SHARE

MANCHESTER, England


KAMA ilivyo kawaida ya Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, anayependa kutumia ‘staili’ ya kupaki basi wakati timu yake inacheza, huku mashabiki wengi wakionekana kutofurahishwa na hali hiyo iliyopo.

Lakini tofauti na ‘staili’ hiyo ya kupaki basi inayotumiwa na Mourinho, Manchester United ni moja ya timu zinazotumia basi lenye thamani kubwa zaidi ya nyingine.

Katika safari wanazokwenda kucheza viwanja vya ugenini Manchester United hutumia basi lao linalotajwa kuwa na thamani ya pauni 400,000 (Sh bilioni 1.18 za Kitanzania), ikiwa basi hilo linafahamika kwa jina la Van Hool TDX27 ASTROMEGA, yanayotengenezwa kutoka nchini Ubelgiji.

Wachezaji kama Paul Pogba, Romelu Lukaku, Jesse Lingard, Marcus Rashford na wengine hupenda kuishi vizuri wanapokuwa nje ya uwanja, wanatajwa kuwa na furaha sana pindi wanaposafiri na basi hilo.

Sababu ni moja ya mabasi yenye uwezo mkubwa wa kuwafanya kupata huduma zao zote wanapokuwa ndani yake ikitambulika kuwa wachezaji wanapofika sehemu husika wanakuwa hawana uchovu.

Jinsi basi hilo lililovyotengenezwa linawafanya wachezaji kuwa salama hata ikitokea wanashambuliwa na mashabiki hawawezi kuathirika.

Mwaka 2016 Manchester United walikwenda na basi lao katika Uwanja wa Upton Park, uliokuwa unatumiwa na West Ham, lakini kabla ya kufika uwanjani walishambuliwa na mashabiki wa wapinzani wao kwa kurushiwa chupa.

Lakini hakukuwa na mchezaji aliyeumia wala kupata jeraha lolote, unajua kwanini? Rahisi tu, basi hilo lilikuwa na kioo cha akiba ambacho hakiwezi kuruhusu shambulizi liingie ndani kuathiri abiria.

Kwa hiyo zile fujo zilizosababishwa na mashabiki wa West Ham ziliishia kwenye kioo cha akiba baada ya kuvunja kilichopo juu.

BASI HILO LIKOJE?

Van Hool TDX27 ASTROMEGA lina urefu wa futi 46.27 (mita 14.105), kimo cha futi 13 (mita 4) na upana wa futi 8.36 (mita 2.5), huku spidi yake ikiwa mwisho 70mph.

Basi hilo lina sehemu za juu na chini linalowezesha wachezaji na wengine kukaa, juu kuna siti 29 na chini zipo tisa.

Kubwa zaidi ndani yake kuna TV 45 zinazowawezesha abiria kuangalia, sehemu ya kupikia, friji na mashine ya kutengeneza kahawa.

Jambo la kuvutia zaidi basi hilo lina WiFi ambayo inawezesha kutumia intaneti bila tatizo lolote, huku wachezaji kama akina Pogba wakitumia na kuweka katika akaunti zao za mitandao ya jamii.

Kama lilivyokuwa na sehemu mbili, yaani juu na chini, basi kwa upande wa chini basi hilo lina sehemu mbili za kupikia ambazo zina jiko la ‘oven’, lenye thamani ya pauni 770 (Sh milioni 2.27 za Kitanzania), Panasonic microwave yenye thamani ya pauni 630 (milioni 1.86 za Kitanzania) na mashine ya kutengenezea kahawa ambyo ni pauni 540 (Sh milioni 1.57 za Kitanzania).

Mwishoni kabisa kuna choo na sehemu ya kuoga zilizobuniwa kama kwenye usafiri wa ndege, si mabasi yote yanaweza kuwa na mfumo huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here