Home Michezo Kimataifa FABINHO MIGUU YAKE MIREFU ITATOSHA KUPONYA MAGONJWA MATATU MAN UNITED

FABINHO MIGUU YAKE MIREFU ITATOSHA KUPONYA MAGONJWA MATATU MAN UNITED

472
0
SHARE

MANCHESTER, England

TETESI zinazoihusisha sana Manchester United na viungo wa kati ni juu ya kiungo wa Chelsea, Nemanja Matic.

Viungo wengine wanaotazamiwa kama machaguo mbadala iwapo United itamkosa Matic, ni Eric Dier wa Tottenham Hotspur, Blaise Matuidi (PSG), Kevin Strootman (Roma) na Arturo Vidal wa Bayern Munich.

Lakini pia kuna Mbrazil, Fabinho, ambaye anakipiga Monaco ya Ufaransa, hazungumziwi sana kwa sababu ni asilimia ndogo ya wanaoutambua uwezo wake.

Fabinho, 23, ni kiungo mahiri wa kati mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali za ulinzi na anaonesha kiwango cha uhakika.

Akiwa katika kikosi cha kocha Leonardo Jardim, Fabinho alikuwa akitumika kama kiungo mkabaji, kiungo wa kati na beki ya kulia, maeneo matatu ambayo hakuna ubishi yanahitajika kuongezewa nguvu pale United na Fabinho anaonekana kuwa na uwezo huo. Na hii ndiyo mifumo mitatu ‘mubashara’ inayoelezea namna atakavyotumika.

Viungo watatu

Wakati Paul Pogba anarudi Old Trafford, wengi walihoji kiungo huyo angetumikaje? Lakini Jose Mourinho alishatambua, 4-3-3 ndio mfumo wenyewe kwa ajili ya mchezaji ghali duniani!

Pogba alifanya vizuri sana katika mfumo huo akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa Euro 2016.

Mfaransa huyo hufanya vizuri akiwa na viungo wawili pembeni yake, pia kama alivyokuwa Juventus. Na aliporudi United, uwepo wa Ander Herrera na Michael Carrick ulimpa nafasi ya kung’ara.

Fabinho atakapotua United atakwenda kuchukua nafasi ya Carrick, ikiwa na maana Marouane Fellaini atasubiri kwanza. Fabinho ataongeza kitu kimoja; uwiano wa safu ya kiungo.

Msimu uliopita, Fabinho aliongoza kwa kupokonya mipira mara 80 pale Monaco kwa upande wa Ligue 1, akashikilia nafasi ya pili kwa kuingilia pasi za wapinzani mara 53 na akaongoza kwa kupiga pasi.

Alifanya kazi zote zinazotakiwa kufanywa katika eneo lake na kama mchezaji wa kulipwa. Siyo tu kuvuruga mipango, pia alimaliza nafasi ya tatu kama mchezaji mbunifu zaidi Monaco nyuma ya Thomas Lemar na Bernardo Silva.

Fabinho alifanikiwa ‘kuzitupa’ pasi ndefu 10 na hakuna aliyezifikisha pasi ndefu kwa mhusika zaidi yake (pasi sita), licha ya kwamba anacheza dimba la chini, tofauti na Silva, ambaye ni mshambuliaji zaidi.

Viungo wawili

Sifa kubwa anayoipata N’Golo Kante ni uwezo wake wa kuhimili presha za safu ya kiungo yenye wachezaji wawili.

Ikumbukwe kuwa, Leicester City alikuwa pamoja na Danny Drinkwater, alipotua Chelsea akaungana na Nemanja Matic. Kante amebarikiwa, maana mfumo wa viungo wawili unahitaji uwe na uwezo mkubwa zaidi ya ule unaoweza kuusikia kutoka kinywani.

United haitapata shida kutumia viungo wawili, Fabinho akiwapo, kwa sababu jamaa aliipa Monaco uhakika zaidi katika mfumo wa 4-4-2. Kama ulikifuatilia kikosi hicho, kilicheza bila wasiwasi (rudi kuutazama mchezo wao wa hatua ya 16 bora UEFA dhidi ya Manchester City pale Etihad).

Fabinho anatumia akili sana kucheza mpira, pale Monaco alikuwa akimuachia mwenzake, Tiemoue Bakayoko kazi ya kutumia nguvu, huku yeye akifukia mashimo ya wenzake, kusoma mchezo na kutambua ni maeneo gani anatakiwa awepo ili asiwape nafasi wapinzani kupenyeza mipira ya hatari kwenye nafasi zitakazoachwa na wenzake.

Uwepo wake ulikuwa kama matroni shuleni. Alihakikisha wanafunzi (Lemar na Silva) kuwa huru kufanya kazi zao, alihakikisha usalama unakuwapo ili kuwapunguzia kazi walimu (makocha), kuwa kazi yao itakuwa ni kuandaa mitaala ya kusaka ushindi, na ndiyo maana Radamel Falcao na Kylian Mbappe pamoja na mabeki wawili wa pembeni, Benjamin Mendy na Djibril Sidibe wakawa na moto wa hali ya juu.

Pogba yeye anaonekana kufanya kazi ya ubunifu zaidi kuliko kuharibu mipango. Msimu uliopita alikuwa akisogea mbele na kupenya kwenye mapengo ya wapinzani, sasa ujio wa Fabinho ni msaada kwake.

Mfumo wa 4-4-2 utatumika na Fabinho atakuwa akitumika kuziba pengo lake katikati, lakini pia itambulike Pogba hataweza kucheza kila mechi, hivyo Ander Herrera ni mtu mwingine anayeweza kutumika.

Uwepo wa Fabinho utamfanya Herrera acheze sasa lile soka alilocheza akiwa Real Zaragoza na Bilbao.

Mbadala wa beki ya kulia

Dunia ya soka nayo huwa inabadilika kama kinyonga. Wakati Herrera anatua United akitambulika kama kiungo mchezeshaji, ghafla akawa kiungo wa kati, na Fabinho hapo awali hakuwa kiungo wa kati, alikuwa beki wa kulia!

Antonio Valencia naye alikuwa winga mzuri tu, alipotua United akabadilishwa na kuwa beki wa kulia na ujio wa Fabinho utamfanya apate changamoto ya hali ya juu msimu ujao.

Kwanza ijulikane kuna aina tofauti za mabeki wa pembeni, ukimtazama vizuri Matteo Darmian yeye anacheza kiulinzi zaidi. Valencia mara nyingi hujaribu kushambulia. Daley Blind yeye anaangalia vitu viwili muhimu; kuusoma mchezo na kuhakikisha anatimiza majukumu yake kwa ufasaha, na Luke Shaw huwa ni beki hatari, mwenye kasi nguvu pindi akiwa fiti kiafya.

Ukweli ni kwamba, Fabinho amekamilika kila idara. Msaada wake hautakuwa katika upande wa kulia tu kupandisha na kushusha mashambulizi, bali kusogea katikati na kuwapa sapoti viungo wa kati.

Pia, atamsaidia sana Mourinho kwenye mbinu yake kukaba ‘hadi jasho’, kwani atakaposajiliwa, mfumo wa kujilinda ambao huundwa na watu sita utakuwa na ongezeko la mwamba wa Brazil, na hata itakapotokea Valencia akapandisha mashambulizi, eneo lake la kulia litakuwa salama sababu ya Fabinho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here