Home Michezo Kimataifa Hawa nao waliitikisa La Liga wakiwa wadogo

Hawa nao waliitikisa La Liga wakiwa wadogo

1414
0
SHARE

MADRID, Hispania

KWA sasa Real Madrid wanafurahia uwepo wa mshambuliaji wao kinda, Vinicius Junior, ambaye kiwango chake kimewafanya mashabiki wa miamba hao wa Hispania kuamini bado wana uwezo wa kufanya vizuri msimu huu.

Licha ya kwamba ndio kwanza ana umri wa miaka 18, Mbrazili huyo amekuwa akicheza kwa kujiamini na akiwa ameyazoea haraka maisha mapya nchini Hispania.

Ipo mifano mingine ya wachezaji walioitikisa La Liga katika mechi zao za kwanza, tena wakiwa na umri mdogo.

Raul Gonzalez

Kila mtoto anayepelekwa kwenye akademi ya Real Madrid, ni lazima atajiwe majina ya wachezaji wakubwa waliopitia hapo na kuacha historia, mmojawapo ni Raul.

Mhispania huyo alicheza mechi yake ya kwanza La Liga akiwa na umri wa miaka 17 na miezi minne, wakati huo Madrid ikiwa chini ya kocha Jorge Valdano.

Kiwango alichokionesha kwenye mchezo wake huo wa kwanza kilikuwa ni cha kuridhisha na mpaka anaondoka Santiago Bernabeu, alishajizolea heshima kubwa.

Lionel Messi

Nyota huyo wa Barcelona alianza ‘uchawi’ wake kwenye soka akiwa na umri wa miaka 17 tu.

Ulikuwa ni mtanange wa La Liga, Barcelona wakiwa wageni wa Albacete kwenye dimba la Carlos Belmonte, ambako Messi alionesha kwamba yeye ni mchezaji wa aina gani.

Messi hakutaka mchezo huo umalizike kwa historia ya kwamba ilikuwa ni mechi yake ya kwanza tu, bali alifunga bao na kuwaaminisha watu kuwa mfalme mpya wa Barca amezaliwa.

Iker Casillas

Ni jina kongwe kati ya wakongwe wa Hispania.

Historia yake alianza kuiandika katika dimba la San Mames, alikocheza mechi yake ya kwanza Real Madrid ilipochuana na Athletic Bilbao, akiwa ndio kwanza na umri wa miaka 18.

Uwanja huo ndio uliotengeneza jina lake na kuwa mlinda mlango wa kuheshimika si tu Madrid, bali hata katika timu yake ya taifa, Hispania.

Xavi Hernandez

Mechi ya kwanza ya kiungo huyo mahiri kwa kupiga pasi za uhakika katika kikosi cha Barcelona, ilisimamiwa na kocha, Louis Van Gaal.

Kipindi hicho, Xavi alikuwa kijana mbichi wa miaka 19 tu.

Hata hivyo, safari yake ndani ya Barca ilianza kwa changamoto na kuna wakati alitaka kuikacha timu hiyo.

Andres Iniesta

Iniesta atakumbukwa kwa mambo yake makubwa aliyofanya akiwa na jezi ya Barcelona.

Alianza kuitumikia Barca akiwa na umri wa miaka 18, lakini na yeye alikuwa kama Xavi, wote walianza taratibu kuonesha maajabu yao.

Alianza kuichezea Barca kwa mara ya kwanza La Liga chini ya Van Gaal dhidi ya Mallorca akiwa na umri wa miaka 18 tu.

Sergio Ramos

Beki huyo alianza soka lake mwaka 2001, lakini miaka minne baadaye ndio kiwango chake kilipoonekana na Madrid akiwa na timu ya Sevilla.

Madrid ilimnyakua Ramos wa miaka 19 akiwa na kiwango cha hali ya juu, kiwango ambacho kiliheshimika hata na kocha wa zamani wa Hispania, Luis Aragones.

Licha ya kwamba ni beki, Ramos pia ni mfungaji mzuri wa mabao na pengine ndio uwezo uliomfanya aitwe timu ya taifa akiwa na umri wa miaka 18.

Isco

Kocha wa sasa wa Arsenal, Unai Emery, ndiye aliyeanza kumtumia kiungo huyo kwenye timu yake ya wakubwa Valencia, licha ya kwamba alikuwa mdogo sana.

Umri wake wa miaka 18 haukumzuia Isco kuonesha kipaji chake na alianza kumsumbua Emery kwa kutaka nafasi nyingi za kucheza, ndipo alipomwacha aende zake Malaga.

Huko alifanya makubwa na ghafla, Real Madrid wakamnasa, kilichofuata ni historia.

Saul Niguez

Ilikuwa ni Aprili 21, 2013, siku ambayo kiungo huyo alianza kuitumikia Atletico Madrid akiwa na umri wa miaka 19, akichukua nafasi ya Koke kwenye mtanange wa La Liga dhidi ya Sevilla.

Licha ya kwamba alicheza kwa dakika mbili tu kwenye mchezo huo, lakini ndio ulikuwa mwanzo wa safari yake ya mafanikio akiwa na Atletico.

Marco Asensio

Kiungo mshambuliaji huyo wa Real Madrid alianza kuonesha makeke yake La Liga akiwa na umri wa miaka 19 tu, wakati huo akiwa Espanyol kwa mkopo.

Kuanzia hapo hadi kufikia sasa, Asensio ameendelea kudhihirisha kuwa amekomaa kwa ajili ya kuitumikia timu ya Madrid.

Thiago Alcantara

Ni Pep Guardiola aliyempa kiungo huyo nafasi ya kwanza ya kuichezea Barcelona akiwa na umri wa miaka 18, umri mdogo zaidi ya Xavi na Iniesta walipoanza kuitumikia timu hiyo.

Kabla ya Guardiola kumchukua na kumtumia kwenye timu ya Bayern Munich, Thiago alionekana kwamba angekuwa mrithi wa Xavi, lakini hakuweza kufanya kile alichotabiriwa.

Samuel Eto’o

Straika huyo matata alianza kuichezea timu ya Real Madrid akiwa na umri wa miaka 18 na mwezi mmoja, chini ya kocha Mholanzi, Guus Hiddink.

Hata hivyo, hakuweza kudumu Madrid ambapo alitolewa kwa mkopo mara kadhaa kabla ya kununuliwa na Barca akiwa kwenye timu ya Real Mallorca kwa mkopo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here