SHARE

MANCHESTER, England

MIPANGO inayofanyika huko Manchester City mbona mtatubu bila kutaka. Imeripotiwa kuwa kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola, anataka kuongeza nguvu kwa kusajili angalau wachezaji wanne mara tu dirisha kubwa la usajili litakapofunguliwa.

Guardiola yupo tayari kuwasulubu tena wapinzani wake msimu ujao wa Ligi Kuu England 2019/2020, kwa kushusha wachezaji wa nguvu katika kikosi chake kilichosheheni nyota ‘kibao’, usajili ambao utaigharimu Man City zaidi ya pauni milioni 200.

Mhispania huyo kwa sasa anaendelea kusherehekea ubingwa wa pili mfululizo wa Ligi Kuu England, alioutwaa wikiendi iliyopita baada ya kuishushia kisago Brighton cha mabao 4-1 na kuwapiku wapinzani wake wa karibu, Liverpool.

Hata hivyo, licha ya kwamba Guardiola na timu yake hiyo wapo mbioni kubeba taji la tatu msimu huu, wakisubiri kucheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Watford wikiendi hii, kocha huyo ameshaanza kujipanga kwa ajili ya msimu ujao.

Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail, kocha huyo wa zamani wa Barcelona anataka kuona mabosi wake wakimshushia beki mmoja, viungo wawili na mpachika mabao.

Kwa sasa Man City inakabiliwa na hatari ya kuwa na upungufu wa mabeki msimu ujao, zaidi ikiwa ni nahodha wa timu hiyo, Vincent Kompany, kuliweka pembeni suala la kutia saini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Etihad.

Aidha, mabingwa hao wa England, huenda wakaondokewa na ‘vitasa’ Nicolas Otamendi na Eliaquim Mangala, hivyo ni wazi kuwa jambo la kwanza muhimu kama si la pili kichwani mwa Guardiola ni kusajili beki wa kati.

Mmoja wa mabeki wanaosakwa na Guardiola ni Harry Maguire, anayeichezea timu ya Leicester City, ingawa Mwingereza huyo amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na Man United.

Lakini, kama Man City watamkosa Maguire, wataelekeza nguvu yao kwa nahodha kinda wa timu ya Ajax, Matthijs de Ligt, ambaye anatajwa kwenye tetesi zinazosambaa kuwa yuko mbioni kutua Barcelona.

Beki mwingine anayefuatiliwa na Guardiola ni Ben Chilwell, ambaye anacheza timu moja na Maguire, Leicester City. Lakini, inaaminika kuwa ameachana na mlinzi huyo wa kushoto ili asajili beki wa kati.

Eneo lingine linalotarajiwa kuongezwa nguvu ni kwenye kiungo, ikikumbukwa kuwa kabla ya kuanza kwa msimu huu, Guardiola alihitaji kupata mrithi wa Mbrazil, Fernandinho, ambaye umri wake umemtupa mkono.

Baada ya kukosa mmoja kati ya nyota aliowahitaji, akiwamo Jorginho, ambaye alimfuata Maurizio Sarri Chelsea, Guardiola aliamua kujitoa mhanga na kumtumia Fernandinho msimu huu, ingawa alishuhudia jinsi gani majeraha yalivyomsumbua mkongwe huyo.

Kutokana na hitaji lake kubwa la kumpata mrithi wa Fernandinho, huenda Guardiola akatumia kila njia kumsajili kiungo wa Atletico Madrid na timu ya Taifa ya Hispania, Rodri Hernandez.

Imeelezwa kuwa Guardiola anamtazama kiungo huyo mahiri anayesifika kwa umakini wake na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za uhakika, kama mrithi wa muda mrefu wa Fernandinho, ambaye amemsaidia kunyakua mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu England.

Kiungo mwingine anayetolewa macho na Man City ni Houssem Aouar wa Lyon, na nyota huyo mbunifu zaidi katika kikosi cha vigogo hao wa Ufaransa anatarajiwa kutua haraka zaidi iwapo Ilkay Gundogan ataondoka Etihad.

Kwa upande wa wapachika mabao, jina la straika wa Frankfurt, Luka Jovic, ni moja kati ya wanaosakwa, huku kinda hatari wa Benfica, Joao Felix, naye akiwamo kwenye orodha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here