Home Michezo Kimataifa EMMANUEL EBOUE ASILITAZAME KABURI LA GARY SPEED, AENDE AKAMSOME THOMAS STRUNZ

EMMANUEL EBOUE ASILITAZAME KABURI LA GARY SPEED, AENDE AKAMSOME THOMAS STRUNZ

1038
0
SHARE
NA NIHZRATH NTANI JNR

TIMU nzima ya gazeti la DIMBA Jumatano inawatakia kheri na fanaka katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2018, ambao tumeuanza tangu juzi Jumatatu. Gazeti la Dimba likiwa ndilo kongwe zaidi na linaoongoza kwa habari za michezo nchini, tunasema asante kwa kutuunga mkono kwa mwaka 2017 na tuwe pamoja nasi kwa mwaka mwingine wa 2018. Ahsanteni sana.

Asubuhi moja ya Novemba 27, 2011, mwanamke aitwaye Louise, anashtuka na kujikuta yuko peke yake kitandani. Anabakia kupigwa na butwaa. Si jambo la kawaida kwa mumewe kutokuwa kitandani kwa muda huo.

Anafungua pazia na kutazama nje. Ghafla macho yake yanajikuta yakitazama mwili wa mwanaume ukiwa pembezoni mwa gereji iliyoko ndani, nyumbani hapo.

Kwa haraka aliyokuwa nayo, dakika chache baadaye, mwanamme huyo anajikuta akitazamana na mwili huo unaoonekana kuwa hauna tena uhai na tayari ni maiti.

Dakika nane baadaye polisi wanafika na kuthibitisha kuwa: Mwanaume huyo amekufa. Mwili wa mwanaume huyo ni wa Gary Andrew Speed.

Mtu huyu aliyepata kuitwa Gary Speed, alipata kuwa kiungo mahiri sana katika Ligi Kuu ya England na kuacha rekodi zenye kuvutia. Alikuwa mwanaume hasa ndani ya dimba.

Akiwa na miaka 42 wakati huo, Gary Speed aliamua kukatisha uhai wake kwa kuamua kujiua, ikiwa ni siku moja tu baada ya kukutana na rafiki yake Allan Shearer, baada ya kutazama mechi kati ya Manchester United na Newcastle United katika dimba la Old Trafford. Huzuni ilioje!

Nyuma ya kifo cha Gary Speed, inaelezwa kuwa ni kutokana na mgogoro kati yake na mkewe kuhusu ndoa yao.

Gary Speed hakuweza kukabiliana na ukweli kuhusu kufikia mwisho wa ndoa yake. Hakutaka kuuona mwisho wa ndoa yake ukifikia kwa namna hiyo.

Haraka akajiua kuepuka fadhaa kama inayomkumba Emmanuel Eboue, wakati huu ambapo mwili wake ukiwa umelala pembezoni mwa ardhi ndani mji wa Hawarden, huko Wales.

Uamuzi aliouchukua Gary Speed unapaswa si tu kupingwa, bali kuchukuliwa wa kipuuzi zaidi miongoni mwa wanaume wengi.

YALIYOMTOKEA EBOUE NI FUNDISHO KWA WANASOKA WENGI

Hali ya maisha ya beki wa zamani wa klabu ya Arsenal ya England, Emmanuel Eboue, imebadilika mithili ya upepo.

Alizaliwa katika maisha yaliyojaa umaskini kule Abidjan, nchini Ivory Coast. Lakini ghafla kupitia miguu yake akajikuta akipata utajiri wa haraka akiwa na umri wa chini ya miaka 33 tu. Inasisimua.

Katika umri wa miaka 34. Historia ya Eboue inabadilika haraka na inapaswa kuanza kuandikwa upya. Hii inatokana na kufikia mwisho wa ndoa yake.

Matokeo ya talaka kutoka mahakamani yanamfanya Eboue kubakia maskini wa kutupwa akiwa hana hata pauni 1000 kutoka kumiliki mamilioni ya Pauni. Inasikitisha.

Kwa sheria na maelekezo ya talaka hiyo, mali zote alizochuma Eboue katika kipindi chake chote cha  soka lake, zinapaswa kubakia chini ya umiliki wa mtalaka wake, huku pia akikosa fursa ya kutowasiliana na watoto wake watatu aliozaa na mwanamke huyo. Inaumiza sana.

Eboue yupo katikati ya mawazo ya umauti na uhai. Ni wakati mbaya zaidi kwa mwanaume katika maamuzi.

Gary Speed alishindwa kukabiliana na hali hii hata kabla ya ndoa yake kufikia hatua ya talaka. Ni yupi mwanaume shujaa mbele ya mwanamke?

ALIPASWA KUJIFUNZA KUTOKA KWA THOMAS STRUNZ

Mnamo mwaka 1990, Stefan Effenberg aliwasili katika viunga vya Uwanja wa Sabener Strabe. Ni uwanja wa mazoezi wa timu ya Bayern Munich, akiwa kijana mdogo.

Ni mahala hapo ndipo alipokutana na mvulana mwingine aliyeitwa Thomas Strunz. Wote wawili walikuwa wachezaji wa Bayern Munich.

Stefano Effenberg akitokea Borussia Monchengladbach, huku Thomas Strunz akiwa hapo tangu 1989 akitokea MSV Dulsburg.

Urafiki wa wanaume hawa wawili ndipo ulipozaliwa katika viwanja hivyo vya Sabener Strabe, wote wawili wakicheza nafasi ya kiungo klabuni hapo.

Miaka miwili baadaye marafiki hawa walitengana. Stefano alirejea Borrusia M’gladbach, huku Thomas akienda VFB Stuttgart.

Miaka mitatu baadaye Thomas alirejea tena Bayern Munich, akiwa tayari ameoa mwanamke mrembo aliyeitwa Claudia Strunz.

Miaka saba baadaye tangu alivyoondoka Bayern, Stefano alirejea kunako klabu ya Bayern Munich akiwa naye ameoa mwanamke aliyeitwa Martina. Urafiki wa Stefano na Thomas ukashamiri tena.

Mwaka huo huo siku moja katika majira ya kiangazi, yaani mnamo mwaka 1998. Familia za marafiki hawa wawili zilijumuika katika ukumbi wa starehe wa P1 Club, uliopo katika mji wa Munich.

Thomas Strunz akiwa na mkewe wa ndoa na mama watoto wake wawili, Claudia Strunz, huku Stefano Effenberg akiwa na mkewe wa ndoa na mama watoto wake watatu Martina Effenberg walikutana kwa mara ya kwanza.

Ni mahala hapo kwa mara ya kwanza macho makali ya Stefano Effenberg yalipotua machoni mwa Claudia ambaye ni mke wa Thomas. Moja kwa moja hisia za kimapenzi zikaibuka kati kati yao.

Si Stefano wala Claudia aliyeweza kuvumilia. Kila mmoja alimuona mwenza wake wa ndoa kuwa sio chaguo sahihi.

Mapenzi yana nguvu sana. Baada ya tukio hilo hayakuwepo mapenzi ya dhati tena kwa wenza wao. Kiapo cha kanisani kikawekwa kapuni.

Wakaanza kusalitiana na miaka miwili baadaye Stefano Effenberg alimtaliki mkewe Martina kwa uchungu mwingi. Na wakati huo huo, Claudia Strunz naye akaomba talaka kwa mumewe Thomas Strunz. Ndoa zikavunjika.

Mnamo mwaka 2004. Stefano Effenberg na Claudia walifunga ndoa kwa furaha kubwa. Mpaka hivi leo wanaishi kwenye ndoa yenye furaha sana wakiwa katika Jimbo la Florida nchini Marekani.

Miezi michache baadaye, Thomas Strunz alihojiwa na jarida moja la Ujerumani kuhusiana na kunyang’anywa mke na rafiki yake ambaye alikuwa mchezaji mwenzake.

Strunz alieleza kuwa;

“Ulikuwa wakati mgumu kwa upande wangu kukubali hali hii. Nilikuwa na vitu vingi kichwani, hata hivyo niligundua kila kitu kilichotokea kilikuwa na sababu. Pengine Claudia aliumbwa kwa ajili ya Stefano na kuwa nami ilikuwa kama njia ya kutimiza maandiko.”

Bila shaka ilikuwa ngumu kukabili na miezi miwili au mitatu sikuweza kuamini. Niliumia sana lakini nilitumia muda mwingi kusoma vitabu. Ni vitabu pekee vilinipa faraja na kuchukulia kama jambo la kawaida.”

Tukio hili lilinipa changamoto kubwa katika maisha yangu. Kwa sasa sina tatizo na Stefano, pia sina tatizo na Claudia. Siku zote napenda kuwaona wakiwa na furaha,” alimaliza.

Stefano Effenberg na Thomas Strunz walikuwa katika kikosi cha Bayern Munich kilichokuwa kinatisha enzi hizo wakiwemo Mehmet Scholl, Oliver Kahn, Lothar Matthaus, Mario Basler na wengineo.

Thomas Strunz alikubaliana na ukweli. Alipoteza utajiri wake na alikubali kuanza moja. Leo hii Thomas Strunz amekuwa mfano bora wa wanandoa wengi waliotalikiana hasa kwa upande wa wanaume.

Maskini Gary Speed hakutambua kile alichokitambua Thomas. Kuwa kila jambo hutokea kwa sababu.

Ni Simulizi hii ndio inayopaswa kusomwa na Emmanuel Eboue. Bahati nzuri Eboue ameshatoka hadharani na kusema maumivu yake.

Baadhi ya watu watabakia kumcheka na wengine watamshauri vyema. Ila uzuri ni kuwa amesema katika jamii kile kinachomuumiza. Ni ngumu kujiua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here