Home Makala HATA ZIDANE AKITUA MANCHESTER UNITED MAMBO YANAWEZA YAKAWA YALEYALE

HATA ZIDANE AKITUA MANCHESTER UNITED MAMBO YANAWEZA YAKAWA YALEYALE

6878
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA


JUMAPILI ya Septemba 2, mwaka huu, katika Uwanja wa Turf Moor, tulimshuhudia Jose Mourinho akionekana kupagawa kwa furaha baada ya straika wake mahiri, Romelu Lukaku, kuifungia Manchester United bao la pili na la ushindi dhidi ya Burnley.
Bao la kwanza lililofungwa na Mbelgiji huyo, lilimfanya Mourinho kufurahi, lakini si sana, ila alipoona bao la pili akaamini kwamba mchezo utamalizika kwa ushindi, ndiyo maana alinyanyuka na kurusha mikono kana kwamba anatupa kitu fulani.
Ilikuwa lazima Mourinho afurahi kwa sababu alitoka kupoteza michezo miwili mfululizo, akianza kufungwa mabao 3-2 na Brighton, kabla ya kukubali kichapo kingine cha mabao 3-0 kutoka kwa Tottenham, Uwanja wa Old Trafford.
United ya Mourinho, iliianza Ligi vizuri, ikipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Leicester City, lakini wakajikuta wakipoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya Brighton na Tottenham kabla ya kufufukia kwa Burnley, wakishinda mabao 2-0.
Mourinho aliingia katika mchezo huo akijua kwamba matokeo yoyote mabaya yangemuweka kwenye wakati mgumu zaidi, ndiyo maana alifurahia ushindi huo, akiamini atatuliza kelele zilizokuwa zikipigwa.
Mourinho alikuwa anajua kwamba huku nje tayari zipo tetesi kwamba Zinedine Zidane anasubiri kwa hamu kubwa nafasi yake kama ataendelea kuboronga.
Hakuna kocha mwingine ambaye anatajwa sana kuchukua nafasi ya Mourinho kama Zidane. Mafanikio yake aliyoyapata akiwa na kikosi cha Real Madrid, ambacho kilitwaa ubingwa wa UEFA mara tatu mfululizo chini yake yanamfanya kupigiwa debe na baadhi ya watu kutua Old Trafford.
Wakati Zidane akitajwa kwamba huenda akaenda Manchester United, mwenyewe ametoa kauli kwamba atarejea uwanjani kufundisha soka muda mfupi ujao, hali ambayo inamfanya Jose Mourinho kuwa tumbo joto.
Hata hivyo, kuna mgawanyiko ambao unaleta maswali ndani ya kikosi hicho cha United, kwani wapo ambao wanaamini matokeo mabaya anayoyapata Mourinho yanachangiwa na Ed Woodward, huku wengine wakimuona kocha huyo ameishiwa mbinu.
Ed Woodward anaweza akawa chanzo cha yote hayo, kwani Mourinho alimuomba fedha za usajili ili asajili wachezaji anaoamini yeye kwamba baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya pili, msimu huu wangemsaidia kutwaa ubingwa.
Baadhi ya wachezaji ambao Mourinho aliwataka sana ni beki wa kati, Harry Maguire, wa Leicester City, winga wa Inter Milan, Ivan Parisic pamoja na Antoine Griezmann wa Atletico Madrid, lakini hakupata hata mmoja.
Kama Ed Woodward anamtakia mema Mourinho, angemtimizia mahitaji yake yote ili apate njia ya kumtumbua kama angeshindwa kufanya vizuri, lakini kwa sasa anaonekana kuchangia matatizo yaliyopo.
Ni kweli kwamba Mourinho amekuwa na uhusiano mbaya na baadhi ya wachezaji sio kwa United peke yake, kwani hata Chelsea na Real Madrid, ilikuwa hivyo, lakini bado kuna swali la kujiuliza.
Swali lenyewe ni kwamba baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson, alikuja David Moyes, na baadaye Louis Van Gaal, ambao hawakuwa na uhusiano mbaya na wachezaji lakini hakuna cha maana sana walichokifanya mpaka wakafurushwa.
Moyes na Van Gaal, walikuwa na uhusiano mzuri sana na wachezaji wa United lakini walishindwa kupata mafanikio aliyoyapata Mourinho mpaka sasa hivyo labda kuna kitu kingine cha ziada cha kuangaliwa katika kikosi hicho kuliko kukimbilia kufukuzana.
Hata huyo Zidane, ambaye anatajwa kuitaka nafasi ya Mourinho, anaweza akayakuta mazingira magumu naye akatimuliwa kama akina Ed Woodward, wataendelea kuwepo na kukataa kutoa fedha za usajili kama alivyomfanyia Mourinho.
United ni timu kubwa sana. Uongozi hautakiwi kukurupuka na kumtimua Mourinho na badala yake wampe nafasi nyingine. Wanatakiwa kumtimizia mahitaji yake, kwani aliikuta timu haijiwezi, lakini amewapa ubingwa wa Europa na pia kumaliza nafasi ya pili, sasa amekosa nini? Bado tunasubiri kitakachotokea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here