SHARE

LONDON, England

NYOTA wa zamani wa Arsenal Mbrazil, Gilberto Silva, amewatupia lawama wachezaji wa timu hiyo kuwa wanamsaliti kocha Arsene Wenger.

Gilberto aliyatoa haya kuhu Arsenal wakichezea kichapo cha mabao 3-1 mbele ya West Brom, mchezo uliopigwa kwenye dimba la The Hawthorns, lenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 26,000.

Mabao ya West Brom kwenye pambano hilo yaliwekwa kimiani na Robson-Kanu na Dawson aliyefunga mara mbili kwenye dakika ya 12 na 75.

Bao pekee la Arsenal lilifungwa na Alexis Sanchez ambaye alitolewa uwanjani dakika ya 78 na nafasi yake kuchukuliwa na Alex Iwobi.

“Wachezaji wanatakiwa kujituma zaidi,” alisema Gilberto, kiungo aliyeiongoza Arsenal kubeba taji la Premier League bila kufungwa katika msimu wa 2003-04.

“Wakati mwingine ukiitazama Arsenal kwa makini, unagundua kuwa hakuwa wanachokosa, nafikiri wachezaji wanatakiwa kujituma zaidi na kupambana ikiwa bado wanapenda kuendelea kubaki na Wenger.

“Washikamane na warudi kwenye mstari ili kuzima presha zote zinazotoka kwa mashabiki hivi sasa, naamini matokeo mabovu si mzigo wa kocha pekee,” aliongeza Mbrazil huyo.

Kwenye mchezo wa jana, mashabiki wa Arsenal waliingia uwanjani na mabango yalioutaka uongozi kutompa Wenger mkataba mpya.

Ikumbukwe mkataba wa kocha huyo raia wa Ufaransa na Arsenal unamalizika mwishoni mwa msimu na mwenyewe aligoma kuongeza kipindi hiki akihitaji muda kwanza wa kuweka sawa hali ya kikosi chake.

Lakini uongozi wa Arsenal ulivunja ukimya siku za hivi karibuni ukiomba mashabiki watulie, wakidai kuwa wako kwenye mazungumzo na Wenger ili kujua hatima ya klabu hiyo.

Miongoni mwa makocha waliotajwa kurithi mikoba ya Wenger ikitokea hajaongezwa mkataba mpya, ni Massimiliano Allegri wa Juventus na Ronald Koeman wa klabu ya Everton.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here