Home Makala Guardiola mwenye tabia za Liewig kwa akina Sunzu

Guardiola mwenye tabia za Liewig kwa akina Sunzu

341
0
SHARE
Pep Guardiola

NA EZEKIEL TENDWA,

MWAKA 2013 mashabiki wa Klabu ya Simba walishikwa na butwaa baada ya aliyekuwa Kocha wao Mkuu Mfaransa, Patrick Liewig, kuwatimua baadhi ya wachezaji waliokuwa nyota, wakati huo timu ikiwa kwenye harakati za kuusaka ubingwa.

Ukiachana na hao waliotimuliwa, walikuwepo wengine wa kikosi cha kwanza ambao walisimamishwa kwa muda, huku kocha huyo akiwaamini zaidi wachezaji chipukizi.

Wachezaji ambao kocha huyo ambaye kwa sasa anaifundisha Stand United hakutaka kabisa kuwaona kwenye kikosi chake walikuwa ni Haruna Moshi ‘Boban’, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Juma Nyosso, Amir Maftah, Paul Ngalema, Abdallah Juma pamoja na mshambuliaji kutoka Ghana, Komabil Keita.

Wale ambao kocha huyo aliwasimamisha kwa muda ni aliyekuwa mshambuliaji wao mahiri kutoka nchini Zambia, Felix Sunzu, pamoja na kiungo mkongwe Mwinyi Kazimoto, ambaye kati ya hao ndiye pekee ambaye yupo kwa Wekundu hao wa Msimbazi mpaka sasa.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Sunzu na Mwinyi iliwabidi kusubiri huruma za mashabiki wao ambao waliuangukia uongozi na kocha huyo ili kuwarudisha, lakini hata hivyo Sunzu hakukaa muda mrefu na badala yake aliamua kutimka zake.

Liewig hakufanya usajili wa maana kuziba nafasi za wachezaji hao, wakiongozwa na Boban na badala yake aliwaamini vijana waliokuwa kikosi cha pil, wakiwamo akina Ramadhan Singano, Said Ndemla, Jonas Mkude na wengine.

Ilikuwa ni presha kubwa kwa idadi kubwa ya mashabiki, lakini hawakuwa na la kufanya, kwani hayo yalikuwa maamuzi ya kocha ambaye hata hivyo naye alijikuta akiondolewa mchana kweupe, ndipo ile methali ya dawa ya moto ni moto ilipotimia.

Kama mashabiki wa Simba walivyopatwa na mshtuko kipindi hicho cha Liewig, pale nchini England mashabiki wa Manchester City hawajaamini kilichofanywa na Kocha Pep Guardiola cha kuwatema baadhi ya wachezaji wake muhimu, huku akishindwa kumjumuisha Yaya Toure katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ni kweli kwamba kocha ana maamuzi yake ambayo lazima yaheshimiwe, lakini mengine yanawaumiza mashabiki na ndiyo maana Guardiola alipoonyesha dalili za kutokuwa na imani na kipa kipenzi cha wengi, Joe Hart, mashabiki walibaki vinywa wazi.

Yaya Toure, yule ambaye Manchester City isingeweza kucheza vizuri kama hakuwepo ndiye ambaye leo hii anaonekana hana msaada wowote kwa kocha huyo. Hiyo ni muendelezo wa yale aliyomfanyia pale Nou Camp walipokuwa pamoja katika kikosi cha Barcelona.

Guardiola ana jeuri baada ya kuwasajili Claudio Bravo, John Stones, Ilkay Gundogan, Leroy Sane na Nolito, lakini kitendo cha kumuona Toure na Joe Hart kama takataka kinawauma mashabiki, lakini hawana cha kufanya.

Kitakachoweza kumbeba Guardiola katika Klabu hiyo ni kufanya vizuri na wachezaji wake hao ambao anawaamini, vinginevyo anaweza akaondoka kwa aibu na mashabiki wa kikosi hicho kumuweka kwenye kumbukumbu zao za kuwaharibia timu.

Guardiola alifanya vizuri alipokuwa Bayern Munich ya Ujerumani, lakini wapo baadhi ya wachezaji ambao hawatamsahau, kwani nusura aue viwango vyao, akiwamo Frank Ribery na mkongwe Arjen Robben ambao kwa sasa wana furaha mbele ya kocha wao mpya, Carlo Ancelotti.

Ni kweli kwamba uongozi wa Manchester City una imani kubwa sana na kocha huyo kutokana na uwezo wake kwenye timu alizopitia, lakini ameshaanza kutengeneza maadui, kwani familia ya Toure na Joe Hart na mashabiki wao hawana furaha kabisa.

Kitakachombeba kocha huyo ni kufanya vizuri mbele ya makocha wenzake wakubwa kama Jose Mourinho wa Manchester United, Arsene Wenger wa Arsenal,  Antonio Conte wa Chelsea, Jurgen Klop wa Liverpool, vinginevyo itakuwa shida kwake.

Guardiola ni kocha mzuri, kwani kila mmoja ameona soka lililokuwa likichezwa na Barcelona na Bayern Munich, lakini tusisahau jambo hili. Katika Ligi ya Hispania ni Barcelona na Real Madrid na kwa mbali Atletico Madrid ndio wana hati miliki na ubingwa, sawa na Ujerumani Bayern Munich.

Kwa Ligi ambayo yupo sasa zipo zaidi ya timu saba ambazo kila moja inao uwezo wa kutwaa ubingwa. Sasa kazi kwake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here