SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

JUNI 2, 2018, wadau wa soka katika Jiji la Arusha walipata burudani ya kutosha baada ya kushuhudia mtanange mkali wa fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho, maarufu kama Azam Sports Federation Cup, kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Singida United.

Ilikuwa burudani kwa wadau wa soka wa Arusha, kwani walikaa muda mrefu bila kushuhudia mchezo wa timu kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu kutokana na timu zao, hasa AFC, kushuka daraja miaka mingi.

Tangu AFC ishuke daraja msimu wa 2010/11, imepita karibu miaka nane mashabiki wa Jiji hilo wakikosa burudani, ndiyo maana haikuwa kazi ngumu kuujaza Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kushuhudia mtanange huo wa fainali, kwani walikuwa na hamu ya siku nyingi kuona timu kubwa zikifika Arusha.

Tangu kuchezwa kwa mchezo huo mpaka leo hii ni miezi minne imepita, lakini cha ajabu ni kwamba Mtibwa Sugar, ambao walitwaa ubingwa huo, waliibuka na ushindi wa mabao 3-2, hawajapewa zawadi zao.

Ilikuwa Mtibwa Sugar walambe milioni zao 50 za Kitanzania, lakini wamejikuta wakiambulia hundi peke yake, huku mzigo wao kamili ukiendelea kushikiliwa na wahusika.

Mpaka sasa haijafahamika wazi kwamba ni Azam ambao ni wadhamini wa michuano hiyo au Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambao wamezikalia fedha hizo, kwani pande zote zimekuwa kimya kama hawajui nini kinaendelea.

Jana asubuhi nilimpigia simu rafiki wa wengi, Thobias Kifaru, Msemaji wa Mtibwa Sugar, ili kusalimiana tu, lakini nikaamua kugusia kuhusu zawadi zao kama wamezipata ama la, akaniambia bado wanasubiri haki yao hiyo.

Katika mazungumzo yetu hayo, Kifaru aliniambia kwamba wakati wanakwenda kwenye mchezo huo waliwaambia wachezaji wao kama watatwaa ubingwa huo, wangewapatia Sh milioni 40, kati ya hizo milioni 50 za zawadi.

Kifaru akanidokeza kwamba, mpaka sasa wanavyowaona wachezaji wao ni kama wamekata tamaa, hata kwenye michezo ya Ligi Kuu, kwani wanafikiri hata wakitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jasho lao linaweza kupotea kusikojulikana.

Hili ambalo limefanywa na TFF na Azam kutokuwalipa Mtibwa Sugar haki yao ni kurudisha nyuma maendeleo ya michezo nchini. Nawataja Azam kwa sababu kama wametoa fedha hizo za zawadi wangejitokeza hadharani waseme.

Kama TFF nao hawajapewa hizo fedha za zawadi na Azam, wanatakiwa wajitokeze hadharani waseme ili kuepuka kurushiwa lawama. Kama pande zote hizo mbili zikikaa kimya tutajua wote ni wababaishaji katika suala hilo.

Hili nalo ni moja ya sababu zinazoufanya mpira wetu urudi nyuma, kwani wachezaji hao hao ambao wanacheleshewa zawadi zao, ndio haohao wanaoitwa kwenye timu ya Taifa na kutakiwa kufanya vizuri, kweli hilo linawezekana?

Wachezaji wa Mtibwa Sugar hawawezi kucheza kwa ari, kwani wanaona kabisa milioni zao 40 walizoahidiwa na uongozi baada ya kutwaa ubingwa wa Azam, hawajazipata, huku siku zikizidi kuyoyoma. Hili haliko sawa kabisa, ni sawa na unyonyaji.

Wachezaji hao walipoahidiwa na uongozi wao kwamba wangepata milioni 40 ili wagawane, ni dhahiri kila mmoja alishapanga mipango yake kuwa katika mgawo huo kile atakachokipata atakitumia namna gani, lakini wameshakwamishwa.

Ili mpira wetu wa miguu upige hatua, kuna mambo mengi sana ya kurekebisha, likiwamo hili la TFF na wadhamini kutoa zawadi kwa muda mwafaka kuliko timu inashinda leo halafu haki zao wanazipata baada ya miezi minne na kuendelea.

Inakatisha tamaa na inasikitisha sana kuona Mtibwa Sugar wakiendelea kusubiri zawadi zao na kama TFF hii itafanya mambo yake kienyeji hivi, bila shaka tutaendelea kupiga hatua moja mbele na nyingine kumi nyuma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here