Home Michezo Afrika EMMANUEL OKWI MATAJI MBONA YANAKUJA SIMBA TU!

EMMANUEL OKWI MATAJI MBONA YANAKUJA SIMBA TU!

1193
0
SHARE

NA MARTIN MAZUGWA

UNAPOTAJA majina ya wachezaji waliojijengea jina kubwa kwa mashabiki wa Simba miaka ya hivi karibuni, huwezi kulikosa jina la straika Mganda Emmanuel Anorld Okwi, nyota huyo wa ‘The Cranes’ mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu.

Mashabiki wa Simba wamekuwa wakimuimba kama mfalme wao mara baada ya Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’ ambaye ni mchezaji pekee kuifunga Yanga mabao matatu ‘hat trick’.

Okwi anasema kuwa anajiona kama vile amezaliwa upya katika kikosi cha Simba, kwani kikosi alichokikuta si kile alichokiacha. Mganda huyo ambaye amewahi kupita katika klabu za Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka (2012), SC Villa ya Uganda, Yanga mwaka (2013) pamoja na Sonderjyske ya Denmark mwaka (2015) ambazo amecheza kwa vipindi tofauti huku timu pekee aliyong’aa ikiwa ni Simba.

Dimba limemtafuta nyota huyo na kufanya naye mahojiano kuhusu maisha yake katika mchezo wa soka mambo aliyopitia hadi hapo alipofika hivi sasa na kwanini ameamua kurudi Simba.

DIMBA: Unakionaje kikosi cha Simba cha hivi sasa?

Okwi: Japokuwa sijapata nafasi  ya kuona vikosi vingi vya timu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini naamini kati ya timu zilizofanya usajili bora na wenye tija msimu huu, ni klabu yangu ya Simba kwani ina mchanganyiko mzuri wa wachezaji wazoefu pamoja na vijana ambao watakuwa silaha katika mapambano ya msimu wa 2017/18.

DIMBA: Ulikuwa nje ya Ligi ya Tanzania kwa kipindi kirefu je, ulikuwa ukiifuatilia?

Okwi: Unajua sisi wachezaji maisha yetu si ya eneo moja tunazunguka sana, nilikuwa naifuatilia mara kwa mara sababu ni kati ya Ligi Bora kabisa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

DIMBA: Ulipokuwa Tanzania ni timu gani ilikuwa ikikusumbua sana unafikiri ulivyorudi itakupa kikwazo tena?

Okwi: Timu zote zilizokuwa zikishiriki Ligi Kuu Bara ni bora lakini kama mchezaji nilikuwa najituma kuhakikisha naisaidia timu yangu kupata  matokeo mazuri ili kuwafurahisha mashabiki wangu.

DIMBA: Timu gani unahisi itawasumbua katika harakati zenu za kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara?

Okwi: Unapotaja Ligi Kuu ya Tanzania Bara unaizungumzia Simba na Yanga ambazo ni timu kubwa, mimi naamini itakuwa vita ya timu  hizi mbili japokuwa kwa maandalizi tuliyofanya hakuna wa kutuzuia kutimiza malengo tuliyojiwekea msimu huu.

DIMBA: Kwanini uliamua kurudi Simba na si Yanga licha ya kupitia katika klabu zote mbili?

Okwi: Kila mtu anapenda kukaa sehemu nzuri na yenye amani ambayo itamfanya afanye kazi kwa moyo, si kwamba Yanga ni timu mbaya la hasha, ni timu nzuri lakini timu ambayo inanipa uhuru ni Simba ambayo ni kama familia yangu kwani nimekuwa nayo kwa muda mrefu na viongozi wake wameonyesha kuniamini sana.

DIMBA: Unauzungumziaje usajili wa Haruna Niyonzima ambaye uliwahi kucheza naye ulipokuwa Yanga umekutana naye pia ukiwa Simba?

Okwi: Haruna ni mchezaji mzuri ambaye kila mtu anatamani kuwa naye na kucheza naye pamoja katika timu moja ana kipaji cha hali ya juu, naamini ujio wake katika klabu ya Simba utaongeza nguvu katika kikosi na harakati za kusaka ubingwa.

DIMBA: Unakionaje kikosi cha Yanga msimu huu?

Okwi: Wana kikosi kizuri nimewaona katika michezo zaidi ya miwili naamini kitatupa changamoto zaidi katika harakati za kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo hii ni mara yangu ya tatu kuja hapa nchini kucheza soka.

DIMBA: Umejisikiaje mara baada ya kubeba taji lako la kwanza na Simba?

Okwi: Nilijisikia faraja sana kwani hiki ndicho kitu kilichonileta tena Simba mashabiki wa Simba wasubiri mambo mengi mazuri yanakuja msimu huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here