Home Makala DOGO ALIYEMKUMBATIA ROONEY AFUNGUKA…..SITASAHAU SAA 24 NILIZOKAA MAHABUSU

DOGO ALIYEMKUMBATIA ROONEY AFUNGUKA…..SITASAHAU SAA 24 NILIZOKAA MAHABUSU

528
0
SHARE

NA ALLY KAMWE


KAMA bado ulikuwa unapata shida kuielewa maana ya neno ‘jasiri’, basi likumbuke tukio la shabiki aliyeingia uwanjani na kumkumbatia Wayne Rooney, kwenye mchezo wa Everton dhidi ya Gor Mahia.

Licha ya ulinzi mkali uliowekwa na askari wa usalama katika kila pembe za dimba la Taifa, Dar es Salaam, kijana Hassan Omary Junior maarufu kama ‘Hans Jr’, aliishtua dunia kwa ujasiri wake wa kuingia uwanjani na kumkumbatia Wayne Rooney.

“Nilipoona askari wako makini wakifuatilia mechi, sikufikiria mara mbili. Nilimuomba Mungu na kuruka,” alisema Hassan ambaye kwa sasa mashabiki wa soka wamempachika jina la ‘Rooney wa Bongo.’

Hassan alifanya tukio hilo lililoripotiwa na vyombo vikubwa vya habari duniani, dakika ya 22 akitokea katika jukwaa la kaskazini mwa uwanja na kuibua shangwe kubwa kwa wapenzi wa soka walioshuhudia mchezo ule.

Wengi wamekuwa na hamu ya kutaka kufahamu mengi kuhusu kijana huyu, ametokea wapi? Ilikuwaje kabla ya kuruka? Nini kimemtokea baada ya kukamatwa na polisi?

Gazeti lako kongwe na kinara wa habari za michezo na burudani Tanzania, DIMBA Jumatano, tuliingia mtaani na kumsaka Hassan kwa ajili ya kukata kiu ya wasomaji wetu.

Yafuatayo ni mahojiano maalumu tuliyoyafanywa na kijana huyu katika ofisi zetu zilizopo maeneo ya Sinza Kijiweni. Karibu kwa uhondo zaidi.

 

Historia yake kwa ufupi

Jina langu ni Hassan Omary Junior, japo sasa hivi kila nikikatiza mitaani naitwa ‘Rooney wa Bongo’. Nilizaliwa Tumbi, Kibaha tarehe 4, 4, 1997.

Elimu ya msingi niliipata katika Shule ya Twende Pamoja iliyopo Kibaha Picha ya Ndege na baadaye nikajiunga na Shule ya Nyumbu kwa masomo ya sekondari.

 

Ulianza lini kuipenda Manchester?

Nilianza kuishabikia Manchester United mwaka 2005. Nilianza kuipenda United kabla ya kuiona kwa sababu nilikuwa nikisikia sifa zake kwa rafiki zangu na watu walionizidi umri.

Ilinivutia zaidi pale nilipoanza kufuatilia mechi zake na kuona wakipata matokeo. Nakumbuka mchezo wa kwanza kuutazama ulikuwa dhidi ya Wigan Athletic.

 

Kwanini ulimchagua Wayne Rooney?

Ni ‘role model’ wangu na ndiye mchezaji niliyekuwa namkubali katika kikosi cha Manchester United. Mimi pia nacheza soka na nafasi ninayoichezea ni straika, hivyo najifunza vitu vingi kila ninapomtazama.

 

Utahamia Everton na Rooney?

Hapana. Nafikiri mimi naweza kuwa shabiki namba moja wa Manchester United hapa Tanzania. Naipenda mno. Rooney atabaki kuwa mchezaji ninayemkubali lakini mapenzi kwa klabu yangu yanabaki palepale.

Ni kweli ulituma text kwenye magroup ya whatsap kabla ya tukio?

Si kweli. Nafikiri ile ilitengenezwa na rafiki zangu. Mimi sikuwa na muda wa kushika simu kwa wakati ule. Akili yangu yote ilikuwa ‘busy’ kufikiria jinsi ya kuingia uwanjani na kukamilisha azma yangu.

Nani wa kwanza ulimpa taarifa kuwa ungeingia uwanjani na kumkumbatia Rooney?

Nilizungumza na marafiki zangu wengi juu ya hilo. Wako waliodhani nawatania lakini pia wako ambao walinisihi nisifanye tukio hilo kwa kuwa ningejiweka kwenye matatizo na Jeshi la Polisi.

Pamoja na yote niliendelea na imani yangu na wale wote walionikatisha tamaa niliachana nao, sikupokea tena simu zao.

 

Ulizungumza lolote na Rooney baada ya kumfikia?

Ndio, nilipomkumbatia nilimuomba anipe jezi yake kwa kumwambia kwa kizungu ‘Give me jersey’ na yeye akanijibu ‘ok ok.’

Lakini ghafla polisi wakawa wamenifikia na kunikamata. Sikujali tena kwa kuwa nilishatimiza lengo langu la kumkumbatia. Sikuwa na hofu kama ningepigwa au la, nilikuwa tayari kwa lolote.

 

Hukuwa na hofu na askari?

Toka nafikiria kufanya tukio lile sikuwahi kuwafikiria askari. Niliamini kufanya hivyo kungenipa woga kidogo. Nilichokuwa najitahidi kufanya ni kufikiria mbinu za kuwatoroka ili nifanikishe lengo langu.

Tangu siku niliposoma kwenye vyombo vya habari kuwa Rooney atakuja na Everton, Tanzania, nilianza kufanya mazoezi ya kukimbia ili nipate pumzi. Nilijua kabisa kama nisingekuwa na pumzi za kutosha askari wangenikamata mapema kabla ya kufanikisha lengo langu.

 

Ulitumia mbinu gani kuwapenya askari?

Tangu mchezo ulipoanza nilikuwa nikiwafanyia doria askari, sikutaka kuipoteza nafasi ile. Nakumbuka kwanza kabisa nilitaka kuingia uwanjani dakika ya 15.

Si unajua ule ni mchezo wa kirafiki kwahiyo nilikuwa na hofu kuwa angeweza kutolewa kipindi cha pili na nisitimize lengo langu.

Dakika ya 15 nilishindwa kuruka kwa sababu askari mmoja alikuwa akitupa jicho jukwaani, lakini ulipofika ule muda niliona wakiwa wameduwaa na hapo hapo kwa kasi nikadandia bomba na kuwaruka askari kichwani.

Kiukweli kama nisingekuwa na mazoezi ya kutosha, wale askari wangenikamata maana Rooney alikuwa mbali kidogo. Nilijitahidi sana kukimbia na Mungu alinisaidia nikamfikia alipokuwa amesimama.

 

Nini kilifuata baada ya kukamatwa?

Baada ya kukamatwa nilipelekwa moja kwa moja katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, nikafunguliwa kesi ya kufanya fujo uwanjani.

Nikavuliwa mkanda nikakabidhi fedha baadhi niliyobaki nayo mfukoni (Sh 22,000) na simu ndogo ya rafiki yangu kisha nikaingizwa mahabusu.

 

Saa 24 ndani ya mahabusu

Niliingia ndani Alhamisi jioni. Nakumbuka wakati maaskari wakiniingiza ndani walikuwa wakitaja kosa langu kuwa niliruka uwanjani na kumkumbatia Rooney, kitendo kilichofanya mahabusu wengine walianza kunishangilia.

Ndani niliishi kama mfalme, kila mtu alitamani kuwa karibu na mimi. Niliagiziwa vyakula vingi, kiukweli siwezi kuyasahau maisha ya mule.

Sikupigwa kama inavyosemwa mitaani, polisi walikuwa kama kaka zangu. Nilizungumza nao na kucheka nao wakati wote, tena baadhi walikuwa wakinitoa nje kupiga picha na mimi, haikuwa sehemu ngumu kwangu kama watu wanavyodai.

Ile Ijumaa usiku, mkuu wa kituo alivyonipa taarifa kuwa niko huru na naweza kwenda nyumbani, nilifurahi sana na kuwaaga maaskari wote.

 

Mama alilipokeaje tukio lako?

Alikasirika sana. Nilivyokutana naye baada ya kutoka alinisema sana kuhusu tukio nililolifanya. Hofu yake ilikuwa ni vipi kama nisingetoka na kupelekwa mahakamani.

 

Maisha yako baada ya tukio lile?

Kiukweli mambo yamebadilika sana. Kila ninapopita watu wananisimamisha na kuniomba picha. Naulizwa sana maswali. Kiukweli nafurahi kuona watu wakinisapoti.

 

Ni kweli ulifanya vile kwa ajili ya kusaka umaarufu?

Tena hili bora niliweke wazi. Sikufanya vile kwa sababu ya kutaka umaarufu kwa watu. Mimi ni shabiki wa Manchester na ni mpenzi wa Wayne Rooney, nilifanya kwa mapenzi yangu tu.

Tangu nilipotoka Polisi, vyombo vingi vya habari vimenisaka lakini nilisita kwenda kuzungumza nao lolote kwa sababu nilihofia kuonekana labda nasaka ‘Kiki’. Naomba Watanzania waelewe kuwa mimi nampenda sana Rooney na niliruka uwanjani kwa mahaba yangu.

 

Unalizungumziaje agizo la Waziri Mwakyembe la kufungwa jela miezi 6 kwa yeyote atakayefanya tukio kama lako?

Kwanza ningependa kumpa shukrani zangu Waziri kwa huruma yake aliyoionyesha siku ile baada ya kukamatwa. Nawashukuru pia na viongozi wengine walionipambania akiwemo mama yetu Makamu wa Rais, Samia Suluhu.

Binafsi sikufanya vile kwa nia mbaya, ni mapenzi yangu tu kwa Rooney. Namuomba Waziri angetufikiria na sisi mashabiki wa soka wenye mapenzi ya dhati na wachezaji wa Ulaya kupata nafasi ya kuwa nao karibu zaidi pindi wanapokuja kututembelea.

 

Kwa hapa Tanzania ni shabiki wa timu gani?

Hapa nyumbani mimi ni shabiki wa Yanga na nilianza kuishabikia kwa sababu ya mama. Mara nyingi alikuwa akiisifia na nikajikuta nikianza kuipenda.

Mchezaji ninayemkubali kwa sasa pale Yanga ni Donald Ngoma japo awali nilikuwa shabiki mkubwa wa Haruna Niyonzima, lakini nilivyosikia tu amejiunga na Simba, nikaachana naye.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here