Home Michezo Kimataifa GUNDU LA 16 BORA Litawaandama Arsenal au litawaacha?

GUNDU LA 16 BORA Litawaandama Arsenal au litawaacha?

612
0
SHARE

LONDON, England

DALILI zinaonesha kwamba klabu ya Arsenal itamaliza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa nafasi kwenye kundi A, baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na PSG katika mchezo uliopigwa mapema wiki hii kwenye dimba la Emirates.

Baada ya matokeo hayo, Arsenal wanaitegemea sana Ludogorets iisimamishe PSG mwezi ujao katika mchezo wa mwisho wa kundi lao. Ni lazima wawe na mategemeo hayo, kwani mabingwa hao wa Ufaransa wana rekodi nzuri ya matokeo ya nyumbani na ugenini.

Kwa jinsi msimamo wa kundi lao ulivyo, kuna uwezekano mkubwa wa Arsenal kukutana na Barcelona, Atletico Madrid au Monaco. Wapinzani wengine wanaotegemewa ni Real Madrid au Borussia Dortmund, Juventus au Sevilla, Napoli na Benfica au Besiktas.

Iwapo kutatokea mtikisiko kidogo na Arsenal wakamaliza katika nafasi ya kwanza, basi wapinzani wao kwenye hatua ya 16 bora huenda wakawa ni Bayern Munich, Leverkusen au Porto.

Historia inasema, kwa kipindi cha misimu sita iliyopita Arsenal wameshindwa kuvuka hatua ya 16 bora baada ya kukutana na timu ngumu, hiyo ikichangiwa mno na wao kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi, mechi zenyewe ni hizi hapa:

2011 (Barcelona 4-3 Arsenal)

Kipindi cha kwanza Arsenal walijikuta wakiwa nyuma kwa bao moja lililofungwa na mshambuliaji David Villa, lakini walirudi vizuri kipindi cha pili na kupata ushindi wa mabao 2-1, baada ya Robin van Persie na Andrey Arshavin kutumbukiza mipira ndani ya nyavu za dimba la Emirates katika dakika 12 za mwisho za mchezo huo.

Mchezo wa marudiano pale Camp Nou, Barca ilibadili matokeo na kushinda kwa mabao 3-1, ingawa walisaidiwa sana na kadi nyekundu aliyooneshwa RVP. Hadi filimbi ya mwisho inapulizwa, Barca ikasonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3.

2012 (AC Milan 4-3 Arsenal)

San Siro. Milan. Ndani ya uwanja huo, ndani ya jiji hilo, ndipo mwisho wa Arsenal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ulipoandikishwa rasmi mwaka huo.

Robinho (mabao mawili), Zlatan Ibrahimovic na Kevin-Prince Boateng waliisaidia AC Milan kuinyuka Arsenal mabao 4-0 yaliyokata maini ya washika bunduki kutinga hatua ya robo fainali baada ya dakika 90 za kwanza tu.

Arsenal huwa ni timu tofauti linapokuja suala la kubadili matokeo mechi ya marudiano, pale Emirates walijaribu kufanya hivyo.

Walikula ng’ombe mzima wakashindwa kumalizia mkia pale Emirates. Mabao matatu ya Laurent Koscielny, Tomas Rosicky na Van Persie yaliwapa mashabiki imani ya kugeuza matokeo, lakini bahati haikuwa kwao na wakatolewa kwa jumla ya mabao 4-3.

2013 (Bayern 3-3 Arsenal)

Ilikuwa ni wiki mbaya sana kwa Arsenal, kwani walijikuta wakisukumwa nje UEFA, ikiwa ni siku chache tu tangu walipotolewa na Blackburn Rovers kwenye Kombe la FA.

Baada ya kuchapwa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza na Bayern Munich ya kocha Jupp Heykens pale Emirates, Arsenal ilikuwa na nafasi nyingine ya kugeuza matokeo na kusonga mbele lakini hawakuweza kufanya hivyo baada ya kufunga mabao mawili tu kupitia kwa Olivier Giroud na Koscielny, hivyo Bayern ikafanikiwa kusonga mbele kwa sheria ya mabao ya ugenini.

2014 (Bayern 3-1 Arsenal)

Kwa msimu wa pili mfululizo, Bayern (chini ya Pep Guardiola) walipangiwa kukabiliana na Arsenal na wakaifanya timu hiyo kama ngazi ya wao kusonga mbele kufuatia ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza pale London.

Arsenal sasa wakawa na jukumu zito la kugeuza matokeo kule Ujerumani, lakini bao la kiungo Bastian Schweinsteiger likasababisha maisha kuwa magumu zaidi kwa ‘Gunners’. Mshambuliaji Lukas Podolski akaifungia Arsenal bao moja, lakini halikutosha kuiokoa timu yake hiyo na janga la kuyaaga mashindano.

2015 (Arsenal 3-3 AS Monaco)

Mchezo wa kwanza baina ya timu hizi ulikuwa na matokeo ya kushitukiza ambapo Arsenal ilikubali kichapo cha mabao 3-1 nyumbani kwao licha ya kuonekana kama ni mechi nyepesi kwao.

Walipoenda jijini Monaco, presha sasa ikawa juu ya wenyeji kuzuia mashambulizi ya vijana wa Wenger na kwenye historia ya michuano hiyo, hakuna timu iliyoweza kufunga mabao matatu ugenini na kugeuza matokeo kama Arsenal ilivyotakiwa kufanya kwenye mchezo huo. Angalau ilitaka kujaribu kuandika historia mpya.

Olivier Giroud akapachika bao kipindi cha kwanza, Aaron Ramsey akafunga lingine zikiwa zimesalia dakika 11 mchezo umalizike. Wenyeji wakapata moto kwenye matumbo yao lakini walishukuru Mungu mwishoni baada ya Arsenal kushindwa kuongeza bao lingine na ikaondolewa rasmi mashindanoni kwa sheria ya bao la ugenini.

2016 (Barcelona 5-1 Arsenal)

Arsenal waliwakaribisha wababe wa Catalonia kwenye Uwanja wa Emirates ambapo ndani ya dakika 70 walicheza soka safi na mara kadhaa walijaribu kutafuta mabao lakini Messi akawakata maini kwa mabao yake mawili.

Baada ya mtanange huo kumalizika na Barca kuondoka na ushindi wa mabao 2-0, Arsenal sasa walibaki na jukumu moja tu la kuzuia maangamizi zaidi kutoka kwa safu kali ya ushambuliaji ya MSN.

Mmoja wa washambuliaji hao, Neymar, alianza kuifungia Barca bao la kwanza kabla ya kiungo Mohamed Elneny kusawazisha bao hilo kwa shuti kali na hapo kila shabiki wa Arsenal aliomba Barca isiendelee kufunga ili waongeze mengine mawili na kusonga mbele.

Lakini ule msemo wa kisicho riziki hakiliki ukadhihirika Nou Camp kwa straika Luis Suarez kupachika bao safi la pili kwa njia ya ‘tik tak’ na Messi akaongeza lingine na kufanya mchezo umalizike kwa Barca kusonga mbele na ushindi mnono wa jumla ya mabao 5-1.

Wakati tukisubiri hatua ya makundi kumalizika, tuendelee kujiuliza pia kama gundu hili la kuishia hatua ya 16 bora litaendelea kuwaandama Arsenal au litawaacha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here