SHARE

CATALONIA, Hispania

TAYARI, Antoine Griezmann ni mali ya Barcelona baada ya dili la Mfaransa huyo lililokua likiendeshwa kwa siri kubwa kukamilika juzi, Ijumaa kwa kitita cha euro milioni 120.

Hata hivyo, Atletico hawajataka kunyamaza kimya baada ya kumpoteza mchezaji wao huyo bora ndani ya misimu mitano iliyopita, ambaye alikaribia kutua Camp Nou majira yaliyopita ya kiangazi.

Atletico wamekasirishwa kwa kiasi kikubwa na uhamisho huo, wakidai kuwa wanatakiwa kulipwa kiasi kingine cha fedha, euro milioni 80, kutokana na kitendo cha Barca kufanya mazungumzo na Griezmann mwezi Machi.

Sababu ya kutaka fedha hiyo ni hii; wakati Barca inazungumza na Griezmann mwezi huo, kipengele cha kuvunja mkataba wa straika huyo kilikuwa ni euro milioni 200 kabla ya kushuka hadi 120.

Kinachosubiriwa ni kama Atletico watafanikiwa kuilazimu Barca izime mzozo huo kwa kukubali kulipa euro milioni 80 zinazotakiwa, lakini hilo sio swali pekee linalohitaji majibu.

Nafasi ipi atatumika Griezmann?

Barca itauanza msimu ujao na safu ya washambuliaji watatu itakayoongozwa na Lionel Messi na Luis Suarez hivyo Griezmann anatakiwa kujua ni wapi atakapofiti vyema.

Griezmann ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi yoyote katika safu ya ushambuliaji, anaweza kusimama na Suarez huku Messi akiwa nyuma yao, au winga ya kushoto, Suarez katikati na Messi akisimama kulia.

Barca inapitia kipindi kigumu cha kushindwa kufanya vyema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu miwili iliyopita, hivyo wanategemea Griezmann ataongeza kasi ya ziada kwenye kikosi chao.

Pia, Griezmann ni mmoja wa washambuliaji wapambanaji mno, kama alivyo Suarez. Hiyo inatokana na historia yake tangu akiwa Atletico chini ya kocha Diego Simeone.

Hivyo, Barca wamempata mchezaji atakayesaidia kila upande na kuwapa ahueni Messi na Suarez. Lakini, haijajulikana iwapo atafiti kikamilifu ndani ya kikosi cha kwanza.

Neymar anafuata?

Huenda Griezmann akawa ndiye mchezaji ghali zaidi kununuliwa na Barca, lakini mabingwa hao wa La Liga wana matumaini pia ya kumchukua Neymar kutoka PSG.

Hata hivyo, licha ya Neymar kuwa tayari kurejea Camp Nou kuungana na marafiki zake, Messi na Suarez, dili hilo lina asilimia chache za kukamilika.

Kwanini? PSG hawaoneshi kuwa tayari kumuuza Neymar kwa bei chee, na ili Barca waweze kumrudisha supastaa wao huyo wa zamani, watalazimika kuwauza nyota wao kadhaa katika majira haya ya kiangazi.

Au, kama PSG wataweza kuwachukua nyota wa Barca kama biashara ya mabadilishano, kwa mfano Philippe Coutinho, Ivan Rakitic na Samuel Umtiti, hapo watakuwa tayari kumwachia Neymar aondoke zake.

Hatma ya Coutinho ipo shakani mno pale Nou Camp. Staa huyo wa zamani wa Liverpool hakuweza kufanya vizuri msimu uliopita kama ilivyotegemewa na wengi.

Hakuwa mchezaji wa kutisha sana alipokuwa akipangwa kama winga wa kushoto, nafasi ambayo kwa sasa ni ya Griezmann na Neymar (iwapo atasajiliwa), na tayari amewekwa sokoni.

Katika hali ambayo huenda wengi wakashangazwa nayo, Ousmane Dembele naye huenda akauzwa.

Winga huyo wa Kifaransa mwenye kasi na hatari anapolikaribia lango la wapinzani, hakuweza kuonesha makali yake ipasavyo kutokana na majeraha yaliyomsumbua kwa kipindi cha miaka miwili.

Barca inaonekana wazi kushindwa kumvumilia Dembele, na wanataka kumtumia kama chambo ya kumrudisha Neymar nyumbani.

Licha ya rais wa klabu ya Barca, Josep Maria Bartomeu, hivi karibuni kudai kwamba Dembele ni mchezaji mzuri kuliko Neymar, lakini inasubiriwa kuonekana kama kauli hiyo ilimaanisha hakuna biashara itakayofanyika kwa wachezaji hao au la.

Suarez atauzwa?

Dembele anaweza akauzwa au Neymar akarejeshwa nyumbani, lakini ujio wa Griezmann unadhihirisha wazi kuwa Suarez hatakuwa na uhakika wa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Barca tangu atue hapo mwaka 2014.

Ni ngumu kwa kocha anayeamini kuchezesha washambuliaji wawili kama Valverde kudhubutu muundo wa mastraika watatu, yaani Messi, Suarez, Griezmann aidha na Neymar au Dembele.

Jibu pekee hapa ni kwamba kutakuwa na mzunguko wa wachezaji kubadilishana mechi, lakini kwa kipindi kirefu sasa, chumba cha kubadilishia nguo cha Nou Camp kimekuwa na sauti za watu wawili tu; Messi na Suarez.
Haitakuwa rahisi kwa Suarez kukubali kushuka chini na hivyo Griezmann atalazimika kuwa mpole kwake.

Itakumbukwa kuwa Griezmann aliwahi kudai kuwa anaipenda tamaduni ya watu wa Uruguay ambako ni nyumbani kwa Suarez, bila ya kuwa na uhusiano wowote na taifa hilo, kauli ambayo Suarez aliiponda.

Hata hivyo, Barca wamefanya biashara nzuri ya kuongeza nguvu mpya hasa ikizingatiwa kwamba Messi na Suarez wote wana umri wa miaka 32.
Lakini, itakuwa ni kazi ngumu kwa mastaa hao kuelewana chini ya Valverde, hasa katika wakati huu ambao Suarez hana mpango wa kuondoka Barca.

Wahispania wanautaka ufalme wao Ulaya?

Uhamisho wa Griezmann, sambamba na ule wa Eden Hazard kwenda Real Madrid na Atletico kumnasa Joao Felix, umeifanya Hispania kuwa na wachezaji 10 bora ambao wamesahjiliwa na klabu zao mwezi huu.

Inasubiriwa pia kama Neymar atarudi Barca na Paul Pogba kusajiliwa na Real Madrid.

Ni kama vile klabu hizo zimepania kufanya kweli kwenye michuano ya UEFA na Europa msimu ujao baada ya kushuhudiwa zile za Ligi Kuu England zikitikisa msimu uliopita.

Hata hivyo, vita ya kwanza itakuwa ni ya kwao wenyewe katika taji la La Liga. Mbona moto utawaka aisee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here