SHARE

NA JOSEPH SHALUWA


WAPO wanawake ambao wamekuwa kwenye uhusiano kwa nyakati tofauti na wanaume tofauti na kuishia kuachwa. Wengine ni warembo kabisa, kiasi kwamba hubaki wameduwaa mara wanapopigwa chini.

Marafiki, kwa bahati sana, urembo au uzuri wa sura ni kati ya sifa isiyo na muhimu sana kwa mwanamume anayetafuta mwanamke wa kuishi naye kwenye ndoa, kuliko sifa nyingine.

Ukweli ni kwamba hakuna kanuni za moja kwa moja kwenye uhusiano, lakini angalau ni vema kuwa na uelewa wa yale mambo ya msingi zaidi kuyafahamu ili kujipa uhakika wa ndoa na boyfriend wako.

Wasichana wanaoachwa, wengi wao hujitathimini sana, lakini hawaoni kasoro iliyowaachanisha na wapenzi wao, ambao awali walikuwa wakitangaza nia ya kuwaoa mara kwa mara.

Inawezekana yapo mambo mengi zaidi, huenda pia yapo unayoyafahamu, lakini mambo haya 7 hapa chini, ukiwa nayo makini, unajisogeza kwenye uhakika wa kuingia kwenye ndoa na boyfriend wako.

EPUKA KUMKOSOA KUPITILIZA

Baadhi ya wanawake wana kasumba hii. Boyfriend wake huenda anazungumza jambo au anachangia hoja fulani, lakini yeye anamkosoa. Mbaya zaidi ukosoaji wake ni ule wa ujuaji, wenye kauli za kutojali na kumuonyesha kuwa anajua zaidi.

Bahati mbaya wanaume kwa namna walivyoumbwa, kihulka hawapo tayari kuwa chini ya wanawake na hawajisikii vizuri kuonekana hawajui. Acha tabia ya kumkosoa mpenzi wako, hata kama una hakika anachosema siyo sahihi.

Lakini kwa uhusiano mzuri, wenye urafiki, zipo njia nzuri za heshima za kumkosoa mpenzi wako kwa hoja na si kumwonyesha kuwa ‘yeye siyo lolote’, bali hana elimu au uelewa wa jambo hilo.

Mfano unaweza kumwambia, “Baby, lakini ujue unavyosema ni sawa, lakini kwa ninavyojua ni hivi…” kwa lugha nzuri kama hii, mwanamume wako atakuwa tayari kukusikiliza na hutakuwa umemjeruhi hisia zake kwa kumuonyesha kuwa hana uelewa wa mambo.

STAHA MBELE ZA WATU

Kipengele hiki hakina tofauti sana na kilichopita, ila cha msingi hapa ni mbaya zaidi kumkosoa mbele za watu. Njia nzuri zaidi, mwenzi wako anapokosea mbele za watu, mpe ishara asiendelee kushikilia hoja yake, kisha baadaye mkiwa wawili unaweza sasa kuzungumza naye kwa utaratibu nilioelekeza kwenye kipengele kilichopita.

Mwanamume hapendi kuonekana hajui mbele ya mwanamke. Ukiwa kulinda heshima yake, hadhi na hisia zake za kiume, mawazo ya kukuoa hayatayeyuka kichwani mwake.

KUWA MKALI

Inawezekana mna mjadala fulani, mpo peke yenu mahali. Zuia hisia zako na kuwa mkali, hasa ule wa kukaripia. Mwanamke anapaswa kuwa mnyenyekevu kwa mwanamume wake.

Kitendo cha kuonyesha ukali kwa boyfriend wako, kitampa taswira kuwa hata kwenye ndoa mnayoendea, kelele na kumshushia heshima ndipo kutakapotawala uhusiano wenu, jambo ambalo litamfanya aondoe kichwani wazo la kufunga ndoa nawe.

KUMLINGANISHA

Epuka kabisa kumlinganisha mwanamume wako na mwanamume mwingine. Wapo baadhi ya wanawake wana hulka hiyo. Wanapokuwa kwenye mijadala fulani au kuelekezana kitu kinachohusu majukumu yao, hulinganisha. Ni kosa.

Utamsikia mwanamke anasema, “Jifunze kwa wanaume wenzako, ona Jumanne anavyofanya kwa mpenzi wake Mayasa.”

Kufanya hivyo ni kumuumiza mpenzi wako, lakini pia kutapunguza mapenzi na mawazo ya kukuoa. Mwanamume anapenda kuwa halisi, wa kipekee na asiyelinganishwa na yeyote.

Mwanamume huamini alivyo, yupo tofauti na mwanamume mwingine yeyote kwa kila kitu, kumlinganisha ni kumfukuza mikononi mwako.

 

USIKUBALI FARAGHA

Wanawake wengi hawajaelewa hili, lakini ukweli ni kwamba ili kumpa mwanamume mshawasha wa kukuoa jiweke mbali na mazingira yatakayorahisisha kukutana kimwili. Ni vizuri zaidi ikiwa kwenye uhusiano wenu kati ya ahadi muhimu iwe na ya kukutana kimwili mtakapokuwa kwenye ndoa.

Mwanamume anaweza kusukumwa na kiu ya kingono tu, lakini akishakupata huenda akakutana na vitu asivyotarajia na hapo ukawa mwisho wenu. Jiulize, utajaribiwa na wangapi?

Kama mwanamume atafanya sababu ya kukataa kwako faragha kabla ya ndoa, ndiyo ya kuahirisha ndoa na wewe, mruhusu aende salama kuliko kugeuzwa wa majaribio. Msimamo wako utamfanya aone anakwenda kumuoa mwanamke mwenye heshima, anayejitunza na kuhifadhi maadili.

Kama bado unao usichana wako ni vizuri zaidi, lakini hata kama ulishafanya kosa, siyo mbaya kuanza kujilinda kwa upya ili mwisho wa siku uingie kwenye ndoa ukiwa mpya kabisa kwa mumeo.

 

ACHA KUOMBA SANA PESA

Hili limekuwa tatizo kwa wanaume wengi. Ni kweli mwanamume ana wajibu wa kumtunza mwanamke wake, lakini usimgeuze mradi. Kwani kabla ya kuwa naye, ulikuwa unaishije?

Ulikuwa huli? Hununui manukato nk? Jibu ni hapana. Jenga utaratibu wa kumvumilia ili akitaka kukusaidia fedha afanye yeye mwenyewe na siyo kwa shuruti zako. Ukiendekeza pesa sana, atakupiga chini na kusubiri mwingine.

MITINDO ISIYO NA STAHA

Kwenda na wakati kumetaka kuharibu wasichana siku hizi. Kuna mavazi ya kubana au kuacha nusu ya sehemu ya mwili nje kwa kuamini ndiyo kuvutia – siyo kweli.

Ukiona mwanamume anakusifia kwa mavazi yako ya ovyo, ujue hana nia ya kukuoa, anakutumia kama chombo chake cha starehe na siku ya kuoa ikifika, atamtafuta mwanamke mwenye maadili.

Usiwe hivyo, linda utamaduni wetu, heshimu uanamke wako kwa kuvaa mavazi ya heshima na kutengeneza nywele zako katika mitindo inayokubalika.

Je, unapenda kujifunza masomo haya zaidi kwa njia ya simu? Wasiliana nami kwa simu 0712 170745/0763 255818.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano. Ameandikia vitabu vingi, vikiwamo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here