Home Michezo Kimataifa GAIZKA MENDIETA ‘FUNDI’ WA SOKA ALIYEGEUKIA U-DJ

GAIZKA MENDIETA ‘FUNDI’ WA SOKA ALIYEGEUKIA U-DJ

550
0
SHARE

NA NIHZRATH NTANI JNR


NI  nyakati za usiku mwingi. Pembezoni mwa pwani ya Mediterrania, katika mji wa Middlesbrough nchini England, ndani ya moja ya klabu maarufu iliyopo katika eneo hilo.

Watu ni wengi sana usiku huu mahali hapo. Akina kaka na akinadada wanacheza muziki kwa madaha. Watu wanaburudika kweli kweli. Ni kama  wapo katika dunia isiyo na shida.

Mbele ya steji katika ukumbi huo, mwanaume mmoja anaonekana akichezea vyombo vya muziki kwa ustadi mkubwa. Anatikisa kichwa kwa madaha huku akifuatilia mapigo ya muziki huo. Masikio yake yamezibwa na ‘headphone’. Bila shaka huyu ni ‘DJ’ usiku huu.

Ni nani mtu huyu? Najiuliza. Kisha naanza kurejelea kumbukumbu zangu. Naam! Miaka 42 iliyopita mwanamume huyu alizaliwa kule katika jiji la Bilbao ndani ya Jimbo la Basque, nchini Hispania. Historia yake imejaa mizaha mingi. Mizaha yenye kuchekesha.

Akiwa angali kijana mdogo, ndoto ya mtu huyu ilikuwa kuja kuwa mwanariadha maarufu duniani ama DJ siku moja. Akiwa na miaka 14 tu, mwanamume huyu aliacha kucheza soka na kujiingiza katika mchezo wa riadha ili kutimiza ndoto hiyo.

Uamuzi wake wa kuacha soka uliwasononesha sana wazazi wake, lakini hawakuwa na budi kumuunga mkono mtoto wao kwa uamuzi wake huo. Lakini alipofikisha miaka 16, mwanamume huyu ambaye ni DJ usiku huu aliamua kuacha mchezo wa riadha na kujiunga tena na soka.

Ni uamuzi huu uliokuja kumpa umaarufu duniani kote miaka michache baadaye. Mtu huyu anaitwa Gaizka Mendieta.

Majina mengi yamepita klabuni Valencia, lakini ndani ya mioyo ya mashabiki wa klabu hiyo katu hawawezi kumsahau fundi huyu wa Kihispaniola. Mendieta anabakia kuwa mfalme pale Mestalla.

Unaikumbuka Valencia yenye watu kama Santiago Canizares, Kily Gonzalez, Claudio Lopez, Ruben Baraja, David Albelda, Jocelyn Angloma, Amedeo Carbon, Pablo Aimar, Zahovic na wengine wengi kikiwa chini ya kocha Hector Cuper? Bila shaka nimekukumbusha mbali sana.

Kikosi hicho kiliongozwa na nahodha Gaizka Mendieta. Akiwa na uwezo wa kucheza namba yoyote katika dimba la kati, alisaidia sana kuifikisha Valencia katika fainali mbili mfululizo za Mabingwa wa Ulaya.

Walifanya hivyo katika msimu wa 1999/2000 na 2000/2001, fainali zote hizo walipoteza dhidi ya Real Madrid, kisha walikuja kupoteza dhidi ya Bayern Munich katika matuta.

Umahiri wa Gaizka Mendieta ulikuwa ukishangaza wengi. Alikuwa fundi kweli kweli wa mpira. Kwa wakati huu naburudika kumtazama Luca Modric ama Andres Iniesta. Lakini miaka 15 iliyopita burudani ya Modric na Iniesta tulikuwa tunapata kutoka kwa Gaizka Mendieta.

Uwezo wa kupiga pasi zenye macho, kusaidia kukaba, ubunifu, uwezo wa kupiga mashuti nje ya 18, lilikuwa jambo la kawaida kwa Mendieta. Haikuwa ajabu kupitia umahiri wake, Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA), kumtangaza kuwa kiungo bora barani Ulaya kwa miaka miwili mfululizo.

Akiwa Valencia alitwaa mataji mbali mbali, likiwamo taji la Copa Del Rey. Ilipofika Julai 1, 2001, Mendieta alifanya uamuzi aliokuja kuujutia baadaye, pale alipohama Valencia na kwenda Lazio ya Italia, kisha kuwa miongoni mwa wachezaji ghali zaidi duniani kwa wakati huo.

Uamuzi huo ulikuwa kama kujimaliza mwenyewe, huku akitupilia mbali ofa kutoka Real Madrid na Barcelona. Alipowasili Lazio alikutana na viungo wawili waliojenga himaya yao klabuni hapo. Uwepo wa viungo hawa, Paved Nedved na Juan Sebastian Veron, ikawa ngumu kupenya katikati yao.

Alitumia miaka mitatu klabuni hapo huku muda mwingi akiwekwa benchi na ilipofika mnamo mwaka 2004, Mendieta alikubali kwenda Barcelona kwa mkopo.

Hata uko nako hakuweza kuteka mioyo ya mashabiki wa klabu hiyo. Msimu mmoja baadaye alielekea nchini England kunako klabu ya Middlesbrough.

Alitumia misimu minne klabuni hapo, huku akiwa sehemu ya timu iliyoweka rekodi ya kutwaa taji la ligi kwa mara ya kwanza katika historia ya Middlesbrough.

Ilipofika Mei 13,2008, Mendieta alitangaza kujiuzulu baada ya kukumbwa na majeraha yasiyokwisha na kupelekea kushuka kwa kiwango chake na kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.

Baada ya kustaafu, Mendieta aliamua kuishi nchini England katika mitaa ya ‘Yarm’ ndani ya mji wa Middlesbrough.

Kwa sasa Mendieta anajihusisha na uchambuzi wa soka kupitia kituo cha Sky Sports cha Uingereza, akichambua mechi za La Liga.

Pia akitumia muda wake wa ziada kufanya kazi ya U-DJ katika kumbi mbalimbali, ikiwa moja ya kazi alizozipenda tangu utotoni, na ndiyo  ndoto yake iliyotimia baada ya kustaafu soka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here