Home Michezo Kimataifa HATA UWACHUKIE… HAO NDIO GOLDEN STATE WARRIORS

HATA UWACHUKIE… HAO NDIO GOLDEN STATE WARRIORS

7985
0
SHARE

OHIO, Marekani            |       


HAKUNA nyota wa Golden State Warriors ambaye angeweza kuvumilia nguvu ya damu inayochemka mwilini kwa furaha, walipolipuka kwa shangwe baada ya kutangaza ubingwa wa NBA kwa mara nyingine mwaka huu mbele ya Cleveland Cavaliers.

Warriors waliitandika Cavaliers kwa pointi 108-85 katika mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia jana, ambao ulidhihirisha kuwa mabingwa hao hawana mpinzani kwa sasa katika Ligi Kuu hiyo ya kikapu nchini Marekani.

Vinara hao walinyakua ubingwa wao huo baada ya kuvishinda vikwazo vyote msimu huu, kikiwemo cha kuibuka na ushindi mbele ya Houston Rockets kwenye fainali za NBA Kanda ya Magharibi kabla ya kuwavaa Cavaliers.

Ushindi huo uliwaweka Warriors kwenye kundi la timu kali za NBA zilizowahi kunyakua ubingwa mfululizo katika kipindi cha miaka minne tu.

Ni timu za Boston Celtics, LA Lakers na Chicago Bulls, zilizowahi kuwa na kiwango cha hali ya juu katika NBA kama inavyofanya Warriors kwa sasa.

Aidha, rekodi hiyo ya Warriors ya kutwaa mataji matatu ndani ya miaka minne na mawili mfululizo, ni ya kwanza katika fainali za NBA tangu 2007, ambapo timu ya San Antonio Spurs ilifanya maajabu.

Stephen Curry na Kevin Durant, walikuwa ni mwiba mchungu kwa Cavaliers kwa mara nyingine na Durant alitangazwa tena kuwa MVP wa ligi hiyo.

Mara baada ya mtanange huo, Durant alikuwa na haya ya kusema: “Hii ndiyo timu bora, kama mlikuwa mnasikia, leo mmejionea.”

“Tumekuwa tukishambuliwa kila kona, wapinzani wetu NBA, makocha tofauti, mashabiki, vyombo vya habari lakini tunafurahi kwani ndio kwanza tunazidi kuimarika,” alisema Durant.

Naye Curry, alisema: “Hakika zilikuwa ni mechi ngumu sana kwetu, tulijua wazi kuwa kazi isingekuwa nyepesi kama mwaka jana.”

Staa wa Cavaliers, LeBron James, alisema katika mechi tatu zilizopita kati ya saba za fainali hizo, alicheza huku mkono wake ukiwa umevunjika.

Alisema sababu ya kuvunjika kwa mkono huo ni kuzidiwa na hisia katika mchezo wa kwanza dhidi ya Warriors na kusababisha ajiumize mkono wake huo wa kulia.

James alifunga pointi 23 kwenye mchezo huo wa juzi usiku na kumaliza fainali hizo akiwa na wastani wa kufunga pointi 34, kucheza mipira iliyorudi ‘rebounds’ 8.5 na asisti 10.

“Mechi ya kwanza nilizidiwa na hisia. Ni kawaida kama ukikosa fursa za kuisaidia timu yako ipasavyo kwenye mechi ya kwanza hasa unapokutana na timu kama Golden State na niliruhusu hisia zinitawale,” alisema James.

“Mechi tatu zote za mwisho nilicheza nikiwa na maumivu ya mkono. Ndio hivyo,” aliongeza staa huyo ambaye anatajwa kuwa huenda akaondoka Cavaliers.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here