Home Michezo Kimataifa Hiyo Real Madrid mpya usipime kabisa

Hiyo Real Madrid mpya usipime kabisa

0
SHARE

MADRID, Hispania

MAFANIKIO na historia vinaonyesha ni jinsi gani Real Madrid ni moja ya timu kubwa duniani, kuna klabu chache ambazo zinaweza kushinda na mabingwa hao wa Ulaya mara 13.

Mara zote malengo yao ni makubwa hasa kushinda mataji kila msimu bila kujali uzito wa kombe husika, iwe makombe ya ndani, Ulaya au duniani wataingia miguu yote miwili kushinda.

Lakini msimu uliopita walishindwa kufikia malengo yao japo ni mapema sana kusema wataendelea kuwa hivyo kwa kipindi kirefu zaidi, ingawa kwa aina ya matokeo waliyoyapata ilitoa picha mbaya kwa mashabiki wa Real Madrid.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya walifungwa na CSKA Moscow ya Urusi katika michezo yote miwili ikiwa ni mara ya kwanza kwa Real Madrid kufungwa na timu moja hatua ya makundi baada ya miaka mingi kupita.

Kubwa zaidi lililowasikitisha mashabiki wa timu hiyo msimu uliopita, ilikuwa Real Madrid kushindwa kufanya vizuri katika michezo ya uwanja wao wa nyumbani, Santiago Bernabeu.

Pia, walishindwa kusonga mbele katika hatua ya robo fainali baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Ajax na kukatizwa ndoto za kutwaa taji hilo la Ulaya kwa mara ya nne mfululizo.

Msimu uliopita walifukuza makocha wawili, Julien Lopetegui na nafasi yake ilichukuliwa na Santiago Solari  lakini bado mambo hayakuonekana kukaa sawa kwa timu hiyo na kuendelea kufanya vibaya.

Maana yake ni kwamba ndani ya klabu hiyo kuna mambo ambayo inabidi yafanyiwe kazi ili irudi katika kilele cha ubora wake kama zamani, ndio maana Zinedine Zidane amerudi kwa mara nyingine tena na Solari kuondoka.

Makala haya yanakuletea mambo ambayo Real Madrid wakifanya watakuwa na nafasi ya kurudi kwenye ubora wao.

BENZEMA KUONGEZEWA NGUVU

Kipindi cha miaka tisa ambayo Ronaldo alivaa jezi ya Real Madrid alifanikiwa kufunga mabao 451 huku akiwa na wastani wa 1.2 kwa kila bao alilofunga.

Kwa urahisi ni ngumu kupata mbadala sahihi ambaye ataweza kuziba nafasi yake, kuondoka kwake ilitarajiwa kuwa Real Madrid wangesajili straika mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao zaidi ya 30 kwa msimu.

Lakini haikuwa hivyo, Karim Benzema amekuwa mchezaji ambaye hana muendelezo wa kiwango chake mara nyingi anashindwa kuisaidia klabu hiyo pale anapohitajika kufanya hivyo.

Pamoja na kufunga mabao 21 msimu uliopita, bado Benzema ameshindwa kudumu katika kiwango chake, si mchezaji anayeweza kuisaidia Real Madrid msimu ujao.

Wamemaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Hispania, La Liga huku wakifunga mabao 63 ambayo ni machache kwao kwenye misimu mitano ya hivi karibuni.

Ili kurudi katika kilele cha mafanikio lazima wasajili straika ambaye atakuwa na uwezo wa kufunga mabao mengi ikiwa tayari Zidane ameshapata saini ya Luka Jovic aliyekuwa Frankfurt ya Ujerumani.

Pia, wamefanikiwa kumng’oa Eden Hazard ndani ya kikosi cha Chelsea, yote hiyo kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo lilishindwa kufanya kazi vizuri msimu uliopita.

Kwa upande mwingine akifukuzia saini za straika wa Bayern Munich, Robert Lewandowski na yule wa Inter Milan, Mauro Icardi.

FALSAFA TOFAUTI

Real Madrid si timu ambayo inajulikana kwa kucheza soka safi na mbinu mara nyingi hubadilika kutokana na makocha.

Zidane alitumia mfumo wa 4-1-2-3 huku akimtumia Casemiro mbele ya mabeki wanne kulinda ngome hiyo ilikuwa rahisi kwao kucheza kwa usawa, yaani wakati wa kushambulia na kuzuia.

Wakati Lopetegui ameichukua timu hiyo, alibadili mfumo wa kucheza na kutumia 4-3-3 huku akihitaji timu hiyo kucheza kwa kumiliki mpira, pia, aliiwafanya wachezaji kucheza kwa kukabia juu kitu ambacho kiliiweka kwenye wakati mgumu kwa wapinzani kutumia nafasi hiyo.

Naye Solari alipofanikiwa kuchukua mikoba ya Lopetegui hupenda kutumia mifumo ya 4-3-3 au 4-2-3-1, mabadiliko hayo yanaifanya timu kushindwa kujengwa kwenye uwiano sawa.

Mabadiliko ya mifumo na majukumu uwanjani yanawaweka wachezaji kwenye wakati mgumu kwani watahitaji kucheza kwa muda ili kuzoea kitu kipya.

Ikiwa hata Zidane ndani ya michezo yake miwili ya hivi karibuni alitumia mifumo ya 4-2-3-1 na 4-3-3, kwa kiasi kikubwa bado wachezaji wake walishindwa kucheza kwa kiwango cha juu.

MAKALI YA MASTAA

Kwa kiasi kikubwa kikosi hicho cha mabingwa wa Ulaya kilikuwa kikibebwa na Ronaldo ambaye mwanzoni mwa msimu huu alitimkia Juventus.

Bado hakuna mchezaji aliyefanikiwa moja kwa moja kuziba nafasi iliyoachwa na nahodha huyo wa Ureno, kwa nyakati tofauti Real Madrid inapitia kipindi kigumu kwa nyota waliobaki kushindwa kucheza kwa kiwango cha juu.

Oktoba mwaka jana, Luka Modric aliweka wazi kuwa hivi sasa hachezi kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa zamani huku akisisitiza anahitaji mapumziko labda uchovu wa fainali za Kombe la Dunia.

Miezi tisa imepita tangu aseme hivyo lakini mpaka sasa mchezaji huyo ameshindwa kucheza kwa kiwango cha juu, bado hayupo kwenye ubora mkubwa.

Toni Kroos ambaye ameongeza mkataba wa miaka minne hivi karibuni inaonekana anacheza kwenye kivuli chake tu, anaonekana amechoka kimwili mpaka akili, unaweza kusema miguu yake haitamani kucheza mpira kabisa.

Gareth Bale amekuwa akiandamwa na majeraha na tena umri wake taratibu umekuwa ukisogea kama ilivyokuwa kwa Marcelo na Sergio Ramos.

Kwa muda mrefu wachezaji wamekuwa tegemeo ndani ya klabu hiyo, tayari vijana kama Dani Ceballos, Valverde na Llorente wanaonekana kufanya vizuri katika michezo yao waliyopata nafasi ya kucheza.

Ni muda wa Real Madrid kuwaamini vijana hao ili kutengeneza kizazi kipya kwa kuwapa nafasi huku wakizungusha kikosi chao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here