Home Makala EURO 2016; NANI KUIBUKA BINGWA?

EURO 2016; NANI KUIBUKA BINGWA?

368
0
SHARE
Mabingwa wa michuano hiyo mwaka 2012, timu ya taifa ya Hispania wakifurahia
Mabingwa wa michuano hiyo mwaka 2012, timu ya taifa ya Hispania  wakifurahia
Mabingwa wa michuano hiyo mwaka 2012, timu ya taifa ya Hispania wakifurahia.

NA MARKUS MPANGALA,

SIKU hizi mabosi wangu wa Dimba wamekuwa wakali kweli kweli, bila shaka wana usongo na michuano ya Kombe la Ulaya yaani Euro 2016. Kila siku wanakuja na kipya na hawachoki kuchapa kazi. Nikiwatazama huwa nafurahishwa na bidii yao.

Sasa kilichonichekesha ni kunipiga mkwara ili nizungumze nawe msomaji wetu. Basi, kwakuwa michuano ya Ulaya ndiyo iliyopo karibu basi ngoja tuone kuzungumzia mambo mawili au matatu.

Michuano ya mwaka huu inafanyika nchini Ufaransa na kuzishirikisha timu 24. Kwa mujibu wa shirikisho la soka la Ulaya timu inayoshika nafasi ya tatu inaweza kufuzu hatua ya pili. Hivyo kundi moja linaweza kuwa na timu tatu.

Binafsi nafuatilia habari nyingi za michuano ya Euro ili kulinganisha na tuliyoshuhudia huko nyuma. Jambo la kujiuliza hapa ni nchi gani inaweza kuwa bingwa wa michuano ya mwaka huu.

Makala haya na yajayo nitakuwa nitaelezea kundi la timu ambazo zinaweza kunyakua ubingwa mwaka huu.

WAJUKUU WA MALKIA

England kwa miaka yote huwa wanatia huruma kwenye mashindano ya kimataifa. Wanaweza kushinda mechi nyingi za kirafiki, lakini wanakuwa si hodari kwenye mashindano.

Nakumbuka mwaka 2001 waliifunga Ujerumani mabao 5-1 kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia. Michael Owen alipachika mabao matatu, halafu  Steven Gerrard na Emile Heskey wakaongeza mawili kwa England. Bao la kufutia machozi kwa Ujerumani lilifungwa na Carsten Jancker.

Lakini linapokuja kwenye mashindano wajukuu wa malkia hawana ubavu wa kupambana. Ujerumani ikafika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002, lakini England wakaishia robo fainali.

Mashindano ya kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 1996 iliniachia kumbukumbu moja muhimu sana. Michuano hiyo ilifanyika nchini England na wenyeji walikuwa na matumaini makubwa.

England imeandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1966 wakatwaa baada ya bao lao la tatu lililofungwa na Geoff Hurst kukubaliwa na mwamuzi licha ya kudaiwa kugonga mwamba na kutogusa mstari.

Wajerumani walilalamika sana lakini haikufua dafu. Sasa kwenye michuano ya mwaka 1996 walifika hadi nusu fainali dhidi ya Ujerumani. Bahati mbaya kwao walishuhudia penalti ya Gareth Southagate ikiota mbawa.

Na huo ukawa mwisho wa michuano kwao. Katika michuano hiyo shujaa wa Ujerumani alikuwa Andreas Kopke, Markus Babbel, Christian Ziege, Jurgen Klinsmann. Hao ni wachezaji niliokuwa nawakubali mno.

Euro 1996 limekuwa kama jinamizi la England kwenye mashindano. Wamekuwa wakifurukuta mara kwa mara lakini hawapiti wala kufika kokote. Michuano ya mwaka 2000 wakiwa chini ya kocha Kevin Keagan waliambulia patupu.

Nakumbuka walipangwa kundi A wakiwa na Ureno, Romania na Ujerumani. Cha ajabu England iliambulia pointi 3 na Ujerumani pointi 1 kwenye kundi hilo. Ureno na Romani zikafuzu.

Euro 2000 iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Uholanzi na Ubelgiji, tulishuhudia Ufaransa ikikabidhiwa ubingwa. Nahodha wao alikuwa Didier Deschamps ambaye ni kocha wao kwa sasa.

Kwa England wakaona labda watajaribu kwenye Kombe la Dunia mwaka 2002 wakiwa na kocha mpya wa kigeni Sven Goran Eriksson. Kumbuka mwaka 1998 kwenye fainali za Kombe la Dunia walikuwa chini ya kocha mzawa, Glenn Hoddle.

Baada ya kuwatumia makocha wazawa England ikabadilika na kumpa kazi Ericksson lakini wakaishia robo fainali. Euro 2004 nchini Ureno waliishia hatua ya robo fainali baada ya kutolewa na wenyeji Ureno.

Ni michuano hii ndiyo ilionyesha uwezo mkubwa wa Wayne Rooney. Kwenye Euro 2008 England haukufua dafu na ikashuhudia

Hispania ikitawazwa kuwa mabingwa kwa bao la Fernando Torres. Ikaja Euro 2012, England haikuwa na chake. Sasa Euro 2016 England wameingia kwa namna ya pekee.

Wanaweza kucheza 3-4-3 kama watakuwa na kiungo Jack Wilshere. Katika mfumo huu Wilshere ndiye namwona kiungo mbunifu na fundi zaidi kuliko alionao kocha Roy Hodgson.

Michuano hii wameingia na vijana wenye ari; kuna Harry Kane, Dele Ali, Marcus Rashford, Eric Dier, Nathaniel Clyne na wengine. katika kikosi hiki safu ya ushambuliaji kuna Jamie Vardy wa Leicester.

Asilimia 80 ya kikosi cha England kinaonesha kama hawaaminiki. Kwanza hakina mastaa wakubwa ukiondoa Wayne Rooney na Daniel Sturridge. Kama kocha wao atapanga 4-3-3 basi atahitaji uwezo wa Dele Ali, Harry Kane na Rooney kuongoza mashambulizi huku Sturridge na Vardy wakiwekwa benchi.

Pia James Milner anaweza kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika nafasi ya kiungo iwe kulia pembeni au kushoto pembeni.

Mara zote Sturridge hakupi asilimia 100 ya uwezo wake. Amekuwa mshambuliaji wa nusu-kazi. Hili si jambo zuri kwa kocha. Lakini kutokana na matatizo ya kisaikolojia ya kutofanya vizuri.

Wataanza kampeni zao dhidi ya Urusi na kwa vyovyote kundi lao si tishio. Je, ni wakati wa England kuibuka kuwa bingwa? Wanafikiriwa.

MSHTUKO WA 2004

Hapa tuweke nafasi ya timu inayoweza kushtua kwenye michuano ya Euro 2016. Kila michuano inapoibuka kunakuwa na taifa lisilotegemewa kufanya vizuri.

Nauchukua mwaka 2004 jinsi Ugiriki ilivyoibuka kuwa bingwa wa Ulaya mbele ya wenyeji Ureno. Likiwa taji la kwanza kwa kocha Otto Rehhagal. Bao la Angelos Charisteas lililowazamisha Ureno.

Ugiriki ilikuwa ikicheza soka la kujihami muda wote wa mchezo. Fowadi wao alikuwa Charisteas peke yake mbele huku wachezaji wengine 9 wakicheza katika eneo lao. Ugiriki ilishangaza kwenye michuano hiyo na bila shaka mwaka huu tunaweza kushuhudia hilo.

HISPANIA LA ROJA

Hispania ni mabingwa watetezi. Kikosi chao kipo chini ya kocha Vicente Del Bosque, tangu alipopokea timu hiyo kutoka kwa marehemu Luis Aragones aliyetwaa taji la Euro mwaka 2008.

Del Bosque amepata mafanikio makubwa katika kikosi hicho, alitwaa Kombe la Dunia 2010, akatwaa taji la Ulaya mwaka 2012 na sasa anafukuzia taji la tatu.

Kikosi chake bado kinawategemea mastaa waliotwaa taji hilo. Iker Cassilas, Gerarrd Pique, Jord Alba (aliyechukua nafasi ya Capdevilla), Sergio Busquet (amechukua nafasi ya Marco Senna), Sergio Ramos, Pedro, Cesc Fabrigas bado wapo kikosini.

Je, La Roja wataweza kutetea taji lao? Udhaifu wa Hispania ni kumiliki mpira muda mrefu na kushindwa kupata plan B.

Wanategemea vipaji vya mastaa wao, lakini kama watakutana na timu inacheza kwa kasi na kujilinda kwa ustadi watapata wakati mgumu. Sitarajii kuona mabadiliko ya mifumo yao ya 3-4-3 au 4-3-3 na 4-1-3-1-1. Safari hii hawana Xavi lakini watakuwa na matumaini makubwa kwa Andre Iniesta.

Tukutane Jumapili wadau.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here