Home Habari HASIRA ZA YANGA HAIJAWAHI TOKEA

HASIRA ZA YANGA HAIJAWAHI TOKEA

850
0
SHARE

*Yawashukia Zimamoto na hasira zote


NA SAADA SALIM

MZUKA wa Yanga katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, haijawahi tokea. Wanajangwani hao mwaka huu wameamua kushiriki michuano hiyo inayoendelea kutimua vumbi kisiwani Zanzibar, huku wakiwa na hasira kali zaidi kutokana na ukweli kwamba hawajalitia taji hilo mikononi kwa kipindi cha miaka 10 sasa.

Kwa mara ya kwanza na ya mwisho, Yanga ililitwaa taji hilo mwaka 2007, ilipoizidi kete Mtibwa Sugar ya Morogoro ambayo walikipiga nayo katika mechi ya fainali.

Baada ya kuanza michuano hiyo kwa kishindo juzi kwa kuipasua Jamhuri ya Pemba kwa mabao 6-0, Yanga leo tena inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Amaan, kukipiga na Zimamoto katika mechi ya mzunguko wa pili kundi B.

Kikosi cha Wanajangwani hao kitashuka dimbani leo huku kikiwa na kiu ya kutaka kuendeleza vipigo kwa kila mpinzani watakayecheza naye wakiwamo Zimamoto, ambao ndio Mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, ameliambia DIMBA Jumatano kuwa kikosi chao kipo vizuri kwa ajili ya mchezo wa leo ambao wana uhakika wa kushinda.

Alisema hawatapuuzia timu yoyote watakayokutana nayo na watahakikisha wanafanya vizuri katika kila mechi na ikiwezekana waweze kutwaa taji la ubingwa wa michuano hiyo.

“Kikosi kipo vizuri, ushindi tulioupata katika mechi yetu na Jamhuri hautatufanya tubweteke kwani tunahitaji kufanya vizuri ili kujenga kikosi imara kutokana na kukabiliwa na michuano ya kimataifa hivi karibuni,” alisema.

Mwambusi alisema wako makini na timu wanazokutana nazo wakiamini kwamba ni michuano ambayo inawapa mwanga wa kuona mapungufu katika kikosi cha timu hiyo.

Wachezaji ambao huenda wakapangwa katika kikosi cha leo ni; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondan, Vincent Andrew ‘Dante’, Said Makapu, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima na Emmanuel Martin.

Hata hivyo, Yanga inashuka dimbani huku ikimkosa kiungo wake ‘Mkata umeme’, Justine Zulu ambaye ni majeruhi.

Kiungo huyo alishindwa kumaliza dakika 90 katika mchezo uliopita baada ya kugongana na mchezaji wa Jamhuri, hali iliyosababisha ashonwe nyuzi tano katika paji la uso.

Daktari wa timu hiyo, Edward Samweli, alithibitisha kutokuwepo kwa Zulu katika mchezo wa leo.

“Zulu ameumia katika mchezo wa juzi dhidi ya Jamhuri hivyo ameshonwa nyuzi tano, kwa hali hiyo tumempa mapumziko mafupi kwa ajili ya matibabu chini ya uangalizi wa daktari,” alisema.

Alisema baada ya matibabu hayo anaendelea vizuri lakini kama jopo la daktari wameamua kumpa mapumziko mafupi hadi hapo atakapokuwa vizuri.

Daktari huyo alisema kiungo huyo anatarajia kuonekana katika mchezo wao wa mzunguko wa tatu dhidi ya Azam FC utakaopigwa Jumamosi.

Ukiachana na mechi hiyo, mechi nyingine ambayo itapigwa leo ni kati ya Azam na Jamhuri, itakayopigwa saa 10:00 jioni kwenye uwanja huo huo wa Amaan.

Ikumbukwe Wanalambalamba hao pia walianza vyema katika mchezo wao wa awali dhidi ya Zimamoto kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, ambapo tayari jana waliendelea na maandalizi yao kwa  kuimarisha zaidi kikosi cha timu yao.

Azam inayonolewa na Iddy Nassor ‘Cheche’, alisema baada ya mchezo wao wa juzi, jana waliendelea na mazoezi mepesi kwa ajili ya kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo.

“Asubuhi ya leo (jana) tumefanya mazoezi, kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza na kikosi kipo vizuri matarajio yetu ni kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mchezo wetu wa pili,” alisema kocha huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here