Home Michezo Kimataifa ENGLAND ITAMKUMBUKA COSTA KWA MABAO AU VURUGU ZAKE?

ENGLAND ITAMKUMBUKA COSTA KWA MABAO AU VURUGU ZAKE?

660
0
SHARE

LONDON, England

RASMI, Diego Costa anaondoka Cheslea. Anaiacha Premier League na kurejea La Liga. Kwa mashabiki wa soka la England, watamkumbuka Costa kwa lipi?

Mabao yake? Ubabe na vurugu zake? Atakumbukwa kwa lipi Diego Costa?

Ni ngumu kuyasema mafanikio ya Chelsea kwenye misimu mitatu iliyopita bila kulitaja jina la Costa. Amekuwa na mchango mkubwa mno.

Ni wazi kuwa mashabiki wa Chelsea watamkumbuka zaidi Costa kwa mabao yake, lakini wapinzani wao wakawa na kumbukumbu ya straika mtukutu.

Hawa kabla ya kuzungumzia mabao yake na medali alizobeba nchini England, wataanza kukwambia kwanza juu ya viwiko, rafu za kipuuzi na ubabe wa Costa kwa mabeki wa klabu zao.

Katika misimu mitatu aliyokaa Stamford Bridge, Costa amebeba mataji mawili ya Premier, si jambo jepesi hata kidogo. Lakini pia kwenye kipindi hicho, straika huyu ameongoza kwa kuandikwa vibaya na vyombo vya habari vya England.

Costa ni msumbufu. Ni ngumu kuishi naye, anapenda kufanya anachojisikia kufanya. Antonio Conte hakuwa na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kumtimua.

Chelsea ‘watayamisi’ mabao yake na watazimisi pia vurugu zake zilizokuwa zikiichafua taswira ya klabu yao. Ni mkorofi, adui wa wengi japo ni si mtu rafiki sana kwa nyavu za wapinzani wake.

Amefunga mabao 52 kwenye michezo 89, lakini ukijaribu kuipitia kwa makini rekodi hiyo utakumbana na vurugu alizokuwa akizisababisha kwa mabeki wa timu pinzani.

Alichokifanya dhidi ya beki wa zamani wa Arsenal, Gabriel Paulista, Septemba 2015, ni kumbukumbu tosha ya tabia za Costa awapo uwanjani.

Costa alimsababishia Gabriel kadi nyekundu kwa maudhi yake na Chelsea wakashinda mchezo licha ya kupondwa sana na wachambuzi wengi wa soka.

Costa ni mzuri kwa matumizi ya nguvu ambapo straika mpya wa Chelsea, Alvaro Morata, hawezi kumfikia hata mara moja.

Dhidi ya Arsenal, Morata alitulizwa mno na Shkodran Mustafi, kitendo ambacho ni nadra sana kuona kikitokea kwa Costa.

Licha ya kuisaidia Chelsea kubeba taji, bado Antonio Conte aliona ni bora ampunguze kikosini ili kulinda taswira ya klabu na wasifu wake kwa ujumla.

Urafiki wa Conte na Costa ulikuwa wa mashaka sana. Kila mmoja alihitaji kuwa juu ya mwingine na hapa ndipo tofauti zao zilipoanzia.

Jarida la Mirror lilifichua Julai, mwaka huu kuwa Costa aliomba kuondoka Chelsea zaidi ya mara tatu msimu uliopita. Katika dirisha kubwa mwaka 2016, alituma maombi ya kuuzwa, uongozi ukagoma.

Dirisha dogo Januari mwaka huu, aliomba pia akatoswa. Na mapema mwezi Mei baada ya ligi kumalizika, straika huyu akaomba tena kuondoka.

Ikumbukwe pia Januari Costa alionekana kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Atletico bila kuujulisha uongozi wa Chelsea, kitendo kilichomkera mno Conte.

Inadaiwa pia Costa hapendezwi na hali ya hewa ya London. Anataka kurejea Hispania, anapenda maisha ya kule, anapenda pia kuichezea Atletico Madrid.

Ni Costa huyu aliyekuwa akifika mazoezini na Range Rover yake nyeupe akifungulia muziki kwa sauti kubwa na kuvuruga programu za Conte. Vipi angeweza kuvumilika mwanadamu huyu?

Ni ngumu kuyasahau mabao yake na mchango wake kwa Chelsea. Anaondoka na sifa hiyo mgongoni mwake.

Lakini kwa mbali uongozi wa Chelsea utakuwa ukipumua kwa nafuu baada ya kukamilisha uhamisho huo wa Costa. Ni bora wabaki na Morata kuliko kuendelea kuichafua taswira ya klabu yao kwa kuendelea kumvumilia Diego Costa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here