SHARE

LIBREVILLE, Gabon

KAMA ulifikiri michezo ya jana ndio imesisimua zaidi nchini Gabon, basi ni bora ukatulia na kufikiri upya, kazi ndio kwanza imeanza.

Usiku wa leo robo fainali mbili zitapigwa kwa timu 4 bora kwenye hatua ya makundi kukutana uwanjani na kutafuta timu mbili za kufuzu hatua ya nusu fainali, Afcon 2017.

Hapa tumekuandalia tathmini fupi ya michezo yote ya leo na ni timu zipi zinapewa nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya nusu fainali.

DR Congo vs Ghana

Wapi na lini?

Ngoma itapigwa leo katika dimba la Free State. Kwa Ghana hii inaweza kuwa bahati kwao kucheza katika uwanja mzuri baada ya kulalamika ubovu wa viwanja walivyotumia kwenye michezo ya makundi.

Tathmini ya timu zote mbili

Leo tutazishuhudia timu bora kabisa kwenye hatua ya makundi zikipambana kwenye robo fainali.

Japo wengi hawakutarajia makubwa kwa DR Congo, lakini ushindi wao dhidi ya Ivory Coast na Togo ulitosha kuonyesha wana usongo kiasi gani na kombe la Afcon.

Wamefunga mabao ya kutosha, ni imara pia kwenye safu yao ya ulinzi na wamekuwa kivutio kwa mashabiki kwa soka lao wanalocheza.

Ghana bado hawajafika katika kilele cha ubora uliokuwa ukitegemewa na wengi. Nguvu yao bado inaonekana ipo kwenye dakika 45, wakikukosa hapo ni rahisi kwao kupoteza mchezo.

Pigo kubwa kwao kwenye mchezo huu ni Asamoh Gyan. Bado hali yake ya majeruhi imewanyima uhakika kuwa watamtumia au la na hata kama wakimtumia ubora wake hautakuwa sawa kama alivyozoeleka na wengi.

Wakuchungwa

Junior Kabananga ndiye kinara wa mabao mpaka sasa na ndiye mchezaji hatari katika kikosi cha Congo. Mchezaji pekee anayekaribiana naye kwa ubora katika michuano hii ni winga wa Ghana, Christian Atsu, mchezaji bora wa Afcon 2015.

Utabiri: Ghana watafuzu kwa penalti

Kwa kuwa watacheza kwenye kiwanja kizuri, ni wazi kuwa Ghana watafunguka na kuonyesha soka safi kama ilivyo Congo. Tutarajie mchezo mzuri na wa kusisimua!

 

Misri vs Morocco

Lini na wapi?

Mchezo wa mwisho wa robo fainali Afcon 2017 utapigwa kwenye jiji la Port Gentil, usiku wa leo.

Tathmini ya timu zote mbili

Misri walimaliza vinara wa kundi D baada ya kuichapa Ghana bao 1-0 kwenye mchezo wa mwisho, lakini bado wanaonekana kukosa muunganiko mzuri katika kikosi chao.

Labda ni kwa sababu ya uwanja, lakini bado nyota wa taifa hilo, Mohamed Salah, hajawa kwenye ubora wake licha ya kuwa na asisti moja na bao moja mpaka sasa.

Morocco walipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Congo, lakini waligeuka na kushinda michezo yao iliyofuatia.

Herve Renard, kocha mwenye rekodi ya kutisha katika bara la Afrika, atakuwa na kazi kubwa ya kuisuka timu yake ili iweze kupata ushindi dhidi ya ‘Mafarao’ ambao hawajafungwa bao lolote mpaka sasa.

Wakuchungwa

Salah ndiye nyota wa Misri, sambamba na kiungo anayekipiga katika klabu ya Arsenal, Mohamed Elneny. Hata hivyo, beki yao inayoongozwa na Ali Gabr na Ahmed Hegazy, wamekuwa imara mpaka sasa wakimlinda vyema mlinda mlango mkongwe, Essam El-Hadary.

Morocco wao wanacheza kitimu na hawategemei mchezaji mmoja, lakini nyota  kama Mbark Boussoufa na Rachid Alioui wameonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga na kuitikisa safu ya walinzi wa timu pinzani.

Utabiri: Misri atasonga mbele kwa ushindi wa dakika 30 za nyongeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here