SHARE

LONDON, England

KAMA kuna kitu kinachowavuruga mashabiki wa Arsenal kwa sasa, basi ni hatima ya kiungo wao, Mesut Ozil, ambaye htama yake bado haijajulikana ndani ya kikosi hicho cha Washika bunduki.

Pia, Ozil na kocha Unai Emery waliingia katika malumbano mwishoni mwa msimu uliopita ambao walimaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Hasira zao zilipanda zaidi baada ya Arsenal kupoteza mchezo wao wa kwanza wa hatua ya 32 bora ya Ligi ya Europa dhidi ya BATE Borisov, mfungaji wa wenyeji akiwa ni Stanislaw Drahun.

Haikuwa matokeo tu, bali Arsenal walicheza hovyo, wakitengeneza nafasi chache za mabao, licha ya kuingia uwanjani wakiwa wamepewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

Kilchowakera zaidi mashabiki ni timu yao kuzidiwa, huku ‘fundi’ Ozil akiwa nje, wakiamini huenda uwepo wake ungekuwa na msaada mkubwa kwa kikosi chao.

Bado haiwaingii akilini kuona Ozil akiwa ameingia mara tano tu kwenye kikosi cha kwanza katika mechi 12 za mwishoni mwa msimu.

Mbaya zaidi kwao ni tetesi zilizopo, kwamba nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani anawindwa vikali na mabosi wa klabu za England, Ufaransa, Ujerumani na China.

Hivi sasa kikosi hicho kipo nchini Marekani kikijiandaa na msimu mpya, licha ya Ozil kuonekana kuwa na furaha, bado mashabiki wamekuwa na wasiwasi juu ya hatma yake. 

Kama akiondoka, mashabiki wanazikumbuka mechi tano alizowahi kuwabeba. Ni mechi gani hizo? 

Arsenal 2-0 Napoli (2013)

Hiyo ilikuwa Oktoba Mosi, ikiwa ni mechi yake ya kwanza kuichezea Arsenal katika mikimiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ozil alikuwa kwenye ubora wake usiku huo, akianza kuitungua Napoli, kabla ya kutengeza jingine katika ushindi wa mabao 2-0 pale Emirates.

Kilichowakosha mashabiki wake ni kwamba ni dakika 15 tu zilizokuwa zimepita tangu alipomfunga kipa Pepe Reina hadi alipotengeza bao la pili.

Arsenal 4-1 Liverpool (2015)

Arsenal waliingia uwanjani wakiwa hawapewi nafasi ya ushindi kwa kuwa mwaka mmoja kabla ya kukutana tena, walishachapwa mabao na Liverpool.

Hata hivyo, Aprili 4, 2015, haikuwa siku nzuri kwa Liverpool, hasa kutokana na kiwango alichokuwa nacho Ozil. Shuti lake la mbali lilimshinda kipa Simon Mignolet na kuifanya Gunners wawe mbele kwa mabao 2-0.

Hadi kumalizika kwa dakika 90 za mtanange huo, Ozil ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo na baadaye bao lakehilo lilitajwa kuwa ndilo bora zaidi kwa Aprili 2015.

Arsenal 2-0 Bayern Munich (2015)

Ilikuwa habari mbaya kwa Arsenal kupangiwa Bayern Munich kwani walishatolewa mara mbili na Wajerumani hao (2013 na 2014).

Hata hivyo, safari hii Bayern walikiona cha moto mbele ya Ozil, akiwatungua dakika ya 94 kwa kutumia krosi ya Hector Bellerin, hivyo Bayern ‘kufa’ 2-0 katika mtanange huo wa makundi, matokeo yaliyowapeleka Arsenal hatua ya 16 bora.

Arsenal 3-0 Chelsea (2016)

Hiyo ilikuwa Septemba 24. Kuelekea mchezo wenyewe, Arsenal hawakuwa wakipewa nafasi ya ushindi. Ni kwa sababu walikuwa wameshinda mechi mbili tu kati ya 13 walizokuwa wamekutana na Blues katika siku za karibuni.

Kama ilivyo kawaida yake, Ozil alikuwa kwenye kiwango chake cha juu, akifunga bao tamu na la mwisho kwa kutumia krosi ya Alexis Sanchez.

Kulipata bao hilo, Ozil ndiye aliyeanzisha mashambulizi katikati ya uwanja, akimzidi kete N’Golo Kante, kabla ya kwenda kuzitikisa nyavu za Chelsea zilizokuwa zikilindwa na Thibaut Courtois.

AC Milan 0-2 Arsenal (2018)

Ulikuwa ni mtanange wa Ligi ya Europa na ulichezwa Machi 8 jijini Milan, Italia. Wengi walitabiri Arsenal ‘kufia’ huko lakini Ozil alikuwa nyuma ya pazia katika ushindi wa mabao 2-0 pale San Siro.

Ndiye aliyetengezea ‘kifundi’ bao la ushindi lililowekwa kimiani na Aaron Ramsey na ilimfanya Ozil kuwa ameshiriki katika upatikanaji wa mabao 100 tangu alipotua Kaskazini mwa London akitokea Hispania alikokuwa akiichezea Real Madrid.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here