SHARE

LONDON, England

MIKE Riley, pengine watakaomkumbuka  mwamuzi huyo ni wale waliofuatilia Ligi Kuu England kuanzia miaka ya 2000 hadi 2010. Ni mmoja kati ya viongozi watatu wa juu katika bodi inayosimamia waamuzi nchini England.

Nchini kwake, ambako Ligi Kuu (EPL) ndiyo inayoongozwa kufuatiliwa zaidi duniani, kuna ile teknolojia inayoteka mijadala, ambayo ni VAR.

Na katika mwendelezo wa mijadala hiyo ambayo kimsingi ni mapokeo ya mashabiki juu ya teknolojia hiyo ya kumsaidia mwamuzi wa kati, Riley naye ametoa kauli inayotokana na rekodi za hadi kufikia sasa.

Teknolojia hiyo mpya imevurunda. Kauli hiyo ni kwa mujibu wa Riley, kwamba hadi kufikia wikiendi hii VAR ilikuwa imeshapinga maamuzi manne makubwa ambayo yalikuwa ni sahihi.

Ni matokeo yaliyokuja katikati mwa presha kubwa kutoka kwa mashabiki na wachambuzi ambao wamekuwa wakitaka VAR itazamwe upya au kusitishwa hadi itakapokuwa bora kutumika tena.

Katika ripoti iliyochapishwa na gazeti la Daily Mail, haya hapa ndiyo maamuzi manne makubwa yaliyofanywa na marefa wa kati, lakini VAR iliyapinga.

“Hali ni mbaya. VAR imekuwa ikiingilia hata maamuzi sahihi ya refa wa kati na kutoa maamuzi yasiyo sahihi,” anasema Riley.

“Ingawa ni jambo la kawaida kutokea. Ni sehemu ya tukio la kuelewa kipi kimetokea wazi na katika mazingira yanayoeleweka.

“Tazama nchi nyingine zinazotumia VAR, zote zinapitia kwenye kipindi cha kujifunza. Na sisi tuko kwenye nyakati hizo pia,” anasema.

Ripoti hiyo ilimaliza kwa kusema kuwa VAR ilikosea kulikataa bao la dakika za lala salama lililofunwga na Sokratis Papastathopoulos wakati Arsenal ikichuana na Crystal Palace mwezi uliopita, na timu hizo kufungana mabao 2-2.

Iliongeza kuwa, Brighton haikuwa na haki ya kuzawadiwa penalti dhidi ya Everton kwenye mchezo wa mwezi uliopita licha ya Michael Keane kumkwatua Aaron Connolly ndani ya 18.

Brighton walifanikiwa kufunga bao kwa mkwaju huo wa penalti na kushinda mabao 3-2.

VAR pia iliamua penalti baada ya winga wa Man Utd, Daniel James ‘kuchezewa faulo’ na beki wa Norwich, Ben Godfrey, au ile ya Gerard Deulofeu wa Watford kuanguka chini wakati akiwania mpira na Jorginho wa Chelsea.

Hata hivyo, kabla ya VAR kuingilia matukio hayo, tayari waamuzi wa ndani walishakataa kutoa penalti na imeelezwa kuwa walikuwa sahihi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here