SHARE

MANCHESTER, England

HIVI karibuni zilisambaa tetesi kwamba Pep Guardiola alikuwa mbioni kutua Juventus ambao wameachana na Massimiliano Allegri, zilizoamsha fununu kwamba Mhispania huyo anawakimbia mabingwa hao wa England baada ya kushindwa kuwapa taji la UEFA.

Hata hivyo, tetesi hizo zimezimwa tena na Guardiola mwenyewe, ambaye aliibuka na kusema kwamba anachoamini Manchester City ni sehemu safi ya kufanya kazi, na amewathibitishia mashabiki kuwa ataendelea kuwa Etihad angalau kwa misimu miwili ijayo.

Hadi kufikia sasa, Guardiola amefanikiwa kutwaa mataji mawili mfululizo ya EPL na pia amenyakua mengine ya FA na Carabao msimu uliopita.

Mkataba wa kocha huyo na Man City unatarajiwa kufikia tamati Juni mwaka 2021, baada ya kuongeza muda wa kuendelea kukinoa kikosi hicho majira yaliyopita ya kiangazi.

“England ndio sehemu nzuri mno duniani, kucheza soka na kufanya kazi yako ya ukocha,” alisema Guardiola.

“Ni sawa na Hispania na Ujerumani. Binafsi sijawahi kwenda mataifa mengine, huenda Italia kukawa kama Hispania. Hapa sijawahi kusikia mashabiki wakikuzomea kama timu haishindi, najiona kama ni shabiki wa Manchester City.

“Nakumbuka mwaka wangu wa kwanza hapa ulikuwa mgumu mno. Tulipoteza mechi dhidi ya Monaco kwenye Ligi ya Mabingwa na hatukuwa vizuri sana EPL, lakini bado watu walikuwa nyuma yetu ‘kutusapoti’.

“Hapa kila kitu kinaenda vizuri katika mazingira yote, kushinda au kushindwa. Sitasahau ushirikiano tulioupata kutoka kwa mashabiki baada ya msimu wangu wa kwanza kumalizika bila taji.

“Kuna utulivu wa hali ya juu ndani ya Man City. Ni klabu nzuri sana kwa ajili ya kazi. Sijajua kwingineko kupo vipi, lakini naiona klabu hii ikiwa vizuri. Nipo tayari kudumu hapa kwa misimu miwili zaidi,” alisema.

Kocha huyo ameonesha dhamira hiyo ya kubaki Manchester akiwa ameipa klabu ya Man City mataji matano ndani ya misimu mitatu, lakini kitu kimoja tu ambacho wengi wanatamani akifanye ni kushinda taji la UEFA.

Tangu atue Etihad, Guardiola hajaweza kuvuka hatua ya robo fainali katika michuano hiyo, msimu uliopita walikutana na kizuizi cha Tottenham, na Liverpool waliwang’oa katika hatua hiyo msimu mmoja kabla.

Katika msimu wa kwanza, Monaco ndio waliowatoa jasho Man City, lakini ilikuwa kwenye hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Guardiola alidai kuwa ana uhakika vijana wake watafanya kazi nzuri zaidi na kufika mbali katika michuano hiyo.

“Ninachoamini, mchezo wa soka una nafasi zaidi ya moja. Nitapata nafasi nyingine kama nilivyoweza kushinda EPL ambayo wengi walidhani sitaweza, sasa wanataka nishinde na taji la UEFA. Nipo tayari,” alisema.

Aidha, kocha huyo aliongeza: “Kama si msimu ujao, basi nitajaribu msimu unaofuata, kama nitashindwa tena, nitarudi msimu unaofuata.”

“Yawezekana Man City ikawa bingwa wa Ulaya nikiwepo, au nisipokuwepo hapa. Pengine na wachezaji hawa wa sasa au watakaokuja baadaye, muhimu ni kwamba tunapambana na tunaamini ipo siku tutashinda,” alisema Guardiola.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here