Home Makala GADIEL MICHAEL: YANGA WALINIFUATA, NIKAWAZIMIA SIMU

GADIEL MICHAEL: YANGA WALINIFUATA, NIKAWAZIMIA SIMU

515
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

NI ngumu sana kusikia jina lake likitajwa na mashabiki wa soka nchini lakini ukitafuta wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Azam FC msimu huu, huwezi kuacha kulitaja jina lake. Hapa namzungumzia Gadiel Michael M’baga.

Ni nadra sana kwenye mchezo wa soka kusikia mabeki wa pembeni wakipewa sifa na hii ni kutokana na majukumu yao makubwa uwanjani, kuwatuliza mawinga wa pembeni. Soka limewatenga sana watu hawa lakini hakuna wanachojali wameendelea kupiga kazi.

Leo hii kila kinapopangwa kikosi cha Azam huwezi kumkosa Gadiel Michael, mzaliwa wa Tanga, ambaye kwa sasa amekuwa gumzo katika usajili wa msimu ujao.

Mbali na umuhimu wake katika kikosi cha timu hiyo na kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, lakini ni mchezaji aliyepitia maisha magumu huku akisafiri kilomita 346.8 sawa na saa 6:03 kutoka Tanga hadi Dar es Salaam kutafuta timu ya kuendeleza kipaji chake.

Licha ya kuja Dar es Salaam kufikia Ubungo nyumbani kwao, lakini alipitia changamoto nyingi za maisha ikiwamo kukosa chakula kwa siku huku akiwa anafanya mazoezi magumu.

Mbali na changamoto hiyo, beki huyo kabla ya kutua Azam alitokea Villa Squad katika timu ya vijana na hatimaye alijipeleka katika kituo cha Azam kufanya majaribio na hatimaye kupita.

DIMBA limefanya mahojiano ya kina na beki huyo kuhusu safari yake ya soka alipoanzia hadi alipofikia sasa na nini anachokitarajia kwa hapo baadaye.

DIMBA: Unazungumziaje kiwango chako msimu huu?

Gadiel: Msimu huu kwangu nimekuwa bora zaidi kuliko misimu mingine, hii inatokana na kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza.

DIMBA: Unadhani ulikosea wapi msimu uliopita mpaka ikaonekana umeshuka kiwango?

Gadiel: Msimu uliopita si kama msimu huu, hii ilichangiwa na kutopewa nafasi ya kucheza. Kocha aliyekuwapo alishindwa kuniamini kama naweza kupambana.

DIMBA: Azam imeshindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu na hata FA unadhani tatizo kubwa lilikuwa wapi?

Gadiel: Ni kweli hatukufanya vizuri, lakini sababu kubwa iliyochangia ni suala la kubadilisha makocha, ni jambo kubwa ambalo limetuathiri wachezaji, ukizingatia kila kocha anayekuja huwa ana mbinu na falsafa zake hivyo hii ilichukua muda kidogo kuzoea mbinu.

DIMBA: Malengo yako miaka mitano ijayo katika soka?

Gadiel: Kucheza soka la kulipwa nje, ninaimani nitafanikiwa kwani hapa nilipo ni rahisi kwangu kufikia malengo yangu, kutokana na fursa iliyopo Azam.

DIMBA: Vipi kuhusu mkataba wako na Azam FC?

Gadiel: Mkataba wangu unamalizika Septemba mwaka huu.

DIMBA: Je, Yanga wamekufuata na kuhitaji saini yako kwa msimu ujao?

Gadiel: Hakuna kiongozi wa Yanga aliyenifuata ila baada ya kumalizika kwa  mechi yetu na Yanga, kuna watu wa Yanga walinifuata na kuhitaji namba yangu ya simu, wakinieleza wametumwa na Katibu wao Charles Boniface Mkwasa, niliwakatalia kwa kuwa mazungumzo yoyote ya kimkataba lazima yamhusishe meneja wangu na si mimi moja kwa moja.

DIMBA: Je, ulikuwa ukiifahamu Yanga kabla ya Azam?

Gadiel: Nilikuwa nikiisika tu ila sikuwa naifahamu, nilipokuja Dar es Salaam sehemu yangu ya kwanza kufanya mazoezi na Villa Squad ilikuwa Uwanja wa Kaunda, Jangwani. Hivyo, siku tunafanya mazoezi Yanga nao walikuja hapo ndipo nikauliza na kuambiwa kwamba ni Yanga.

DIMBA: Vipi kuhusu thamani yako kwa timu inayokuhitaji?

Gadiel: Siwezi kuzungumzia suala hilo, kwani niko chini ya msimamizi, yoyote anayenihitaji anakutana na meneja wangu na kuzungumza naye.

DIMBA: Kwa makocha waliokufundisha, je, kocha gani ni chachu ya mafanikio yako?

Gadiel: Joseph Omog ambaye kwa sasa yuko Simba, kwa mara ya kwanza alipokuja Azam 2012/13 alitaka kuona timu ya vijana, mimi nilikuwa chaguo lake la kwanza kwa wachezaji aliowapandisha timu mwaka huu, aliniamini na kucheza kikosi cha kwanza na kufanikiwa kupata ubingwa.

DIMBA: Usingekuwa mchezaji unadhani ungekuwa nani?

Gadiel: Ningemfuata baba yangu, ningekuwa dereva wa magari makubwa ambayo yanasafiri nje ya nchi, kwani nilipomaliza shule na kuja Dar na kufeli katika soka baba aliniambia ningeshindwa soka, basi niende anifundishe gari.

DIMBA: Je, soka ilikuwa ndoto yako, timu gani ulipendelea kucheza?

Gadiel: Soka ilikuwa ndoto zangu, Azam ni timu iliyokuwa katika ndoto hizo kwani nakumbuka nilipokuwa kidato cha tatu tuliangalia Azam TV kipindi hicho ilikuwa ikirusha habari za timu ya Azam FC, nikamuahidi mama yangu Rose kwamba, ipo siku nitacheza katika timu hii.

DIMBA: Kupatikana nafasi ya kukaa kambini Azam ilikuwa ngumu wewe uliwezaje kupata nafasi hiyo?

Gadiel: Pasi yangu ya mwisho  ilisababisha tupate ushindi wa bao 1-0 na timu mmoja ya mtaani, hii ilikuwa tiketi yangu ya kupata nafasi ya kuishi hapa.

DIMBA: Ni jambo gani hutakuja kulisahau?

Gadiel: Nilipoambiwa nimepata nafasi ya kuishi hapa nililia sana nikiamini kwamba nitapata sehemu ambayo nitakula na kulala vizuri, pia taarifa hizo zilipomfikia mama yangu alilia sana na ndipo alipotoa baraka za mimi kucheza soka.

DIMBA: Vipi kuhusu sapoti ya wazazi katika soka?

Gadiel: Katika hilo sikuwa na sapoti yoyote, kwani mama yangu hakutaka kusikia nacheza mpira hivyo ubishi wangu na huruma za walimu wangu wa shule kumuomba mama aniruhusu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here