aina hii. Hili ni jambo ambalo anatakiwa kulifanyia kazi kwa makini zaidi ili awe na ubora unaoridhisha.

NINI AFANYE?

Katika umri wa Alli, hakuna kitu kikubwa zaidi ya kujitolea. Inapokuja nafasi ya kufanya hutakiwa kufikiria mara mbili, unafanya. Hutakiwi kudhani kuna mtu bora zaidi yako duniani, unachotakiwa kujiuliza, ni vipi utakuwa bora zaidi duniani.

Nilipokuwa na umri wa miaka 19 nilikumbana na changamoto nyingi sana. Tulishinda kombe la vijana U-18 kule Uswisi, lakini jambo baya zaidi nilivunjika mguu wangu mara tatu. Mambo mengi sana yalikuwa yakijirudia kichwani mwangu.

Don Howe, aliyekuwa kocha wangu nikiwa West Brom, aliniambia nitafanikiwa kila kitu ninachokitaka maishani mwangu kama nitaamua kufanikiwa. Sikubadili aina yangu ya uchezaji, niliendelea kuamini kwenye ubora niliokuwa nao.

Tulipokwenda Kombe la Dunia 1982, mashindano makubwa zaidi kucheza kwa mara ya kwanza. Akili yangu ilianiambia pale ndipo ninapotakiwa kwenda kujipima na wachezaji bora zaidi dunia.

Zilikuwa ndoto zangu tangu utotoni. Ni moyo huu wa upambanaji niliouona pia kwa Ryan Giggs na Paul Scholes. Iko mifano mingi ya wachezaji ambao walifika kwenye ubora wa Alli, lakini mwisho wa siku walipotea kusikojulikana.

Kitu pekee kinachotakiwa kuwa kwenye kichwa cha Alli, ni kusema ‘mimi ni bora na ninataka kuwa bora zaidi, hata kama sio mwaka huu, basi mwakani.’

Nataka kuwa bora na itakuwa hivyo milele. Napenda kukiona kitu hiki kwa Barkley na kwa Alli, pia. Barkley ni miongoni mwa vijana walionivutia zaidi. Natamani kuona vijana hawa wawili wakikomaa na kupambana zaidi na zaidi watakapopata nafasi, wajue kwanini wana jezi za taifa. Ni wakati wao sasa kusimama kama wanaume kufanya kazi ya kiume iliyowashinda wanaume wengi wa England.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here