Home Habari GORAN AKUBALI KUMRITHI OMOG

GORAN AKUBALI KUMRITHI OMOG

1570
0
SHARE

NA SAADA SALIM

UNAWEZA usiamini, lakini ndio ukweli. Kocha, ambaye viongozi wa Simba waliwahi kushindwana naye mwaka juzi, Mserbia Goran Kopunovic, ametamka kwamba; “Naweza kuja Dar es Salaam dakika yoyote na kuifundisha Simba kama tutakubaliana.”

Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika, aliwahi kuinoa Simba mwishoni mwa msimu wa 2014/2015 na baadaye kuondoka baada ya kushindwa kukubaliana na uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi.

Lakini sasa Kopunovic amewaita mezani viongozi wa Simba kwa ajili ya kufanya nao mazungumzo na kama watakubaliana anaweza kurejea wakati wowote ili kurithi mikoba ya Joseph Omog, ambaye inadaiwa kuwa siku zake zinahesabika.

Wakati akitua Simba, Mserbia huyo alirithi mikoba ya Mfaransa Patrick Liewig, aliyetimuliwa baada ya kikosi cha timu hiyo kutofanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Kwa hivi sasa uongozi wa Simba unadaiwa kumpa mechi tano kocha wa sasa Mcameroon, Omog, kubadili mwenendo wa matokeo ya timu na kuhakikisha timu inapata ushindi na kucheza mpira unaovutia.

Simba ilianza vizuri mechi yake ya kwanza ya ligi kwa kuibamiza Ruvu Shooting mabao 7-0, lakini ikasimamishwa na Azam Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, jijini Dar es Salaam, katika mechi ya pili na kulazimishwa suluhu ya bila bao, huku safu yake ya ushambuliaji ikionekana kuwa butu.

Kitendo cha timu hiyo kulazimishwa suluhu, kimeufanya uongozi wa Simba, chini ya Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kumtaka Omog ahakikishe timu yake inashinda mechi nne zijazo, ikiwamo dhidi ya Mwadui FC, inayopigwa leo Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Mechi nyingine zijazo ni dhidi ya Mbao FC ambapo Simba watakuwa wageni katika mchezo huo, utakaopigwa Mwanza, dhidi ya Stand United, utakaochezwa Shinyanga na Mtibwa Sugar utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Taarifa za uhakika zilizoifikia DIMBA kutoka kwa kigogo wa Simba, zinadai kwamba, Kamati ya Utendaji ya Simba ilikutana hivi karibuni na kujadiliana mwenendo wa timu yao na kutoa maelekezo kwa benchi la ufundi linaloongozwa na Omog kuhakikisha wanashinda mechi tano, ingawa walianza na suluhu dhidi ya Azam FC.

Kigogo huyo ameliambia DIMBA kuwa, timu yao hiyo iliambulia pointi moja katika mchezo huo na sasa wanaendelea na hesabu yao, huku mechi dhidi ya Mwadui ikiwa ni mchezo wa pili kati ya michezo mitano ambayo alipewa Omog kuhakikisha wanashinda.

Miongoni mwa makocha wanaotajwa kurejea nchini baada ya uongozi wa Simba kumpa masharti Omog ni Goran Kopunovic, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari.

Hiyo inafuatia baada ya shabiki kipenzi na mwanachama wa Simba, Mohammed Dewji (MO), kuwapa jeuri kwamba yupo tayari kumlipa kocha mwenye kuiletea mataji klabu hiyo.

DIMBA jana lilifanikiwa kuzungumza na Goran kwa simu akiwa kwao Serbia, ambapo alisema yupo tayari kurejea kufundisha Simba endapo uongozi wa timu hiyo utamfuata na kuhitaji huduma yake.

Alisema kwa sasa yupo nchini kwao amepumzika na kuna baadhi ya ofa anazisikilizia, hivyo yupo tayari kuinoa timu hiyo, kwani aliondoka Simba kutokana na kushindwa kulipwa kiasi alichokihitaji.

“Sina tatizo na Simba, niko tayari kuja kuifundisha kwa mara nyingine, hivyo suala la maslahi siyo kubwa sana, kikubwa kama wanahitaji waje tuzungumze na kufikia mwafaka,” alisema Goran.

Mserbia huyo alisema kuondoka kwa klabu hiyo si kwa ubaya wala kutupiwa virago, bali ni baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika na Simba kushindwa kumpa fedha anayohitaji, akaamua kuondoka.

Wakati wa utawala wa Kopunovic, Simba ilifanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar kwa kuifunga Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalti, lakini pia ikamaliza ikiwa ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara nyuma ya Azam, ambao walikuwa nafasi ya pili na Yanga waliokuwa mabingwa wa msimu wa 2014-2015.

Kocha huyo alitimka zake Mtaa wa Msimbazi baada ya kushindwa kufikia makubaliano na klabu hiyo kwenye masuala ya mkwanja wa ada ya usajili wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here