SHARE
Francis Cheka

UKIACHANA na soka, mchezo unaofuata kwa kupendwa nchini na duniani kwa ujumla ni masumbwi, lakini katika siku za karibuni umeanza kupoteza mvuto katika ardhi hii ya Mlima Kilimanjaro.

Wakongwe kama akina Muhammad Ali, Joe Frazier, Mike Tyson, Evender Holyfield pamoja na Lennox Lewis, kwa nyakati tofauti wamewahi kupata umaarufu mkubwa pamoja na kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia mchezo huu unaokubalika sana ulimwenguni.

Mara baada ya kupita kwa zama za wakali hawa, hizi ni zama za wakali wengine kama bondia anayeongoza kwa kumiliki kiasi kikubwa cha fedha Floyd Mayweather ambaye amekuwa katika ubora wake akiweka rekodi ya kucheza mapambano 49, bila ya kupoteza hadi alipotangaza kustaafu karibuni.

Kwa Tanzania, moja kati ya mabondia walioweka heshima kubwa katika mchezo wa ngumi ni bondia Francis Cheka aliyedumu kwa muda mrefu katika tasnia ya masumbwi na kuwa mfano kwa mabondia chipukizi nchini.

Kona ya IT’S SHOW TIME leo imepata nafasi ya kupiga stori na fundi huyu wa ngumi jiwe ambaye wapinzani wake wamekuwa wakipata shida sana kumkalisha kutokana na madai kuwa jamaa ni sugu na hapigiki Knock Out (KO) kizembe.

UMEANZA LINI KUCHEZA MASUMBWI?

Nimeanza kucheza ngumi mwaka 1998 na nimekaa katika mchezo huu kwa zaidi ya miaka 19, hadi sasa mimi bado ni bondia na ninatarajia kupanda ulingoni siku ya mkesha wa sikukuu ya Krismasi kupambana na Dulla Mbabe katika pambano linalodhaminiwa na promota, Kaike Selaju.

KWANINI NGUMI ZIMESHUKA TANZANIA?

Kilichosababisha kushuka anguko la mchezo wa ngumi hapa nchini ni suala la umimi baina ya viongozi wa vyama vya mchezo huu ambao wamekuwa wakijali zaidi masilahi yao na kutuacha mabondia tukiwa hatuna kitu.

Viongozi wa vyama vya ngumi wanapaswa kukaa chini na kuangalia mustakabali wa mchezo huu ambao hivi sasa umepoteza mvuto kabisa, tofauti na miaka ya nyuma ambapo watu walikuwa wakiusapoti sana mchezo huu.

KUFUNGIWA KWA PST KUMEKUATHIRI VIPI?

Moja kati ya mashirikisho yaliyochangia kukua kwa mchezo wa masumbwi nchini ni PST, hivyo kitendo cha kuwafungia si kizuri hata kidogo Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) inapaswa kuangalia uamuzi wao.

Kwa sababu kitendo cha kuifungia PST kimesababisha mabondia wakose mapambano mengi ya nje ya nchi, kwani hadi sasa ni pambano moja pekee la nje limechezwa, jambo ambalo ni tofauti na kipindi shirikisho hilo lilipokuwa likifanya kazi.

UNA NENO LOLOTE KWA WAZIRI NAPE?

Namwomba Waziri Nape Nnauye atusaidie sisi mabondia kututafutia wadhamini wa kuwekeza katika mchezo wa masumbwi ili uweze kurudi katika chati kama zamani, kwa sababu kwetu ngumi ni ajira. Kukosa udhamini ni moja ya sababu kubwa inayozorotesha mchezo hivyo Nape kama Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anapaswa kuingilia kati kunusuru mchezo huu.

NINI UMEJIFUNZA KWA WAKONGWE?

Tanzania imewahi kupata mabondia wenye uwezo mkubwa waliowahi kuiletea sifa, watu kama akina Yomba Yomba, Emanuel Mlundwa, Rashid Matumla na wengine wengi ambao walinifundisha mambo mengi ikiwemo kujiamini na kujitunza kama bondia ili niweze kutimiza ndoto zangu, jambo ambalo limenifikisha hapa nilipo sasa.

NINI SIRI YA KUDUMU KWAKO MCHEZONI?

Siri yangu kubwa ya kudumu mchezoni ni nidhamu yangu ya nje na ndani ya ulingo na kujitunza kwa kupata muda mzuri wa kupumzika na kufanya mazoezi pamoja na kufuata maelekezo ya mwalimu wangu ambaye siku zote amekuwa msaada mkubwa kwangu.

UNA MIKANDA MINGAPI HADI SASA?

Hadi sasa ninashikilia jumla ya mikanda nane tofauti ambayo ni ya TPBO, WBF, IBF, WBC, WBO, UBO, IBO na IFB niliyopata, mara baada ya kuwapiga mabondia wenye sifa na rekodi nzuri ndani na nje ya nchi.

UNAZUNGUMZIAJE TUHUMA ZA UCHAWI?

Mabondia wengi wamekuwa wakitoa lawama kila kukicha kuhusu kukutana na mambo ya kishirikina, siamini kabisa kuhusu suala hili namwamini Mungu ndio sababu ya kufika hapa nilipo na mafanikio niliyoyapata .

MAPAMBANO MATATU AMBAYO HUTAYASAHAU

Nimepanda ulingoni mara nyingi lakini kuna mapambano ambayo siwezi kuyasahau kutokana na upinzani nilioupata, pambano la kwanza lilikuwa dhidi ya Rashidi Matumla mwaka 2009, jingine dhidi ya Mbwana Ally lililokuwa la kuwania ubingwa wa Taifa mwaka 2006 na pambano la tatu ni dhidi ya Japhet Kaseba nililoshinda kwa KO, lakini nilirushwa nje ya ulingo na kupata maumivu ya shingo.

DONDOO TATU USIZOJUA KUHUSU CHEKA

  1. Aliwahi kufanya majaribio ya kucheza soka katika klabu ya Yanga mwaka 1999.
  2. Ni bondia wa kwanza kupewa kiwanja na Serikali kutokana na mchango wake katika mchezo wa masumbwi.
  3. Amepoteza pambano moja pekee nchini, hii ilikuwa dhidi ya Thomas Mashali.

JE, BONDIA GANI ATAFUTA NYAYO ZAKO?

Kuna mabondia watano ambao kama wakilinda viwango vyao na kujitunza vya kutosha wanaweza kufuata nyayo zangu na kuwa tishio kwenye ulimwengu wa masumbwi nchini Tanzania. Mabondia hao ni pamoja na:-

  1. Ethan John
  2. Kudra Tamimu
  3. Twaha Kassim
  4. Cosmas Cheka
  5. Ibra Twasi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here