Home Habari HAPPY NEW YEAR SIMBA

HAPPY NEW YEAR SIMBA

697
0
SHARE
NA MARTIN MAZUGWA, MTWARA

NI wazi kwamba Simba watakuwa wameuanza mwaka 2018, wakiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Ndanda FC, mchezo uliochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Shujaa wa mchezo huo ni nahodha wa Simba, John Bocco, ambaye alifunga mabao yote mawili na kuifanya klabu yake hiyo kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, wakifikisha pointi 26.

Ushindi wa Simba jana una maana kubwa kwani walikuwa wameshushwa kileleni na Azam FC, baada ya Wanalambalamba hao kushinda mabao 3-0 dhidi ya Stand United, lakini sasa Bocco, amewarejesha kwenye nafasi yao.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa huku Ndanda FC, wakionekana kuwamudu Simba dakika 45 za kipindi cha kwanza kutokana na kujiamini.

Kipindi cha pili ndicho kilicholeta maumivu kwa Ndanda FC, kutokana na kandanda la kuvutia lilioonyeshwa na Simba ambalo liliwafanya Wekundu hao kupata mabao hayo yote mawili, yaliyowarejesha kileleni.

Bocco alianza kupeleka furaha kwa mashabiki wa Simba katika dakika ya 52, akifunga bao safi kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na winga machachari, Shiza Kichuya, kutoka upande wa kulia.

Ndanda walipambana ili kulirejesha bao hilo lakini walijikuta wakiruhusu jingine katika dakika ya 56, kupitia kwa Bocco huyo huyo, ambaye alimalizia kwa shuti hafifu, mpira uliokuwa ukizagaa eneo la kipa, baada ya Moses Kitandu kuwahadaa mabeki wa wapinzani wao hao kwa kuupisha mpira ambao ulimkuta mfungaji.

Kipindi hicho cha pili ambacho Simba walionekana wazi kupania kuibuka na ushindi, nusura waongeze bao la tatu, dakika ya 59, baada ya Said Ndemla kuachia shuti kali, ambalo lilitoka sentimita chache langoni mwa wapinzani wao.

Kwa upande wa Ndanda walishindwa kutumia nafasi muhimu katika kipindi cha kwanza kupitia kwa John Tiba pamoja na John Masawe ambao hawakuwa makini katika kumalizia, huku kipa Aishi Manula, akifanya kazi kubwa kuchomoa michomo kadhaa.

Matokeo hayo yanadhihirisha wazi kwamba Ndanda FC ni wateja wa Simba kwani tangu wapande Ligi Kuu hawajawahi kuonja ushindi mbele ya Simba kwani wamekutana michezo saba, Wanakuchele hao wakifungwa yote nao wakiambulia kufunga bao moja tu.

Kwa matokeo hayo, leo mashabiki waSimba watakuwa wakila kuku kwa mjira wakisubiri kuukaribisha mwaka mpya, huku wakiiombea mabaya Yanga ipoteze mchezo wao dhidi ya Mbao FC, utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Kikosi cha Simba kilikua hivi; Aishi Manula, Paul Bukaba, Shiza Kichuya, Jjuuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, John Bocco, James Kotei, Juma Luizio/Moses Kitandu, Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim/Said Ndemla.

Kikosi cha Ndanda kilikua hivi: Jeremiah Kisubi, Willium Elias,Abdalah Seleman, Ibrahim Job, Hamad Wazir, Hemed Khoja, Jacob Massawe, Majid Bakar, John George, Jabir Aziz na Mrisho Ngassa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here