Home Makala ‘FANTASTIC FIVE’ NGUVU YA DORTMUND IPO MIGUUNI MWA NYOTA HAWA

‘FANTASTIC FIVE’ NGUVU YA DORTMUND IPO MIGUUNI MWA NYOTA HAWA

7459
0
SHARE

DORTMUND, Ujerumani

TIMU ya Borussia Dortmund inafanya makubwa msimu huu kwenye Bundesliga, ikionesha makali yao hasa katika eneo la mashambulizi, lenye nyota watano wanaotisha zaidi kwa sasa, wakiongozwa na nahodha wao, Marco Reus.

Wanaoshirikiana vyema na Reus kuhakikisha Dortmund inatoa upinzani mkali kwa wababe wa Bundesliga, Bayern Munich, ni kinda Jadon Sancho, straika wa zamani wa Barcelona, Paco Alcacer, Jacob Bruun Larsen na Christian Pulisic.

Aidha, nyota hao wameirudisha Dortmund ile ya mwaka 2011 na 2012 ambayo ilitikisa Bundesliga kwa kutwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi hiyo, ambapo Reus alikuwamo sambamba na Robert Lewandowski na Mario Gotze.

Kikosi cha Dortmund cha msimu huu kimeonekana kuwa hatari kutokana na uwezo wa wachezaji hao wenye vipaji vikubwa vya kutengeneza nafasi na kufunga mabao, wakiwa na takwimu nzuri mno msimu huu.

Makali yao katika kutafuta mabao yameifanya Dortmund iongoze msimamo wa Bundesliga, ikiwa imefunga jumla ya mabao 23 katika mechi saba za kwanza, huo ukiwa ni wastani wa kufunga mabao matatu kwa mechi.

Hata hivyo, kilichoifanya Dortmund iwe hatari zaidi ni jinsi wachezaji hao wanavyoshirikiana kuubeba mzigo wa kufunga mabao kuliko kumtegemea mtu mmoja. Kila mmojawao amekuwa akichangia kufunga na kutoa ‘asisti’, si Bundesliga tu, na katika michuano yote.

Reus – mabao sita, asisti nne

Wakati Dortmund ilipokuwa na wapachika mabao kama vile Lewandowski na Pierre-Emerick Aubameyang, Rues yeye kazi yake ilikuwa ni kutengeneza nafasi ili wao wafunge mabao. Lakini msimu huu, amekuwa akifanya shughuli zote mbili kwa umahiri mkubwa.

Mpaka sasa amekwishatupia kambani mara sita na kutoa asisti nne kwa wenzake, akitarajiwa kuifikia rekodi yake bora ya msimu wa 2013/14, ambayo alipachika mabao 21 na kutoa asisti 20.

Licha ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, Reus bado anaonekana kuwa na makali yaleyale hata anapokuwa katika timu yake ya taifa ya Ujerumani, na sasa amepata msaada mkubwa kutoka kwa vijana wanne wanaotisha Bundesliga.

Sancho – bao moja, asisti saba

Mapema wiki hii Sancho alifanikiwa kuwa Mwingereza wa kwanza kuzaliwa mwaka 2000 na kuitwa timu ya taifa ya England ya wakubwa, lakini si jambo la ajabu sana.

Kitendo cha kocha wa England, Gareth Southgate, kumjumuisha Sancho katika kikosi chake kimetokana na msaada mkubwa ambao kinda huyo amekuwa akiutoa katika timu ya Dortmund.

Sancho alianza kuonesha cheche zake katika msimu wa kwanza Bundesliga (2017/18) kwa kutoa asisti nne katika mechi 12 alizocheza, na msimu huu tayari ameshavuka idadi hiyo, huku akifunga bao moja Dortmund ilipoibamiza Nuremberg mabao 7-0.

Dortmund haijataka kuchelewesha. Tayari imeshamwongezea mkataba kinda huyo hadi mwaka 2022. Itakuwa ni mwendo wa miaka minne ya timu hiyo kufaidika na kipaji cha Sancho, mwenye kasi, chenga zisizotabirika, mkokotaji mzuri wa mpira na jicho la goli.

Bruun Larsen – mabao matatu, asisti mbili

Kama hujawahi kumtazama kinda huyo wa Denmark akifanya yake dimbani, hebu tafuta muda kuiangalia Dortmund ikicheza, kwa mara ya kwanza unaweza kumfananisha na Reus, si kwa sura, bali uchezaji.

Bruun Larsen amekuwa akicheza soka linalofanana sana na Reus, hiyo ikitokana zaidi na kwamba, kinda huyo amejifunza vitu vingi kutoka kwa mshambuliaji huyo anayevutiwa naye tangu akiwa mdogo.

Wanasema ukijifunza kwa anayejua, lazima na wewe ujue tu. Hadi sasa Bruun Larsen ametikisa nyavu mara tatu na kutoa asisti mbili, likiwemo bao la kwanza Bundesliga na katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ni wazi kwa sasa Dortmund imempata mrithi wa Reus, ambaye ni Bruun Larsen.

Pulisic – mabao mawili, asisti moja

Bruun Larsen si anafanana uchezaji na Reus, basi hiyo haitoshi. Kuna hii nyingine, yeye na Pulisic wamepishana siku tu za kuzaliwa.

Pulisic, mwenye uwezo mkubwa awapo na mpira, hasa kuumiliki na kuanzisha shambulizi, alizaliwa siku moja kabla ya Bruun Larsen mwaka 1998, na aliwahi kuingia akademi ya Dortmund kabla ya mwenzake huyo.

Kiwango chake pamoja na Bruun Larsen kimemuibua hadi kocha wa zamani wa Dortmund, Jurgen Klopp, ambaye anajuta kuondoka mapema na kukosa nafasi ya kuwanoa vijana hao wenye vipaji vya hali ya juu, licha ya kwamba alikuwa nao akina Lewandowski na Gotze.

Hata hivyo, hasara kwake ni faida ya kocha wa sasa wa Dortmund, Lucien Favre, ambaye amemkuta Pulisic na kugundua anafiti vyema katika falsafa yake ya mashambulizi ya kushtukiza.

Nguvu na uelewano kati yake na akina Reus na Sancho, umeifanya Dortmund kutokuwa na wasiwasi na suala la mabao msimu huu.

Alcacer – mabao sita

Wikiendi iliyopita Alcacer aliwashangaza wengi kwa kuifungia timu yake ya Dortmund ‘hat-trick’ ya kwanza ndani ya dakika 34, wakati vijana hao wa Favre walipoibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Augsburg.

Baada ya kuwa nyota wa mchezo huo, orodha ya wafungaji Bundesliga msimu huu ikasomeka yeye ndiye kinara mwenye jumla ya mabao sita, huku akiwa amecheza dakika 81 tu msimu huu.

Kwa hakika, Dortmund imebarikiwa kuwa na utajiri wa wachezaji wote hawa wenye uwezo wa kutengeneza mabao, jumlisha na Alcacer, anayezitikisa nyavu kama kichaa.

Alcacer ametua Dortmund msimu huu akitokea Barcelona kwa mkopo. Akiwa Katalunya, Alcacer hakuwahi kupata huduma bora ya asisti kama anayoipata akiwa Ujerumani, ambako katika mechi yake ya kwanza tu alitupia bao na kuonesha dalili nzuri mno.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here