SHARE

el classicoNA NIHZRATH NTANI
“KWA mtazamo wangu kuna wafalme wanne wa soka duniani. Yupo Alfred Di Stefano, Pele, Johan Cruyff na Diego Maradona.”
Maneno haya yalitoka kinywani mwa kocha wa zamani wa FC Barcelona, Cesar Luis Menotti, Oktoba mwaka 2011.
Wakati huo alikuwa akihojiwa  na jarida maarufu la soka nchini Hispania liitwalo Marca. Wakati mashabiki wengi wa soka wakiendelea kuaminishwa kuwa kuna mfalme mmoja wa soka duniani ambaye ni Edson Nascimento ‘Pele’ wa Brazil, Cesar Luis Menotti amekuwa na mtazamo tofauti na bahati nzuri wote wanne amebahatika kuwatazama. Ajabu iliyoje hii?

Miaka mitatu baadaye, yaani Julai 7, 2014 tangu Menotti alipotoa kauli hiyo, mmoja wa wafalme kati ya hao wanne, Alfredo Di Stefano, alikuwa anaaga dunia akiwa na miaka 88 na kuacha jina lake katika kumbukumbu za historia ya soka duniani, hususan klabuni Real Madrid na historia ya kuwepo kwa El Clasico. Miaka mitano baadaye tangu Menotti alipotoa kauli hiyo na miaka miwili tangu Di Stefano aage dunia, ndipo ambapo mfalme mwingine, Johan Cruyff anaaga dunia kwa ugonjwa wa kansa akiwa na miaka 68 tu Alhamisi ya tarehe 24 mwezi Machi mwaka 2016. Huzuni iliyoje.

Wanaume hawa magwiji wa soka hawapo tena duniani na si tena wafalme wa soka, lakini bado wameacha historia kubwa katika soka. Wakati Alfredo Di Stefano alikuwa akitambulika kama alama ya soka ya Real Madrid na mchezaji bora wa muda wote klabuni hapo, huku historia ya mataji wanayojivunia mashabiki wa Real Madrid hivi leo ni kwa sababu ya miguu ya Di Stefano. Ufalme wa soka wa Real Madrid nchini Hispania ulichangiwa sana na mtu huyu aliyeitwa Di Stefano.

Hata sera ya kununua wachezaji ghali na mahiri sana kisha kuwaleta Real Madrid ilianzia kwa Alfred Di Stefano. Yeye ndiye aliyekuwa Galactico wa kwanza kuletwa Santiago Bernabeu na Rais wa Real Madrid wakati huo, Santiago Bernabeu Yeste. Historia ya Di Stefano klabuni Real Madrid haina tofauti na aliyoyafanya Johan Cruyff klabuni Barcelona. Wakati ambapo tunaiona Barcelona katika staili ya kipekee ya ‘Tik Taka’, soka lenye kuvutia na pasi nyingi. Nyuma ya haya yote tunayoyaona kwa Barcelona hivi leo yupo Johan Cruyff, ambaye ndiye muasisi wa staili hii klabuni Barcelona. Wote wawili hawapo nasi tena. Wapumzike kwa amani.

Jumamosi hii ya Aprili 2, 2016, nyasi za uwanja wa Camp Nou zitawaka moto wakati miamba ya soka nchini Hispania na dunia kwa ujumla itakapopambana katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya soka Hispania, maarufu kwa jina la La Liga. Ni kwa mara ya kwanza baada ya kupita zaidi ya miaka ishirini. Wachezaji wawili wenye historia kubwa kwa klabu hizi mbili hawataonekana pale kwenye jukwaa la watu mashuhuri wa heshima. Hatutamuona Cruyff akiwa na tabasamu lake na wala hatutamuona Di Stefano na fimbo yake jukwaani. Wamekwenda na tutawakumbuka kwa historia zao.

Pamoja na kupoteza magwiji hao, lakini hilo halitaondoa msisimko mkubwa wa El Clasico hii. Na  ni kutokana na Barcelona kuwa mbele kwa tofauti ya pointi 10 kileleni dhidi ya mahasimu wao, Real Madrid, ambao wanashika nafasi ya tatu nyuma ya Atletico Madrid, huku zikibakia mechi 8 kukamilisha mzunguko wa pili. Lakini kutokana na timu hizi kuundwa na mastaa wa soka na wachezaji mahiri kabisa, bado tunaweza kuona ule upinzani ukiibuka.

Luis Enrique Vs Zinedine Zidane
Sahau kuhusu El Clasico. Uwepo wa Zidane katika benchi la Real Madrid akiwa kiongozi na uwepo wa Luis Enrique akiwa kiongozi wa benchi la Barcelona ni jambo litakaloleta burudani kubwa kwa watazamaji wa mechi hii. Wote wawili wamepata kuwa wachezaji mashuhuri wa klabu zao. Wakati Luis Enrique akipata bahati ya kuchezea klabu zote mbili hizi, lakini akiwa na heshima kubwa klabuni Barcelona, Zinedine Zidane aliichezea Real Madrid pekee na kustaafu hapo, huku akiacha heshima kubwa klabuni hapo.

Tangu alipoteuliwa mwanzoni mwa Januari mwaka huu baada ya kufukuzwa kwa Rafa Benitez, Zidane ameiongoza Real Madrid katika mechi 12 za La Liga na kushinda mechi tisa, sare mbili na kupoteza mechi moja dhidi ya Atletico Madrid. Kwa upande wake Luis Enrique ameiongoza Barcelona katika mechi 30 msimu huu katika La Liga na kushinda mechi 24, sare mechi nne, huku akipoteza mechi mbili. Takwimu zinamuweka mbele zaidi Enrique na kuwa na nafasi kubwa ya kushinda mechi hii kutokana na uzoefu wake wa El Clasico, wakati Zidane hii itakuwa El Clasico yake ya kwanza kuiongoza Real Madrid akiwa kocha wa klabu hiyo.

Vita ya MSN vs BBC
Kwa miaka ya karibuni kumeibuka vita ya kombineshi hizi mbili, hasa inapokuja pambano la El Clasico. Macho ya wapenzi wengi wa soka huwa kwa wachezaji Lionel Messi, Suarez na Neymar, wanaounda kifupisho cha MSN na Benzema, Bale na Cristiano Ronaldo wanaounda ushirikiano wao uliobatizwa jina la BBC. Msimu huu MSN ipo katika fomu ya hali ya juu na huwezi kuwalinganisha na BBC hata kidogo, ambao wanapitia kipindi kigumu mno.

Takwimu zao hazidanganyi. Msimu huu MSN wamefunga jumla ya mabao 107 katika mechi 119 pekee za La Liga, ukijumlisha mechi na mabao ya kila mmoja, huku kwa pamoja wakichangia kutoa pasi za mwisho 48. Ingawa hawana msimu mzuri, kombinesheni ya BBC wametupia kwa pamoja mabao 80 katika mechi 84 na kusaidia kutoa pasi za mwisho 27. Hata hivyo, bado hawawezi kudharauliwa katika El Clasico hii.

Vita ya Ronaldo vs Messi
Sahau kuhusu BBC na MSN. Kwa takribani misimu saba sasa, El Clasico inachukuliwa zaidi  na mashabiki wa soka kama pambano la kutoa hukumu ya nani zaidi kati ya Messi na Ronaldo. Wachezaji hawa wawili wana mvuto ndani na nje ya uwanja. Upinzani wao huongeza msisimko wa mechi hii inayochukuliwa kuwa tukio kubwa la soka ngazi ya klabu duniani. Wakati Lionel Messi akiwa na rekodi ya kufunga mabao 21 katika El Clasico kwa misimu 11, Cristiano Ronaldo amefanya hivyo mara 15 katika misimu yake saba, huku akiwa na rekodi ya kufunga mabao saba katika mechi sita mfululizo za El Clasico. Inavutia sana kuwatazama watu hawa wawili wakipambana kwa pamoja na huleta upinzani kwa mashabiki wa pande zote.

Rekodi ya Barcelona Vs Real Madrid.
Katika  La Liga pekee wamekutana jumla ya mechi 171. Real Madrid wakiibuka na ushindi katika mechi 71, huku Barcelona wakiibuka na ushindi jumla ya mechi 68, huku mechi 32 zikitoa matokeo ya sare kwa timu hizi. Real Madrid imeweza kuutumia uwanja wake wa nyumbani na kuibuka na ushindi wa mechi 52 na kutoa sare mechi 15 dhidi ya Barcelona, wakati Barcelona imeifunga Real Madrid uwanjani Nou Camp jumla ya mechi 48 na kutoa sare mechi 17. Real Madrid wameweza kushinda Nou Camp mechi 19 tu wakati Barcelona nao wakifanya hivyo sawa na Real Madrid kushinda mechi 19 uwanjani Santiago Bernabeu.
Mechi ya Jumamosi hii itakuwa yenye kulinda heshima zaidi kwa timu zote mbili wakati huu Real Madrid wakiwa wamepoteza matumaini ya kutwaa ubingwa huo. Ni wakati mwamuzi Alejandro Jose Hernandez atakapopuliza filimbi ya mwisho kumaliza dakika tisini, ndipo kila mmoja atakuwa amefahamu matokeo ya mechi hii. Mechi hii si ya kukosa.

8

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here