SHARE

NA JESSCA NANGAWE

KIKOSI cha Singida United huenda kisiwe kwenye orodha mpya ya timu zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao kutokana na kuwa kwenye nafasi hatarishi ya kuteremka daraja.

Licha ya ligi hiyo kuisimama kwa sasa kufuatia tamko la serikali la ligi kuisitisha kwa siku 30 kutokana na wimbi la virusi vya Corona kutapakaa duniani kote, lakini ni dhahiri tayari kikosi hicho kipo kwenye nafasi kubwa ya kutoa mkono wa kwa heri msimu huu.

Kwa sasa timu hiyo mkia chini ya kocha Ramadhan Nsanzurwimo tayari imecheza jumla ya michezo 29 na kuambulia pointi 15 tu, kiasi cha viongozi wake kuanza kukata tamaa na sasa wanasubiri miujiza kuibakisha timu yao kwenye ligi hiyo yenye ushindani.

Mikosi ilipoanzia

Ilianza ligi ikiwa na kocha Fred Felix Minziro ambaye alipokea mikobatoka kwa Hans Pluijim, kikosi hicho hakikuwa na maisha mazuri katika ligi kikajikuta kinapokea vichapo mfululizo iwe ugenini ama kwenye uwanja wao wa Namfua.

Uongozi wakiri

Mkurugenzi wa klabu hiyo Festo Sanga alikiri kikosi chake kutokuwa katika nafasi nzuri ya kujitetea kubaki msimu ujao, hiyo inatokana na nafasi waliyopo, wanachosubiri kwa sasa ni muujiza tu katika soka ambayo inawezekana.

“Tulitumia nguvu nyingi kupanda daraja na tukafanikiwa kwa hiyo ikitokea tutashuka pia tutatumia nguvu kupanda kwa mara nyingine, lakini tunachoamoni pamoja na nafasi tuliyopo soka linamiujiza yake”anasema Sanga.

SIASA

Zipo sababu zinazotajwa kuchangia kikosi hicho kuporomoka na kushindwa kufanya vyema msimu huu lakini kubwa zaidi ni kuingizwa siasa pamoja na ukata kama sehemu ya sababu zilizochangia kutofanya vizuri.

Siasa imekuwa moja ya sababu kubwa inayotajwa kuwa chanzo cha timu hiyo kupoteza mwelekeo huku baadhi ya viongozi wa juu wakitupiwa lawama kwa kuendesha timu hiyo kisiasa zaidi ikiwemo suala zima la kuchagua wachezaji wanaowataka.

Timu hiyo ambayo inalelewa na baadhi ya viongozi wa serikali inadaiwa kuwa haifanyi vizuri na makocha wake kushindwa kudumu hasa kutokana na kupangiwa majukumu pamoja na kikosi.

UKATA/WADHAMINI KUJITOA

Kwa siku za hivi karibuni Singida United imeonekana kukumbwa na ukata hasa baada ya baadhi ya wadhamini kujiondoa hali inayofanya timu ishindwe kupata matokeo mazuri inapokua kwenye uwanja wake au ugenini.

Baadhi ya wachezaji wamekuwa wakilalamika kutopata mishahara yao kwa wakati na hata mlo wao kutozingatiwa pamoja na stahiki mbalimbali wanazodai, kushindwa kulipwa hali iliyowashusha wachezaji, ari ya kushindana uwanjani.

Minziro afunguka

“Nimeondoka Singida United baada ya wachezaji na uongozi mzima kukosa ushirikiano na mimi hali iliyochangia timu kutopata matokeo mazuri kwa muda wote niliokuwa nao pale”ilisema sehemu ya taarifa ya kocha huyo ambaye kwa sasa ametuwa ndani ya kikosi cha Alliance.

Minziro aliipandisha timu hiyo msimu wa 2016/17 toka daraja la kwanza na alienguliwa na nafasi yake kupewa Mholanzi Hans Van Pluijm kabla ya kurejea kwa mara nyingine na kisha kuondoka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here