Home Chombezo HATUA ZA KUZINGATIA UNAPOSAKA MCHUMBA

HATUA ZA KUZINGATIA UNAPOSAKA MCHUMBA

589
0
SHARE

NA JOSEPH SHALUWA,

MAPENZI ni sawa na mchezo wa karata tatu, hata hivyo, kama ukiwa
makini, hakika mapenzi hayawezi kuwa karata tatu kwako. Tumeshuhudia
mara nyingi mtu akiamua kukatisha uhai wake baada ya kuachwa na mpenzi
wake, unajua kwanini?

Kwa sababu hakuwa amejiandaa juu ya tukio hilo, amelipokea kwa ukubwa
na anajinyima haki yake ambayo ni ya kimsingi ya kuendelea na maisha
kama kawaida.

Mambo huwa mrama, baada ya kugundua mpenzi uliye naye hakupendi,
hakufikirii na wala hajakupa nafasi katika moyo wake, lakini kumbuka
kitu kimoja, mambo haya hutokea ikiwa hukujipanga tangu mwanzo kabla
ya kumkaribisha katika moyo wako.

Hatua zifuatazo ni muhimu mno kwako kuzizingatia kabla ya kuingia
katika uhusiano na mpenzi mpya ambaye mategemeo ya baadaye ni kuishi
naye katika ndoa takatifu.

TAZAMA MAISHA YAKO YAJAYO

Katika mahusiano ni vizuri ukaanza kwanza kujipa nafasi ya kwanza
kabla ya kumpatia huyo ambaye unatarajia awe mwandani wako wa maisha
yako yote!

Kosa kubwa linalofanywa na vijana wengi kabla ya kuingia katika
mahusiano ya kimapenzi na mpenzi mpya ni pamoja na kuweka maisha ya
kimapenzi katika wingi.

Ninaposema wingi ninamaanisha kuwa, unachanganya maisha ya mpenzi
wako aliyepita, huyo mpya na maisha yako kama mamoja, jambo ambalo
kisaikolojia na mpangilio mzima wa maisha yako yajayo sio zuri. Jiweke
namba moja, halafu mpenzi wako afuate nyuma yako!

Ukifanya hivyo, itakusaidia kuwa na uamuzi sahihi katika kila ufanyalo
na kuwa na uhakika na mambo yako yajayo. Hiyo ina maana kuwa, hata
kama mwanamume unayetaka kuanzisha naye uhusiano ana pesa nyingi kiasi
gani, lakini usizihesabu kama zenu, bali zake!

Utakapokuwa na mtazamo wa kuangalia maisha yako yajayo, utajiweka
katika nafasi nzuri kiakili na kutoruhusu uharibifu wa mwili wako,
hasa kama mpenzi huyo alikuwa na nia ya kushiriki na wewe mapenzi
kisha kukuacha.

USIMWONGOPEE…

Katika uhusiano na mapenzi, udanganyifu ni moja katika ya sumu kali
sana zitakazoweza kuharibu kabisa mapenzi yenu. Katika kikao chenu cha
kwanza, mnapozungumza juu ya matarajio yenu ya baadaye katika uhusiano
wenu huo mchanga, hupaswi kabisa kudanganya.

Anapokuuliza juu ya wapenzi wako waliotangulia mweleze ukweli bila
kumficha. Ingawa kama ulikuwa na idadi ya wapenzi zaidi ya watano,
usimwambie kwa kuwa inawezekana akakuchukulia kama mapepe!

Mwombe naye awe mkweli kwako, usiruhusu uongo kabisa, ni sumu kali
sana ya mapenzi. Mweleze athari za uongo katika mapenzi na umtake awe
wazi kwa kila kitu kinachotokea katika maisha yake.

Mathalani una tatizo la msisimko wa mapenzi, ni vyema ukimwambia
mapema. Pia inawezekana ukikaribia kufika mshindo, unafedheheka au
unazimia, ni vizuri kumwambia mapema ili aamue kusuka au kunyoa!

ELEZA  HISIA ZAKO

Hapa hutakiwi kuogopa, kwa sababu ndio mhimili wa penzi lenu changa,
mwambie mapema kuwa hupendi disko ila unapenda kwenda beach, au
mwambie unapenda sana kunywa pombe au hutaki kusikia habari za pombe.
Hapo utakuwa umewasilisha hisia zako kwa uwazi.

Bila shaka mpenzi wako mpya atakujua ulivyo na haitakuwa kazi ngumu
kufanya yale unayoyapenda na kuacha yale ambayo anatambua kabisa
huyapendi.

Hebu fikiria kidogo kuhusu hili, upo na mpenzi wako mahali fulani,
kwenye mfuko wake wa shati ana pakiti zima la sigara, anachokifanya ni
kuchomoa moja baada nyingine, basi anatoa mimoshi mtindo mmoja!

Ni jambo linalokuudhi, lakini unashindwa kumweleza, hata kama
ukimweleza, atalichukuliaje? Bila shaka itakuwa ni matatizo kwa sababu
ataona unamharibia starehe yake kama sio kumwingilia maisha yake.

Lakini kama mngekuwa wazi tangu mapema haya yote yasingetokea.
Angeelewa wewe unahitaji nini kutoka kwake na yeye anahitaji nini
kutoka kwako, ungefahamu hapendi nini naye angejua unachukia nini, huo
ndio umuhimu wa kuwa wawazi katika hatua za mwanzo kabisa za uhusiano
wenu.

Bado zipo hatua nyingine muhimu, tutaziona wiki ijayo.

Je, unapenda kupata masomo haya zaidi kupitia kundi letu la WhatsApp?
Karibu inbox na useme tu unataka kuunganishwa kundi la Love Moment,
nasi tutakuunganisha ukutane na marafiki wengi.

Pasaka njema!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, ameandika vitabu
kama True Love, Let’s Talk About Love, Maisha ya Ndoa. Kwa sasa ametoa
kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here