SHARE

LONDON, England

HAKUNA kulala. Mambo yanazidi kunoga nchini England, wikiendi iliyopita tulishuhudia michezo ya Ligi Kuu iliyokuwa na ushindani mkubwa lakini jana na leo mechi za Kombe la Carabao zilichukua nafasi.

Hata hivyo, hisia za mashabiki wengi wa soka nchini England wataelekeza macho yao katika viwanja viwili vya Anfield na Stamford Bridge ambavyo vitakuwa na michezo mikubwa.

Leo, ndani ya Uwanja wa Anfield, Liverpool watakuwa wenyeji wa Arsenal huku Chelsea wakiikaribisha Manchester United kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Liverpool inayonolewa na Jurgen Klopp ambaye ni raia wa Ujerumani mara ya mwisho walifungwa mabao 2-1 na Wolverhampton katika michezo ya ndani ya England. Yaani Ligi Kuu, FA na Carabao.

Tangu hapo, imekuwa timu imara zaidi ambayo imecheza michezo zaidi ya 15 bila kufungwa katika Uwanja wa Anfield. Lakini kuelekea mchezo wao dhidi ya Arsenal, kuna uwezekano mkubwa wakakosa huduma ya beki wao kisiki, Virgil van Dijk ambaye alipata maumivu ya mguu dhidi ya Tottenham.

Pia, Joel Matip naye anatarajiwa kuwa nje kutokana na kusumbuliwa na majerha ya enka yaliyompelekea kukosa michezo miwili iliyopita dhidi ya Genk na Tottenham.

Kukosekana kwa mabeki hao, kutamfanya Klopp kuwapa nafasi akina Joe Gomez na Dejan Lovren ambao wamekosa namba za kudumu tangu kuanza kwa msimu huu ndani ya kikosi cha Liverpool.

Hata katika eneo la ushambuliaji, Mohamed Salah ahatajumuishwa kwenye mchezo wa leo sababu ya majeraha ya enka aliyopata dhidi ya Tottenham.

Arsenal ambao walitoka sare ya mabao 2-2 mechi iliyopita ya Ligi Kuu dhidi ya Crystal Palace, wataingia Anfield kwa lengo la kulipa kisasi dhidi ya Liverpool ambao waliwachapa mabao 3-1 mapema msimu huu.

Taarifa kutoka Arsenal zinasema kocha wa timu hiyo, Unai Emery amepanga kumwacha nahodha wake Granit Xhaka baada ya kuonyesha nidhamu mbovu dhidi ya mashabiki wikiendi iliyopita.

Pia, kumekuwa na taarifa za kiungo mshambuliaji wa Arsenal, Mesut Ozil kupewa nafasi ya kucheza leo baada ya kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza.

Liverpool XI: Adrian; Hoever, Lovren, Gomez, Milner; Oxlade-Chamberlain, Henderson, Keita; Lallana, Brewster, Origi

Arsenal XI: Martinez; Bellerin, Holding, Mustafi, Kolasinac; Torreira, Willock; Maitland-Niles, Ozil, Saka; Martinelli.

Upande mwingine, Manchester United wataingia Stamford Bridge wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Chelsea, msimu uliopita katika Kombe la FA.

Pia, wakali hao wa Ole Gunnar Solskjaer watakuwa na kumbukumbu nzuri ya kuichapa Chelsea kwa mabao 4-0 katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu England msimu huu.

Lakini kiwango ambacho kimekuwa kikionyeshwa na Chelsea mpaka sasa kinampa kiburi kocha wao Frank Lampard kwa kuamini wanayo nafasi ya kulipiza kisasi kwa Manchester United.

Lampard ameiongoza Chelsea kushinda michezo saba mfululizo katika michuano yote msimu huu, huku wakifunga mabao zaidi ya moja kwenye mechi hizo walizocheza.

Naye Solskjaer alikishuhudia kikosi chake kikivunja mwiko wa kutokushinda ugenini kwa miezi saba, baada ya kuifumua Norwich City kwa mabao 3-1.

Chelsea XI: Caballero, James, Zouma, Tomori, Alonso, Barkley, Gilmour, Pedro, Hudson-Odoi, Batshuayi, Giroud.

Man United XI: Romero, Wan-Bissaka, Maguire, Rojo, Williams, McTominay, Pereira, Fred, Lingard, James, Rashford.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here