Home Michezo Kimataifa Ibrahimovic na ndoto mfu za kuwa Mungu Man United

Ibrahimovic na ndoto mfu za kuwa Mungu Man United

555
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

ARSENAL wanachanja mbuga bwana! Hawataki ujinga kabisa, kwani wanajua wanayo miaka ya kutosha wakiusikia tu ubingwa kwa majirani zao na wao wakibakia kama washiriki watiifu.

Ukiangalia timu za England, bila shaka hutakuwa na la kujiuliza juu ya ile ambayo imeshiriki mara nyingi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Barani Ulaya.

Kwa haraka ukiulizwa hilo swali utaitaja Arsenal, lakini likija lingine wameutwaa ubingwa huo mara ngapi, itabidi uangalie njia ya kulikwepa swali hilo.

Ukiachilia mbali ubingwa wa michuano hiyo ya UEFA, katika Ligi Kuu ya nchini England Arsenal wamekuwa wakiusikia ubingwa kwa Manchester United, Chelsea na Manchester City, lakini wao wamekuwa wakigombea kumaliza nafasi ya nne.

Hata hivyo, msimu huu wanaonekana dhahiri kupania kufuta machozi ya mashabiki wao na hii ni kutokana na kandanda safi lenye matokeo chanya kwao, kwani mpaka sasa wanashika nafasi ya pili, wakiongozwa na Man City.

Wakati Arsenal wao wakitajwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu, kwa upande wa Manchester United hakuna lolote linaloeleweka na badala yake watu wamebakia na ile kauli moja tu ya Zlatan Ibrahimovic.

Wakati Ibra anasajiliwa alitoa kauli ambayo mashabiki wa United waliifurahia, kwamba wamepata mtu sahihi kwa wakati sahihi. Unakumbuka alisemaje? Kama hukumbuki ngoja nikukumbushe, alisema atakuwa Mungu.

Ibra ni mtu mwenye maneno ya shombo kama ilivyo kwa kocha wake, Jose Mourinho, si mtu wa kupima nini anakwenda kukizungumza, bali kile kinachokuja mdomoni mwake hichohicho anakitoa kama kilivyo.

Alichokozwa tu kidogo na mkongwe Erick Kantona, aliyezungumzia habari ya ufalme pale Old Trafford na Ibra bila kuwaza mara mbilimbili akatamka kuwa, anakwenda kuwa Mungu. Yaani hata hakufikiria upana wa neno hilo.

Baada ya neno hilo mashabiki wa United wakakaa mkao wa kula, wakijua kwamba, wamepata mkombozi na timu yao itapata matokeo mazuri waliyoyasubiri kwa muda mrefu tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.

Na kweli alivyoanza kuitumikia timu hiyo akaanza kufunga, hapo ndipo wale mashabiki wake wakaanza kuamini kuwa wamempata Mungu na wala si mfalme kama mwenyewe alivyotamka.

Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo huyu aliyejitabiria Uungu mtu anavyozidi kupotea, hafungi kama alivyosema na wala ule upambanaji  wake hauonekani kama wengi walivyodhani.

Uzuri wa mpira unachezwa hadharani, ambapo kila mmoja anaona. Ukicheza vizuri utasifiwa na utapongezwa, lakini ukicheza vibaya watu watakuongelea kwa ubaya huohuo.

Ni kweli kwamba, mchezaji anaweza asifunge, lakini kiwango anachokionyesha ndani ya uwanja kikatosha kabisa kuamsha shangwe kwa mashabiki, vyote hivyo vinaonekana kuanza kutoweka kwa Ibra.

Umri wa Ibra siyo ule wa akina Jesse Lingard, yeye jioni yake inakaribia, muda wowote anaweza kutangaza kutundika daluga, sasa anapokawia kufikia malengo yake ya Uungu mtu pale Old Trafford, anaweza akawafuata akina Frank Lampard kwenye soka la nchini Marekani bila kuacha chochote kwa timu yake hiyo ya sasa.

Wakati Ibra anatamka maneno hayo alisahau kuwa umri wake unakwenda mbio, alisahau kwamba kuweka historia kubwa kwenye timu yoyote inatakiwa kuwa na muda wa kutosha. Siyo rahisi ufikie hatua ya kujijengea jina kubwa la kuitwa Mungu ndani ya miaka miwili au mitatu.

Mashabiki wa Man United wanasubiri timu yao ishinde na badala yake inatoka tu sare, wanamsubiri aliyejitabiria Uungu mtu afunge na badala yake nafasi za kufunga anazozipata zinayeyuka hivihivi.

Tunaendelea kuomba uhai, tunamuombea pia uhai Cantona mpaka pale Ibra atakapoondoka pale Old Trafford ili tuone kama ataondoka kama Mungu au atatuachaje, maana aliiaminisha jamii ya watu wa mpira kuwa anauweza.

Uzuri ni kwamba, baada ya Ibra kusema atakuwa Mungu, Cantona hakutaka kusema jambo jingine lolote, bila shaka anasubiri mwisho wa maneno hayo, kwani ni maneno mazito yanayotaka ujasiri wa hali ya juu kuyatamka.

Anayeweza kuyatamka maneno hayo ni Ibra peke yake, kwani wengine hata ukiwaambia habari ya kuwa mfalme hawataki, lakini kwa mwenzetu Ibra amekimbilia kutamka neno la kuwa Mungu. Ngoja tusubiri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here