Home Makala Faustino Asprilla alivyoiachia dunia kumbukumbu ya chenga

Faustino Asprilla alivyoiachia dunia kumbukumbu ya chenga

679
0
SHARE

NA HENRY PAUL,

UNAPOZUNGUMZIA historia ya wachezaji waliokuwa na uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kuchezea mpira kama wanavyotaka, kamwe huwezi kuacha kulitaja jina la mshambuliaji raia wa Colombia, Faustino Asprilla.

Asprilla anakumbukwa na wapenda soka duniani kote kutokana na kwamba alikuwa na kipaji cha kipekee cha kuwasumbua mabeki kwa kuwapiga chenga kama anavyotaka na hatimaye kwenda kupachika bao.

Nyota huyu ambaye alikuwa anamudu kucheza vyema nafasi zote za ushambuliaji, lakini ilikuwa ni burudani alipokuwa akicheza winga ya kulia, ambapo alikuwa anawatesa mabeki waliokuwa wakimkabili kwa kuwapiga chenga na mara nyingi mabeki hao kutokana na kushindwa kumkabili walikuwa wakimchezea rafu.

Asprilla akiwa na timu yake ya Taifa ya Colombia katika michuano ya kufuzu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina iliyochezwa Buenos Aires mwaka 1993, nyota huyo aliifungia timu yake mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-0 na hivyo kuiwezesha kufuzu kucheza fainali hizo mwaka 1994.

Katika michuano hiyo ya kufuzu fainali hizo za mwaka 1994, Asprilla akicheza na nyota wengine wawili, viungo mahiri Carlos  Valderrama na Freddy Rincon alinga’ra, huku akionyesha uwezo mkubwa.

Pia katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1998, Asprilla aling’ara tena pamoja na timu ya Colombia kutolewa katika hatua za awali ambapo ilishinda mechi moja na kufungwa mechi mbili.

Katika ngazi ya klabu Asprilla aling’ara akiwa na Atletico Nacional ya Colombia, Parma ya Italia, Newcastle United ya England na Palmeiras ya Brazil, ambapo wakati huo alikuwa na kiwango cha juu.

Akiwa na klabu ya Parma ya Italia katika misimu mitatu aliyokaa na klabu hiyo kuanzia 1992 hadi 1995, Asprilla alikuwa ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha kupata mafanikio ambapo msimu wa kwanza katika ligi ya Serie A, ilimaliza ikiwa nafasi ya pili, msimu wa pili ilimaliza ikiwa nafasi ya tano, huku msimu wa mwisho ikimaliza ikiwa tena nafasi ya tatu.

Pia akiwa na klabu hiyo misimu miwili 1994/1995, 1998/1999, Asprilla alikuwa ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha kutwaa Kombe la UEFA.

Akiwa na Palmeiras ya Brazil, Asprilla mwaka 2000 alikuwa ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha kutwaa taji la michuano ya Rio Sao Paulo na ubingwa wa Brazil.

Ufundi na utaalamu wa kupiga chenga alizokuwa akifanya nyota huyu kwa kiasi kikubwa unaweza ukafananishwa na mshambuliaji wa zamani wa Tanzania, Malota Soma, maarufu ‘Ball Juggler’, ambaye alitamba akiwa na klabu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars.

Malota alikuwa ni miongoni mwa washambuliaji wachache nchini aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kuchezea mpira kama anavyotaka na kuwafanya mashabiki wa Simba kumbatiza jina la ‘Ball Juggler’.

Nyota huyu, ambaye alikuwa na umbo la kimpira, alikuwa na uwezo wa kupiga chenga mabeki hata watano na kupachika bao.

Malota alijiunga na Simba mwaka 1981 akitokea katika klabu ya Zaragoza ya Morogoro. Mshambuliaji Zamoyoni Mogela, maarufu ‘Golden Boy’ baada ya kujiunga na Simba mwaka huo wa 1981 aliwaambia viongozi wa Simba kuwa kama wanataka afunge mabao, basi wamchukue Malota.

Mogela alikuwa na Malota pamoja klabu ya Zaragoza, Morogoro na ndiye aliyekuwa akimwezesha kufunga mabao, kwani Mogela alikuwa akipewa pasi za mwisho ambazo ilikuwa rahisi kupachika mabao.

Baada ya wawili hao kujiunga na Simba, timu hiyo yenye maskani yake makuu Mtaa wa Msimbazi ikawa moto katika safu ya ushambuliaji kwa sababu Malota alikuwa anapiga chenga karibu mabeki wote na hatimaye kumpasia Mogela afunge kirahisi.

Lakini hata hivyo, Malota baada ya kujiunga na Simba aliwaambia viongozi wa Simba kuwa kama wanataka yeye acheze vizuri na kusababisha kufunga mabao basi wamsajili Thobias Nkoma, ambaye naye walikuwa naye klabu ya Zaragoza ya Morogoro.

Viongozi wa Simba walikubali ushauri huo na mwaka huo huo wa 1981 wakamsajili beki Thobias Nkoma, ambaye kimchezo alikuwa na uelewano mkubwa na Malota, ambaye naye alikuwa anamrahisishia Mogela kupachika mabao hadi akabatizwa jina la ‘Golden Boy’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here