Home Habari NYOTA YA MBAGALA INAYONG’ARA EPL

NYOTA YA MBAGALA INAYONG’ARA EPL

1675
0
SHARE

NA AYOUB HINJO

IMEKUWA furaha kubwa kwa kila Mtanzania aliposikia au kuona habari za nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta, kuhitajika na klabu za Everton, West Ham, Burnley na Brighton, zote zinazokipiga Ligi Kuu England.

Ni safari ya mafanikio ambayo alianza kuiota tangu alipojiunga kikosi cha Simba mwaka 2010, akitokea timu ya African Lyon, wakati huo ikijulikana kwa jina la Mbagala Market.

Ndoto alizokuwa nazo wakati ule anakimbia katika mitaa ya Mbagala zimemfanya kila siku kula kuku katika mitaa ya Brussels, nchini Ubelgiji, akiwa na kikosi cha KRC Genk, baada ya kuitumikia kwa mafanikio TP Mazembe, ambao ni mabingwa mara tano wa Afrika ngazi ya klabu.

KWANINI EVERTON NA WENGINE?

Tetesi za usajili kuelekea dirisha dogo Januari mwakani zimeshika kasi kubwa baada ya kubainika timu za Everton, West Ham, Burnley na Brighton kuwania saini ya straika huyo wa Genk.

Iko hivi, kwa upande wa Everton, tangu kuondoka kwa straika wao, Romelu Lukaku, aliyejiunga na Manchester United, kwa kiasi cha pauni milioni 75, hawakufanikiwa kupata mshambuliaji wa uhakika wa kufunga mabao.

Nafasi hiyo ya ushambuliaji inaonekana kuwa na tatizo katika timu hiyo, ambayo ilimrejesha Wayne Rooney kutoka Manchester United, ambaye hivi sasa ametimkia DC United ya Marekani.

Dirisha dogo la usajili mwaka jana, Everton, waliowahi kuja nchini Tanzania walifanikiwa kupata saini ya straika wa Uturuki, Cenk Tosun.

Tosun ameshindwa kuvaa viatu vya Lukaku, ikiwa msimu huu amefanikiwa kufunga bao moja tu katika michezo aliyocheza. Kutokana na ubutu huo, klabu hiyo kongwe nchini England iliamua kumwaga kitita cha pauni milioni 50 kumsajili winga wa Watford, Richarlson.

Richarlson, ambaye anamudu vizuri kucheza nafasi ya winga wa kushoto, amebadilishwa na kutumika kama straika na kuonyesha kufanya vizuri kwa kufunga mabao muhimu ndani ya Everton.

Lakini kadri muda unavyosogea, Samatta amezidi kuonyesha uwezo mkubwa kuwa na uadui na makipa pamoja na mabeki kwa kujiunga urafiki na nyavu za wapinzani wao kila wanapokutana.

Samatta amefanikiwa kufunga mabao 14 katika michezo 16 kwenye michuano yote mpaka sasa, yaani mabao saba ndani ya Ligi Kuu Ubelgiji, ikiwa imechezwa michezo tisa na mengine saba kwenye Ligi ya Europa, wakikipiga mechi saba tangu hatua za awali na kutinga hatua ya makundi.

Kiwango anachokionyesha hivi sasa ni kivutio kikubwa kwa Everton na timu nyingine zilizo mstari wa mbele kuwania saini yake kwa thamani yoyote ile itakayowekwa mezani.

West Ham walianza Ligi Kuu England kwa kusuasua, baada ya kufungwa michezo minne mfululizo ya mwanzo, huku wakionyesha udhaifu mkubwa katika safu yao ya ushambuaji ambayo inaongozwa na Marko Arnautovic.

Arnautovic hajawa katika ubora mkubwa kama ilivyokuwa misimu ya nyuma, kupungua kwa kasi yake kunafungua milango ya Samatta kuhitajika ndani ya kikosi hicho cha ‘The Hummers’, kilichopo katika jiji la London.

Kwa upande wa Burnley, ni moja ya timu za Ligi Kuu England zilizotengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini hazikutumika vizuri na washambuliaji wa klabu hiyo.

Kocha wa kikosi hicho, Sean Dyche, anahitaji kusajili straika kiwembe ambaye ataweza kufanikisha hilo kwa kufunga mabao kutokana na nafasi zinazotengenezwa na timu yake.

Dyche, ambaye ni raia wa England, amekuwa muumini mkubwa kucheza soka la kasi na kupiga mipira mirefu kwa washambuliaji wake, ambao kwa kiasi kikubwa huwa hatari kutumia kwa mipira ya vichwa.

Samatta ana nguvu, kasi na uwezo wa kupambana na mabeki bega kwa bega, anaweza kuwa funguo katika kilio cha kocha huyo tangu kuanza kwa msimu huu, ambao mapema tu walifungashwa virago katika Ligi ya Europa, ambayo straika huyo wa Genk anatamba.

Ni furaha kwa Watanzania kusikia tetesi hizo zikikua kwa kasi kubwa, huku kila mmoja akiamini ni njia sahihi kwa nahodha huyo wa Taifa Stars kusonga mbele kwenda ligi ambayo ina ubora zaidi na ushindani wa hali ya juu.

MWAKA 2015 AANDIKA HISTORIA

Alipojiunga na TP Mazembe iliyopo nchini DR Congo mwaka 2011 kutoka Simba ya Tanzania, alifanikiwa kutengeneza jina kutokana na kiwango alichokionyesha.

Samatta alifanikiwa kuwateka mashabiki wa TP Mazembe, ambao hawakuchoka kuimba jina lake kila alipokuwa uwanjani, mwishowe alifanikiwa kufuta ufalme wa Tresor Mputu, mzawa wa Congo na mkongwe wa timu hiyo kubwa Afrika.

Ukitoa kushinda taji la Ligi Kuu ya DR Congo, mwaka 2015 hauwezi kusahaulika kwa Samatta, ambaye alitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza akiwa na TP Mazembe.

Lakini chachu kubwa ya ushindi wa taji hilo kubwa katika ngazi za klabu Afrika ilikuwa mabao yake saba aliyofunga na kuiwezesha kutwaa ubingwa huo.

Mwaka huo huo ulikuwa na baraka kubwa kwake, alipochaguliwa katika majina matatu ya wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika wa Ndani na kufanikiwa kunyakua tuzo hiyo.

Katika kinyang’anyiro hicho, Samatta alifanikiwa kupata kura 127, akiwashinda Robert Kidiaba, kipa wa TP Mazembe aliyepata kura 88 na mshambuliaji wa Etoile du Sahel, Baghdad Bounedjah, aliyepata kura 63.

Samatta aliandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, Cecafa, kutwaa tuzo hiyo kabla ya kipa wa Mamelodi Sundowns, Dennis Onyango, raia wa Uganda kutwaa tuzo hiyo mwaka 2016.   

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here