SHARE

MANCHESTER, England

KLABU zingine barani Ulaya zimebakisha wiki moja kabla ya dirisha la usajili kufungwa, huku dirisha hilo likitarajiwa kufungwa Septemba 2, mwaka huu duniani kote.

Tayari sajili mbalimbali zimefanyika mfano kwa nyota hawa Eden Hazard, Joao Felix, Antoine Griezmann, Nicolas Pepe na Harry Maguire, wote wameondoka katika klabu zao kwa fedha nyingi zilizoweka rekodi na kinyume chake.

Lakini wiki iliyopita, tetesi zilikuwa nyingi kuhusu mastaa ambao wanahusishwa kuhama timu zao kama Paul Pogba, Neymar, Gareth Bale, Alexis Sanchez na wengine wengi.

Nani ataondoka au kusalia kwenye klabu zao, ikiwa wiki moja imebaki ya usajili kufungwa?


ALEXIS SANCHEZ

Inaonekana Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer alishafanya maamuzi juu ya Alexis Sanchez, ambaye anahusishwa kutakiwa kwa mkopo na Inter Milan.

Kama dili hilo likikamilika, nyota huyo raia wa Chile ataungana na straika wa zamani wa Manchester United, Romelu Lukaku ambaye inadaiwa anamshawishi kujiunga na klabu hiyo yenye maskani yake San Siro.

Hata hivyo, imefahamika mshahara wa pauni 500,000 ambao Sanchez analipwa na Manchester United ni kikwazo kwa Inter Milan kushindwa kufikia makubaliano, lakini kuumia kwa Anthony Martial kunaweza kubadili maamuzi ya Solskjaer na kumrudisha haraka kikosini winga huyo aliyewahi kucheza Barcelona na Arsenal.

NEYMAR

Majeruhi ya Edinson Cavani na Kylian Mbappe yanaweza kuwafanya PSG wasifikirie kabisa kumuuza Neymar ambaye anahusishwa kurudi Barcelona na kutakiwa na Real Madrid.

Barcelona na Real Madrid zote zipo tayari kupigana vikumbo kwa ajili ya winga huyo raia wa Brazil, lakini PSG walipiga chini ofa za klabu hizo.

Neymar alijiunga na PSG kwa dau la pauni milioni 196, mwaka 2017, inatajwa kuwa mabingwa hao wa Ufaransa wanataka kiasi kama hicho cha pesa ili kumwachia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27.

PAUL POGBA

Pogba alikuwa mfungaji bora wa Manchester United msimu uliopita, lakini kiwango alichokionyesha katika michezo ya mwisho ya msimu huo iliwafanya mashabiki kuingia kwenye utata mkubwa kwa nyota huyo kuonyesha kiwango cha ovyo.

June mwaka huu, Pogba aliweka wazi lengo lake la kutaka kuondoka kwa mabingwa hao wa zamani wa England, akidai kuwa anatafuta changamoto mpya baada ya kuwa ndani ya kikosi hicho kwa misimu mitatu.

Baada ya kukosa penalti dhidi ya Wolverhampton wiki iliyopita, ilizidi kuchochea zile tetesi za kutakiwa na Real Madrid, huku baadhi ya mashabiki wakishutumiwa kwa maneno ya ubaguzi kwa kiungo huyo wa Ufaransa.


CHRISTIAN ERIKSEN

Mauricio Pochettino alimpa nafasi mara moja tu Eriksen katika michezo mitatu waliyocheza mpaka sasa ya Ligi Kuu England.

Kama Pogba, hata Eriksen aliweka wazi lengo lake la kutaka kuondoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake Uwanja wa Tottenham, huku mkataba wake ukielekea mwishoni msimu huu.

Taarifa zinadai kuwa kiungo huyo atasajiliwa na Real Madrid kama wakishindwa kuipata saini ya Pogba ambaye ni chaguo la kwanza la Zinedine Zidane.


PAULO DYBALA

Kama lilivyosekeseke la Neymar, basi, Dybala aliishia kuwa mchezaji wa akiba tu katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Italia dhidi ya Parma, ambao Juventus walishinda bao 1-0.

Kuwasili kwa Cristiano Ronaldo msimu uliopita, ilikuwa habari mbaya kwa Dybala ambaye alikuwa mchezaji tegemeo wa Juvetus.

Inaaminika kocha wa kikosi hicho, Maurizio Sarri yupo tayari kumfungulia milango ya kuondoka nyota huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 25.

Tottenham na Manchester United ziliingia katika vita ya kuwania saini yake, lakini ziliishia patupu, hawakufanikiwa kumsajili nyota huyo, lakini bado anahusishwa katika mabadilishano na PSG kwa ajili ya kumnasa Neymar.

LUKA JOVIC

Real Madrid wana wachezaji wengi, licha ya straika huyo raia wa Serbia kujiunga akitokea Eintracht Frankfurt ya Ujerumani, Jovic bado anaweza kuruhusiwa kuondoka kwa mkopo.

Mabao yake alipokuwa Frankfurt yalikuwa msingi wa klabu hiyo kutinga mpaka nusu fainali ya Europa, lakini Zidane si shabiki wa straika huyo mwenye umri wa miaka 21.

Jovic alisema hayupo tayari kuondoka ndani ya kikosi hicho cha mabingwa wa zamani wa Hispania, lakini kama klabu hiyo itamtoa kwa mkopo atakubali kuondoka.


GARETH BALE

Mahusiano ya Zidane na Bale yanaonekana kurejea kuwa mazuri, japo kocha huyo wakati wa maandalizi ya msimu alisema bora winga wake aondoke ndani ya kikosi hicho.

Lakini baada ya dili la kwenda China kufeli kujiunga na Jiangsu Suning, Bale amefanikiwa kuanza mechi zote mbili za Ligi Kuu Hispania.

Pamoja na mahusiano yao kuanza kuimarika, bado Bale anaweza kuondoka Sanyiago Bernabeu ikiwa wiki moja tu imebaki kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

JAMES RODRIGUEZ

Sakata lake linafanana na Bale, James amechaguliwa na Zidane katika michezo ya msimu huu, licha ya mahusiano yao kwenda mrama.

Kiungo huyo raia wa Colombia alikuwa Bayern Munich kwa mkopo wa misimu miwili kabla ya kurejea Santiago Bernabeu, hata hivyo, Atletico Madrid walitajwa kutaka kumsajili mchezaji huyo.

Pia, Carlo Ancelotti ambaye aliwahi kumfundisha kiungo huyo ndani ya kikosi cha Real Madrid, alithibitisha kuwa Napoli wapo kwenye mpango wa kuwania saini ya James, lakini inaonekana kuwa ngumu kwa klabu hiyo ya Italia kukamilisha dili hilo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 anasumbuliwa na majeraha ya kigimbi, hilo halimfanyi ashindwe kuondoka katika viunga vya Santiago Bernabeu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here