Home Michezo Kimataifa Hii ndiyo timu ya wiki Ligi Kuu England

Hii ndiyo timu ya wiki Ligi Kuu England

540
0
SHARE

MAREGES NYAMAKA NA MITANDAO

HADI kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita, tayari timu zote za Ligi Kuu ya England zilikuwa zimekwishacheza jumla ya michezo mitano, huku Manchester City ikishika usukani baada ya kushinda mechi zake zote tano bila kupoteza wala kutoka sare mechi hata moja.

Inafuatiwa kwa karibu na Everton inayoshika nafasi ya pili, Tottenham ya tatu, huku Arsenal, Chelsea, Liverpool na Manchester United zikiwa katika nafasi ya nne, tano, sita na saba kwa mfuatano.

Baada ya kupigwa kwa mechi hizo, tayari wachambuzi mbalimbali wamekwishaanza kuvichambua vikosi vya timu tofauti tofauti kupitia mitandao ya kijamii, huku wakipima ubora wa wachezaji.

Mbali na hao, pia mashabiki wa timu pinzani kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakitumia mwanya huo kushambulia kiwango cha mchezaji ghali duniani anayekipiga katika kikosi cha Mashetani Wekundu, Manchester United, Paul Pogba, ambaye anaonekana kuisaidia vyema timu yake katika kupata matokeo mabaya ambapo ndani ya siku nane tu timu hiyo imeambulia vichapo vitatu mfululizo.

Kupwaya kwa Manchester United, inayonolewa na kocha Mreno mwenye ‘maneno ya shombo’, Jose Mourinho, kumeifanya klabu hiyo kuingia kwenye rekodi hasi ambapo takwimu zinaonyesha hakuna mchezaji wa timu hata mmoja ambaye ameweza kuingia kwenye kikosi bora cha wiki kwenye Ligi Kuu ya England licha ya kuwa na nyota wenye majina makubwa kama Zlatan Ibrahimovic, Wayne Rooney pamoja na Pogba.

Baada ya mechi hizo za wikiendi iliyopita zilizoongozwa na mechi kali ya wababe wawili Chelsea na Liverpool, iliyomalizika kwa Liverpool kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya The Blues katika dimba la Stamford Bridge, makala hii inakuchambulia nyota waliong’ara na kuwafanya waingie kwenye timu ya wiki.

 

KIPA

Jordan Pickford (Sunderland)

Mlinda mlango huyu wa Sunderland mwenye umri wa miaka 22, licha ya timu yake kupoteza mchezo kwa bao 1-0 mbele ya Tottenham, bado aliibuka shujaa kwa kuondoa hatari zaidi ya nane langoni kwake kutoka kwa washambuliaji matata kama Harry Kane na Toby Alderweireld.

Nyota huyu aliyepewa nafasi na kocha wa sasa wa Sunderland, David Moyes, ameonekana kujiamini na kufanya vyema langoni kwake akichukuwa nafasi ya kipa chaguo la kwanza, Vito Mannone, ambaye ni majeruhi.

 

MABEKI

Virgil van Dijk (Southampton)

Dijk, raia wa Uholanzi aliyenunuliwa na Southampton akitokea Celtic 2015, ameonekana kuwa mgumu kwelikweli na kuwazuia washambuliaji kupita ukuta wake kirahisi. Mwishoni mwa wiki alicheza kwa kiwango cha juu akifanikiwa kwa zaidi ya asilimia 95, akipiga pasi sahihi 55 na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Swansea City kwa kumzuia vilivyo mmoja wa mastraika hodari, Fernando Llorente, kusogelea lango lake.

 

Scott Dann (Crystal Palace)

Dann, ambaye ni beki wa Crystal Palace, aliimarisha ulinzi kwa juhudi ya hali ya juu na kuwafanya viungo wa timu yake wapige pasi nyingi mbele kwenda kwa mafowadi ambapo walifanikiwa kuwapa wapinzani wao Stoke City, mvua ya mabao 4-1.

Licha ya Stoke kuwa na mshambuliaji wao msumbufu mwenye uwezo wa kutikisa nyavu kwa staili yoyote, Wilfried Bony, lakini hakuweza kuleta madhara makubwa kwenye beki hiyo kutokana na uimara.

 

Aleksandar Kolarov (Manchester City)

Aleksandar Kolarov ameanza msimu vizuri chini ya kocha wake mpya, Pep Guardiola, akiingia kwenye kikosi cha kwanza na kuonyesha uwezo wa juu kwa kushirikiana na John Stones na kutoonyesha pengo lolote la nahodha, Vincent Kompany, ambaye ni majeruhi.

Kolarov anayetumia mguu wa kushoto mara nyingi, katika mechi chache zilizopita ameonyesha umahiri mkubwa wa kumiliki mpira kuliko kipindi chochote huko nyuma.

Uwezo wa kupiga pasi sahihi na kuanzisha mashambulizi kwa haraka ni kitu kingine kipya kilichoongeza thamani yake ndani ya uwanja.

Akitokea upande wa beki ya kushoto na kutiririka kama winga, alikuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Bournemouth ambapo hadi dakika 90 zinamalizika, timu yake ikishinda mabao 4-1, alionekana kung’ara baada ya kutoa pasi 88 sahihi zilizopigwa na nyota kadhaa wa Manchester City.

 

VIUNGO

Nacer Chadli (West Brom)

Ni kiungo Mbelgiji aliyefanya maamuzi magumu ya kuhama Tottenham na kwenda West Brom kipindi cha usajili majira ya kiangazi kwa kitita cha pauni milioni 13. Chadli, mwenye kupiga mashuti ya nguvu kwa umbali mrefu ameingia kwenye orodha ya wachezaji wanaounda timu ya wiki baada ya kusaidia timu yake hiyo mpya kwa kiasi kikubwa katika eneo la kiungo.

 

Kevin De Bruyne (Man City)

Kevin De Bruyne kwa muda mchache amekuwa mchezaji tegemeo kikosini hapo kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha akipewa jukumu la kucheza kama mchezaji huru na kocha wake Pep Guardiola ndani ya kikosi.

Mbelgiji huyo alikuwa wa kwanza kufunga bao katika mchezo wao wa mwishoni mwa wiki dhidi ya Bournemouth akitumia vyema pasi matata ya Raheem Sterling katika ushindi wa mabao 4-1.

 

Etienne Capoue (Watford)

Moja ya bao lililofungwa mwishoni mwa wiki ilikuwa kutoka kwa kiungo huyu wa Watford aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa wa Manchester United, David de Gea, baada ya mchezaji mwenzake kupiga krosi akiwa amempokonya mpira Athony Martial.

Etienne Capoue, mwenye umri wa miaka 28, alimiliki mpira kwa kiasi kikubwa hasa katika eneo la katikati ya dimba kushinda nyota wa Man United, Paul Pogba, ambapo alipiga mipira sahihi kwa mafowadi wake.

Kiungo huyo alikuwa mchezaji pekee aliyepokonya mipira mingi akifanya hivyo mara tano kuliko mchezaji yeyote.

 

Jordan Henderson (Liverpool)

Jordan Henderson, anayecheza sambamba na viungo wenzake wawili, Gini Wijnaldum na Adam Lallana katika mfumo wa 4-3-3, alikuwa msaada kwa timu yake iliyowalaza chali Chelsea katika dimba lao la nyumbani, Stamford Bridge, kwenye ushindi wa 2-1, yeye mwenyewe akifunga bao la ushindi la umbali mrefu.

Mwingereza huyo usiku wa Ijumaa katika mchezo huo alipiga pasi 68 ambazo asilimia 88, zilikuwa sahihi, zikifika kwa mlengwa na kukata mirija kabisa ya Chelsea kutoka kwa wachezaji wake wenye madhara kama Oscar na Eden Hazard.

 

Andros Townsend (Crystal Palace)

Andros Townsend, aliyepata uhamisho wa kwenda Crystal Palace kwa kitita cha pauni milioni 13 akitokea Newcastle United, ameingia kwa haraka katika mfumo wa kocha wake, Allan Pardew, akishirikiana na Wilfred Zaha, kuiwezesha timu yake kupata ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Stoke City.

 

WASHAMBULIAJI

Islam Slimani (Leicester City)

Ukiwa ni mchezo wake wa kwanza kuichezea Leicester City dhidi ya Burnley, kama timu yake mpya msimu huu ndani ya Ligi Kuu England, ‘movement’ zake straika huyo asili katika namba 9 ameonekana ni aina ya wachezaji wanaoendana na mfumo wa timu hiyo.

Akiwa katika kasi yake ya kupachika mabao wavuni, alifanya hivyo katika mchezo huo akiingia kimiani mara mbili.

Uwezo wake huo unatajwa kuwa unaweza kuongezeka zaidi endapo watashirikiana vyema na Jamie Vardy na hivyo kuweza kuvuna mabao ya kutosha msimu huu.

 

Alexis Sanchez (Arsenal)

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, anamuangalia Alexis Sanchez kama mchezaji tegemeo, akicheza vema na kinda, Alex Iwobi.

Sanchez  alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kilichoweza kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 ugenini dhidi ya Hull City, huku yeye pia akihusika katika mabao hayo. Kwa asili Sanchez ni winga mwenye uwezo wa kucheza

zaidi upande wa kulia, lakini kwa siku za hivi karibuni Wenger amekuwa akimtumia kama mshambuliaji wa kati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here