SHARE

NA MWANDISHI WETU


MSIMU wa 2015/16, dunia ilishangazwa na kitendo cha aliyekuwa kocha mkuu wa Chelsea, Jose Mourinho, kuamua kulitimua benchi lake la kitabibu lililokuwa chini ya daktari wake mkuu, Eva Carneiro.

Tatizo kubwa lilikuwa kwa daktari huyo kutimiza majukumu yake ya kumtibu Eden Hazard ambaye alionyesha hali ya kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu nchini England dhidi ya Swansea City.

Kitendo cha Eva kwenda kumtibu Hazard kilionekana kama upuuzi flani kwa Mourinho ambapo mawazo yake yote yalikuwa yanataka timu yake iibuke na ushindi kwenye mchezo huo uliomalizika kwa timu hizo kufungana mabao 2-2.

Wakati Mourinho akilazimisha timu yake kuibuka na ushindi mchezo huo uliokuwa ukichezwa nyumbani, tayari kipa wake Thibaut Courtois, alikuwa ameshalimwa kadi nyekundu kutokana na mchezo mchafu aliomchezea straika wa Swansea, Bafetimbi Gomis.

Wala hazikupita siku nyingi baada ya mchezo huo kumalizika, Mourinho akatoa tamko la kumtimua daktari Eva akimshutumu kwenda kumtibu Hazard ambaye kwa madai ya kocha huyo hakuwa ameumia bali alikuwa amechoka tu ndiyo maana akakaa chini madai ambayo yalipingwa kila kona ya dunia.

Bila hiana daktari huyo akafungasha kila kilicho chake na kujiondokea kwani hakuwa na la kufanya kwani hilo lilikuwa agizo la bosi wake wa benchi la ufundi aliyekuwa na njaa ya kutetea ubingwa wao, lakini akiamua kupitia njia iliyoonekana na wengi kuwa haikuwa sahihi.

Tangu kuondoka kwa Eva hali ilianza kuwa mbaya zaidi na timu kuzidi kupata matokeo mabaya na mwisho wa siku Mourihno akaamua kutamka wazi kuwa baadhi ya wachezaji wake muhimu akiwamo Hazard na Diego Costa, wanamhujumu.

Kama Waswahili wanavyosema ukiua kwa upanga utakufa kwa upanga, ndivyo maisha ya Mourinho yalivyokuwa katika kikosi hicho kwani matokeo hayo mabaya yalimfanya mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich, kuchukua maamuzi magumu na kumfuta kazi Mreno huyo.

Kuondoka kwa Mourinho kulisababisha mengi kuzungumzwa mitaani kuwa hiyo ilikuwa laana ya daktari huyo ambaye hakuwa na hatia yoyote na badala yake alikuwa akitimiza majukumu kama ilivyo kawaida.

Mwisho wa siku Mourinho akatimkia Manchester United, ambako hali ilianza kuwa tete wakipata matokeo yasiyoridhisha mpaka mashabiki wao wakaanza kukata tamaa wakijua fika msimu huu utakuwa mwaka wa shetani.

Hata hivyo, mambo yameanza kumnyookea Mourinho kwani timu inashinda na inazidi kuwasogelea wale waliopo mbele yao huku pia wakicheza kandanda la kuvutia na bila shaka mashabiki wao wameanza kurudisha mioyo wakiamini lolote linaweza kutokea mbele ya safari.

Huenda kinyongo alichokuwa nacho Dk. Eva, kimekwisha ndiyo maana Mourinho ameanza kupata ahueni kutokana na ushindi mfululizo wanaoupata huku wakiwakaribia Arsenal ambao walikuwa juu zaidi kuliko wao.

Mwishoni mwa wiki hii Man United watakuwa na kibarua pevu cha kuwakabili Liverpool na kama mashetani hao wekundu watashinda bila shaka watapiga hatua kubwa mbele na kama wanaowatangulia watateleza ni wazi watapanda hatua moja.

Man United wapo nafasi ya sita wakiwa na pointi 39 na kama watashinda dhidi ya Liverpool wanaweza wakapanda hadi nafasi ya tano endapo Arsenal wenye pointi 41 watapoteza mbele ya Swansea City.

Kama Man United wakishinda watafikisha pointi 42, huku wakiwaombea pia mabaya Tottenham na Manchester City wenye pointi hizo 42 wapoteze ili wabakie hapo hapo na hayo yote yatajulikana mwishoni mwa wiki hii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here